April 5, 2019


MFANYABIASHARA na Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji, anadaiwa kumficha kiungo mkabaji raia wa Ivory Coast, Jean Vital Ourega, ambaye anawaniwa na wapinzani wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo.

Mo amelazimika kumficha staa huyo baada ya kupendekezwa na kocha wao Mbelgiji Patrick Aussems ambaye amewahi kuona uchezaji wake akiwa katika timu ya Karela United ya nchini Ghana na kwamba takribani miezi miwili nyuma aliletwa nchini na wakala wa kocha huyo akiwa mchezaji huru.

Chanzo makini kimelieleza Championi Jumatano kuwa, Ourega ni kati ya wachezaji ambao wanamilikiwa na wakala wa kocha huyo pamoja na beki wa kulia wa Simba raia wa Burkina Faso, Zana Coulibaly, ndiyo maana kocha ana imani naye kwani siku zote amekuwa akihitaji kusajili kiungo mwenye umbo kubwa na mrefu kama yeye.

“Kocha ndiye amemtaka mchezaji huyo aje nchini kwa sababu ni mzuri sana katika kiungo lakini mbali na hivyo anawaniwa na TP Mazembe ambao tayari walikuwa wameshaongea na wakala wake hivyo utaona hata aliporudi kwao baada ya kuja mara ya kwanza viongozi walijua tayari Mazembe wamemsajili.

“Mo amepewa baadhi ya video za mchezaji huyo ili ajiridhishe zaidi kwani malengo yake katika dirisha lijalo ni kusajili watu wa kazi tu na si wakujaribu kama ilivyokuwa huko nyuma, alipoelezwa kila kitu aliridhika na kusema kuwa aliletwa Dar akakae hotelini,” kilisema Chanzo hicho.

Mo ambaye pia anapambana kuhakikisha Simba inatwaa ubingwa wa Bara msimu huu, hesabu zake ni kutengeneza kikosi imara kitakachoingia kiushindani kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao. Bilionea huyo ambaye ana uchungu na Simba anaamini kwamba kikosi atakachokisuka safari hii kitaingia siriazi kimataifa na mashabiki watafurahia soka.

Championi lilipomtafuta meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kuwa suala la kusajiliwa au kutosajiliwa yeye halijui kwa sasa, lakini anachofahamu ni kwamba mchezaji huyo aliwahi kucheza kwenye akademi ya TP Mazembe.

1 COMMENTS:

  1. Mazembe haisajir kwa kwa mtindo huo bun achen kukisahaulishaaa kesho mtatafutana tyuu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic