April 6, 2019


MATOKEO ya sare ya bao 1-1 waliyoyapata Yanga, juzi Alhamisi dhidi ya Ndanda FC, yanazidi kuipa nafasi kubwa Simba ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa watashinda ‘viporo’ vyao vilivyosalia.

Yanga ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, ililazimishwa sare hiyo baada ya kusawazisha bao dakika ya 61 kupitia kwa kiungo wake Papy Tshishimbi aliyefunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Kelvin Yondani.

Kabla ya hapo, Vitalis Mayanga aliitanguliza timu yake ya Ndanda kwa bao la mapema dakika ya 19 akitumia makosa ya walinzi wa Yanga walioonekana kujipanga vibaya kuondoa hatari hiyo ambapo Mayanga alimchambua Yondani, kisha kipa Klaus Kindoki, kabla ya kufunga bao hilo.

Yanga itajilaumu kukosa ushindi kwenye mchezo huo baada ya Amissi Tambwe kukosa mkwaju wa penalti dakika ya 29 iliyotokana na Heritier Makambo kuangushwa.

Tambwe alipiga mpira nje licha ya kumchambua vizuri mlinda mlango wa Ndanda, Said Mohammed ‘Nduda’. Licha ya kuambulia sare hiyo, lakini Yanga inaendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo ikijikusanyia alama 68 baada ya kucheza mechi 29.

Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 57 kutokana na kucheza mechi 22. Azam ni ya tatu ikijikusanyia alama 62 katika michezo 29.

Kwa sasa tofauti ya pointi kati ya Yanga na Simba ni alama 11, na endapo Simba itashinda mechi saba zijazo ili iwe sawa kimichezo na Yanga, itafikisha alama 78 ambazo ni kumi zaidi ya Yanga na kukaa kileleni jambo ambalo litakuwa njia nyeupe kwao kutetea ubingwa wao wa ligi hiyo.

Katika mchezo huo wa jana, kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa na mashambulizi ya kupokezana, lakini Ndanda ndiyo iliyomaliza kipindi hicho ikiwa mbele kwa bao 1-0. Kipindi cha pili Yanga ilikitawala muda mwingi na kuwafanya kusawazisha bao hilo ambapo Deus Kaseke ndiye aliyeleta uhai kwenye kikosi hicho akitokea benchi kuchukua nafasi ya Tambwe.

Hii ni mechi ya tano kwa Yanga kutoka sare msimu huu, imeshinda 21 na kupoteza tatu, imebakiwa na mechi tisa kukamilisha msimu huu ambao kila timu itacheza mechi 38. Simba imebakiwa na mechi 16 baada ya kucheza 22 na kushinda 18, sare tatu na imepoteza moja.

Kwa hivi sasa kama kila timu itashinda mechi zake zilizobaki, Yanga itamaliza msimu na alama 95 na Simba itafikisha 105. Baada ya mchezo wa jana, Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alilalamikia maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo na kudai kuwa yalichangia timu yake kutoshinda.

Kauli kama yake pia ilitolewa na Kocha wa Ndanda FC, Khalid Adams ambaye alisema huwa siyo kawaida yake kulalamikia waamuzi lakini kwa jana siyo kwamba walikuwa wakiipendelea timu moja bali aliona wameushindwa mchezo na walifanya maamuzi kadhaa tata ambayo yalichangia matokeo ya sare.

1 COMMENTS:

  1. Katika viporo vilivobakia na Yanga ishinde michezo yote iliyobakia na Simba ifungwe michezo mitatu bado bingwa atakuwa mnyama

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic