OFISA MTENDAJI MKUU WA BODI YA LIGI, BONIFACE WAMBURA |
NA SALEH ALLY
WIKI hii imeisha, gumzo badala ya kuwa ubingwa wa Simba, mambo yaligeuka na kuwa nani aliyeteremka.
Suala la timu iliyoteremka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza, limekuwa juu zaidi ya chochote.
Si kwamba aliyekuwa akiteremka ilikuwa kazi kubwa kumjua badala yake kutokuwa makini kwa wataalamu wa takwimu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ndio kumefanya mambo yaende hovyo kabisa.
Walishindwa kung’amua kati ya Kagera Sugar na Stand United ni timu ipi ilikuwa imeteremka daraja baada ya mechi ya mwisho ya 38.
Wao wakatangaza aliyeteremka daraja ni Kagera Sugar, lakini uhalisia alikuwa ni Stand United. Baada ya hapo kukazuka mjadala mkubwa sana kuhusiana na timu ipi hasa imeteremka.
Mimi niliporejea ofisini, niligundua pia kuna mkanganyiko huo. Kitengo cha takwimu cha Gazeti la Championi kilionyesha aliyeteremka ni Stand United. Lakini Bodi ya Ligi walionyesha ni Kagera Sugar. Nikawashauri wahusika kuhakiki upya matokeo ya timu zote ambayo yanahifadhiwa kwenye kumbukumbu zao.
Baada ya kazi ya saa takribani moja na ushee, wakagundua walikuwa sawa na kuendelea kusisitiza Stand United ndio walikuwa wameteremka daraja. Baada ya hapo ikawa kazi kuwatafuta watu wa Bodi ya Ligi kama walikuwa na kitu kingine. Haikuwa kazi nyepesi kuwapata hadi kesho yake walipoomba radhi kwa wadau kwa madai walikuwa wameghafilika na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura akaahidi kuchukua hatua kwa wahusika ambao alisema hii ni safari ya pili.
Kiasi kikubwa inasikitisha sana lakini ni funzo kubwa kama kuna tatizo ndani ya kitengo cha TPLB kinachohusika na takwimu. Mara nyingi sana imekuwa si kazi nyepesi kwao kutoa ushirikiano unapotaka takwimu.
Hili ni jambo linalokatisha tamaa na lionaonyesha kiasi gani wahusika “hawajatulia” na wao wanaona mambo ni ya kawaida tu kama vile hawana sababu ya kuwa na hofu ya kuharibu, jambo ambalo si sahihi hata kidogo. Lazima wawe makini, lazima wafanye kilicho sahihi kwa kuwa wanapozembea wanafanya mambo yanayoondoa imani ya TPLB au timu zinatazojenga hisia ya kuonewa.
Kukosea ni ubinadamu lakini si katika makosa makubwa kama hilo la kuiteremsha timu. Kama wananchi wasingehoji, ingekuwa dhuluma kubwa ya kupita kiasi.
Wambura lazima awe makini na watakaoadhibiwa, basi ni lazima taarifa ziwafikie wadau kwamba hatua gani zimechukuliwa ili kuonyesha kweli kama viongozi wa juu wamepania hasa kukomesha suala la aina hiyo ambayo linatokea sasa kwa mara ya pili.
Haiwezi kuwa kimyakimya kwa kuwa suala hili ni la jamii, waliokosewa ni wadau, hivyo lazima wajue hatua zilizochukuliwa ni zipi kuona kama kweli kuna umakini unatengenezwa baada ya kutokuwepo kwa mara ya pili.
Kuishusha timu daraja wakati bado haijateremka ni kashfa na ingekuwa katika nchi zilizopiga hatua kimpira, Wambura angeweza kuwajibika kutokana na uzembe wa watu wake. Sasa hapa nyumbani, inaweza kuwa tofauti lakini yeye sasa anapaswa kuonyesha hataki mchezo na suala hilo.
Kingine ambacho TPLB wanaweza kujifunza ni suala la kuachia kazi hiyo ikafanywa na kampuni nje ya bodi. Kuwaachia ambao ni wataalamu hasa badala ya wao bodi kufanya.
Hata Ligi Kuu England, wanaofanya si shirikisho wala bodi badala yake ni kampuni maalum yenye wataalamu wa kazi hiyo ndio maana kila kitu kinakuwa na uhakika na mambo yanakwenda sahihi tofauti na tunavyoona hapa nyumbani.
Kupata data za Ligi Kuu Bara tu imekuwa tatizo wakati wao TPLB walipaswa kuwa kama nyenzo muhimu ya jambo hilo na hasa katika uhakiki. Huu ni wakati wa mapinduzi na wanapaswa kubadilika ili mambo yaende sahihi la sivyo walio juu nao watapaswa kuwajibika ili mambo yaende sahihi.
Kweli kabisa kwa sababu kosa lililofanywa na TFF ni la kitakwimu kwa hiyo kunahaja ya wahusika kushughulikiwa ili iwe fundisho kwa wengine.
ReplyDeleteKweli kabisa kwa sababu kosa lililofanywa na TFF ni la kitakwimu kwa hiyo kunahaja ya wahusika kushughulikiwa ili iwe fundisho kwa wengine.
ReplyDelete