May 11, 2019

UTEKELEZAJI wa kile ambacho mlikuwa mnakiimba wakati wa kampeni kwa sasa ndio jambo la msingi ambalo mnapaswa mlipe kipaumbele kuliko kingine viongozi wapya wa Yanga.

Kwa kumchangua Mwenyekiti mpya Msindo Msolla ni jambo jema kwa kuwa huyu ni mtu wa mpira na amewalea watu wengi ambao ni wachezaji wazuri kwenye timu ya Taifa.

Fredy Mkwalebela ambaye ni Makamu huyu ni kiongozi mwenye uzoefu kwenye masuala ya mpira hivyo nina amini ni watu sahihi wanaojua mpira.

Pamoja na wajumbe wote ambao wamechaguliwa napenda kuwapa pongezi wote na kuwapongeza wanachama wa Yanga kwa hatua ambayo wamefikia.

Ukurasa mpya unapofunguliwa mambo mapya mengi yanatarajiwa kutokea basi na iwe hivyo kama ambavyo mliahidi kwa wanachama wenu muda ule wa nichagueni mimi nitafanya hiki na kile.

Kwa mlioshindwa kupenya bado muda upo siku zinakwenda kasi sana kesho itafika na muda wako ukifika kila kitu kitakuwa sawa endeleeni kushirikiana na wengine.

Yale makundi ambayo yalikuwepo awali ni muda wa kuyavunja na kuanza maisha upya kuijenga Yanga mpya yenye mafanikio hapo baadaye.

Viongozi ambao mmeshinda ni wakati wenu wa kushirikiana na viongozi ambao wameshindwa, kama mgombea anafaa kuwa pamoja nanyi haina haja ya kumtenga mpeni nafasi.

Hii itasidia kuijenga Yanga mpya na yenye nguvu kwa kila mwanachama na kila mmoja ambaye amefanya uchaguzi kwa kuwa tumeona haki imetendeka na kila mmoja anafurahi kuwa ndani ya Yanga.

Tukiachana na uchaguzi wa Yanga ngoja kidogo leo nigusie mwenendo wetu wa Ligi Kuu Bara kwa sasa ambayo imeanza kuyumba hasa kwenye usimamiaji.

Hakuna timu iliyo salama hasa kwenye upande wa kushuka daraja ingawa timu mbili tayari zimeshapenya kupanda ligi kuu bara hizo nazipa hongera.

Namungo ya Lindi pamoja na Polisi Tanzania ya Kilimanjaro karibuni huku kwenye ligi ya moto ambayo maajabu yake kuna timu bado zinamalizia viporo na nyingine bado zinahaha kupata nauli.

Siwatishi ila nawapa mwanga kidogo mjue mlipo hapa kuna nini na mambo gani ambayo yanaendelea heri yenu mlikuwa mnatambua mkishinda mtapanda daraja huku mpaka sasa mshindi hajua anashindania nini.

Yote kwa yote ligi bado ina mengi ambayo yanatokea hasa kwa muda huu ambao timu nyingi zimekalia kuti kavu kutokana na matokeo ambayo watayapata.

Ni ajabu ila ndivyo ilivyo, nashangaa kuona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inazitazama kwa ukaribu mechi za Simba na Yanga na kutoa maamuzi kwa haraka kama ilivyokuwa kwa waamuzi wa KMC na Simba.

Ila kwa timu nyingine wamekuwa wazito kutoa maamuzi hii sio sawa, mfano mchezo wa hivi karibuni kati ya Mtibwa Sugar na Singida United, tumeona kocha analalamika juu ya mamuzi ya waamuzi.

Mpaka sasa imekuwa kimya hali ni mbaya sana na inaumiza ukizingatia kwa sasa ni mwendo wa kampeni kwa kila timu inayocheza nyumbani, hatari kubwa inakuja.

Timu nyingi kwa sasa zimebakiwa na michezo minne na nyingine mitano ambayo kila timu inacheza kama fainali hivyo kupata matokeo kwenye mechi zote kwa timu hizi za juu ni lazima zijipange kwa sasa.

Kumekuwa na kampeni ambayo inaendeshwa kwenye kila mkoa ambapo timu zinakwenda kucheza na zile ambazo zipo nafasi ya chini yaani kivyovyote lazima mgeni unyooshwe.

Kama mwendo utakuwa huu hapa tunacheza mchezo ambao sio sawa kwa afya ya soka letu unahitajika umakini mkubwa na nidhamu ya hali ya juu.

TFF hapa mechi za lala salama kuna muvi ndefu sana inachezwa hapa kama mtabaki kimya bila kuchunguza zitashuka daraja timu ambazo zina uwezo zitaachwa zile zenye mipango ya kampeni ya kubaki.

Hali yetu ya soka sasa imekuwa mbaya na inatia huzuni wakati huu wa lala salama, ninaamini waamuzi wakifuata sheria 17 za mpira na kanuni zikafuatwa tutapata bingwa wa haki.

Kama waamuzi wataendelea kutupiwa lawama hii ni hatari kwa soka letu na kwa bingwa ambaye atapatikana kila mmoja ajitathimini namna anavyotimiza majukumu yake hatua zinapaswa zichukuliwe.

Muda huu kila timu ijipange kupata matokeo chanya kwa njia halali na sio kuungaunga, kama ipo timu itakayoshuka basi ishuke kihalali na kama ipo timu itakayobaki ligi kuu ibaki kihalali.

Lala salama siku zote huwa haiachi timu salama kwa kuwa kila mmoja anapambana na hali yake, TFF umakini na kufuatilia kila mechi za mwisho ni jambo la msingi.

Ninaamani kila kitu kinawezekana endapo kila mmoja atajipanga na kutenda haki, kupitia kanuni zilizowekwa na kupitia sheria basi bingwa atapatikana kwa haki.

Kama bingwa atapatikana kwa njia ya kubebwa hataweza kuibeba nchi kimataifa kwa kuwa anakwenda kukutana na watu wengine ambao hawajui namna alivyoshinda.

Cha msingi kila timu ijiandae vema kupata matokeo chanya kuelekea kwenye ushindani wa kimataifa ambao tunautarajia nina amini hilo litatufanya tuwe salama, TFF toeni maamuzi hapa hali sio shwari kwa sasa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic