May 23, 2019


KOCHA wa Lipuli, Seleman Matola amesema kuwa kwa sasa kikosi chake kinapata taabu kubwa kutokana na ratiba kubana huku mamlaka zikiacha suala liendelee hilo bila kuchukua hatua.

Matola jana alikubali sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Ndanda kisha leo anaanza safari kurejea Iringa kabla ya jumapili kuanza safari kuifuata Mbeya ambapo anamchezo na Tanzania Prisons Jumanne pia ana mchezo Alhamisi wa fainali ya FA dhidi ya Azam FC, Lindi.

Akizungumza na Saleh Jembe, Matola amesema wachezaji wake wanapitia kipindi kigumu kutokana na ratiba kutokuwa rafiki kwani hawapati muda wa kujiaanda kwa kila mchezo badala yake wanaishia barabarani.

"Kikosi changu hakina ratiba nzuri kwani maandalizi yetu yote yanaishia kwenye safari, hivyo wachezaji wanaingia uwanjani wakiwa wamechoka hali inayofanya wacheze chini ya kiwango.

"TFF nimewaandikia barua ili wabadili ratiba kwani ratiba inaonyesha ninacheza tena fainali Juni mosi jambo ambalo ni hatari kwa afya ya wachezaji wangu ukizingatia kwa sasa ligi inakamilika jumanne sioni haja ya kuendelea kubanwa tena," amesema Matola.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura amesema ratiba ilitolewa muda mrefu hivyo ni maandalizi kwa timu husika yanapaswa yazingatiwe.

"Mwezi huu una siku 31 hivyo kama atamaliza mchezo wake Mei 28 bado ana muda wa kujipanga na kupumzika kwa ajili ya mchezo wake wa Juni Mosi hivyo suala la kubadili ratiba hilo halipo," amesema.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic