NI HUZUNI, FAMILIA YAMLILIA MWANAFUNZI MTANZANIA ALIYEFARIKI MAREKANI
“TUMEPOKEA taarifa hizi kwa masikitiko makubwa. Alipenda sana masuala ya utabibu, na alienda Marekani kupata mafunzo na kutekeleza ndoto zake,” imeeleza familia ya kijana Allen Buberwa, ambaye amefariki nchini Marekani mwanzoni mwa wiki.
Buberwa, 22, ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa unesi katika Chuo cha North Arkansas College alifikwa na umauti baada ya kuteleza na kutumbukia kwenye mto Buffalo. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 12 jioni jimboni Arkansas, Marekani.
Taarifa rasmi zinaeleza kuwa, Buberwa na rafiki zake watatu walienda mtoni huku wawili kati yao wakiingia majini na kuogelea. Buberwa pamoja na kijana mwengine walisalia ukingoni mwa mto.
Ghafla Buberwa aliteleza na kutumbukia mtoni na kushindwa kujinasua, kijana mwenzie aliyekuwa naye pia alijirusha ili amuokoe lakini pia akanasa. Rafiki zao wawili waliotangulia mtoni walijitahidi kuwaokoa lakini Buberwa alisalia chini ya maji.
Vikosi vya uokozi viliupata mwili wake majira ya saa tano usiku wa siku hiyo hiyo ya tukio.
“Kwa ujumla tumeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa sana, na tumeumia sana juu ya Allen,” mjomba wa marehemu na msemaji wa familia, Bw. Philbert Simon, ameiambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) na kuongeza: “Baba (wa Allen) yupo kwenye hali mbaya, anaumia sana, ndiyo kijana wake mkubwa… anaumia sana juu ya kijana wake.”
Bw. Simon anasema Buberwa alipata chuo Marekani baada ya kufanya jitihada binafsi mtandaoni akishirikiana na wazazi wake.
Kwa sasa mwili wa marehemu upo kwenye jumba la kuhifadhia maiti la Coffman Funeral Home of Harrison of Harrison and Jasper, na kwa mijbu wa Simon, wanarajia mwili huo kuwasili Tanzania kati ya Jumatano au Alhamisi wiki ijayo na mazishi yanarajiwa kuwa siku moja baada ya kufika.
Gharama za kuhifadhi na kusafirisha mwili huo mpaka Tanzania zinakadiriwa kufikia dola 14,000.
“Jitihada za kuurejesha nyumbani mwili wa kijana wetu zinaendelea nchini Marekani. Kuna Watanzania wanaoishi kule wanafuatilia suala hili, wanafunzi wenzake pia wanachangishana lakini bado tunahitaji mchango wa kila mtu kutoka kila upande ili kufanikisha kumleta mpendwa wetu,” alisema Simon.
0 COMMENTS:
Post a Comment