TUMEONA timu mbili kubwa hapa bongo ambazo ni Simba na Yanga, zimejitoa mashindano ya Kagame Cup ambayo mtetezi wake ni Azam FC.
Hapa kuna kitu cha msingi cha kujifunza kwa kamati ya mashindano ambayo ipo chini ya katibu Musonye kujitathimini na kuangalia wapi anapokosea hasa kwa upande wa maandalizi.
Muda wa kujibizana kwa sasa sio wakati sahihi ni lazima kamati ikubali kwamba mashindano yamepoteza ule mvuto wa awali kama mashindano yalivyoanza.
Hivyo kuna umuhimu wa kufanya maboresho kwa namna ya kuzichagua timu pamoja na kuongeza zawadi kwa washindi kwani kwa sasa mambo yamebadilika.
Muda mzuri wa kukaa chini na kujiuliza wapi kamati inakwama na kwa nini michuano kila iitwapo leo thamani yake inashuka.
Nina imani maboresho yakifanyika itakuwa ni rahisi kupata timu nyingine nyingi zaidi ambazo zitashiriki michuano hii mikubwa.
Kwa kufanya hivyo mvuto utarejea na heshima itarudi kama ilivyokuwa zamani kila mmoja atafurahi kushiriki michuano hii mikubwa.
Turejee kwenye timu yetu ya Taifa ya Tanzania ambayo inashiriki michuano ya Afcon baada ya kupita miaka 39.
Kupata nafasi ndani ya timu ya Taifa ni jambo kubwa kuliko vile ambavyo wanafikiria hivyo masuala ya uwezo ni matokeo tu hapo baadaye kuitwa ni jambo la kwanza.
Kuna mambo mengine mashabiki tuyaache tuiunge mkono timu yetu ya Taifa ifanye vizuri kwenye michuano hii mikubwa wakati ukifika yatazungumzwa kwa uzuri.
Tukija kwa upande wa kambi ya timu ya Taifa ni muda mwafaka wa kutazama namna ya kuweza kujiaanda kufanya maajabu hasa kwenye michezo ya michuano ya Afcon ambayo tunashiriki.
Wachezaji wote mnapaswa muwe na jicho la kipekee hasa mliopata nafasi kushiriki michuano hii wakati huu watanzania hawatakubali kulia tena.
Muda wa kuwatoa kimasomaso mashabiki ni sasa na kinachotakiwa ni kufanya vizuri kwenye michezo yenu yote mtakayocheza.
Hakuna haja ya kuhofia majina ama aina ya wachezaji ambao mnakutana nao wote asili yao ni moja na uwanja ni mmoja tu matokeo ni muhimu.
Pia suala la kujua kwamba mpo kwenye soko la dunia litapanua wigo mpana kwenu na kuwapa fursa ya kutengeneza fedha na soko la kutafutwa na timu nyingine.
Ipo hivi kama bado hamjajua ni kwamba wengi kwa sasa ambao ni mawakala wanatizama kwa ukaribu michuano ya Afcon kama sehemu yao ya kazi.
Hivyo kama wachezaji mtagundua hilo nina amini mtapata mlango wa kutokea kwa ajili ya kutengeneza maisha yenu nje ya bongo.
Hata kwa wale ambao wanatimu nje bado mawakala lazima watajua namna ya kuwapa nafasi nje ya hapo mlipo tena kwa ofa kubwa.
Hizi ofa haziji kimchezomchezo tu ni lazima timu ipambane na wachezaji wajitoe kwa hali na mali kwani juhudi bila maarifa huwa ni bure.
Endapo mtatambua kwamba ninyi mnathamani kubwa hapo mlipo ni lazima mpambane kweli kujiweka sokoni na kuongeza gharama zenu za kuuzwa.
Nina imani wale watakaofanya vizuri watafungua milango ya mafaniko na wale watakaozembea itakuwa ni hasara kwao na Taifa kiujumla.
Tumeona kwa sasa timu ina muunganiko wa wachezaji wengi wanaocheza nje ya bongo haya ndiyo mafaniko ambayo tunayafikiria.
Kila siku mchezaji unapaswa ujue kwamba hapo ulipo sio sehemu yako pambana ili uliokoe Taifa na kwa faida yako binafsi.
Kwa mashabiki mnapaswa msijigawe ninyi timu yenu ni moja Tanzania na wachezaji wote walioitwa kwenye kikosi ni watanzania asili yao ni moja tusiwabague.
Mwalimu tumwache afanye kazi yake kwa umakini kwani waliompa timu wanamwamini ndio mana yupo hapo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni muda wa kuwaandalia wachezaji mazingira mazuri ili wakipata nafasi kucheza nje ya nchi iwe rahisi kwao kupenya.
Imani yetu na dua zetu kwa timu ya Taifa kuleta ushindani utakaosaida kupeperusha Bendera ya Taifa kwa wakati na kwa muda sahihi bila kuacha maumivu.
0 COMMENTS:
Post a Comment