July 4, 2019




NGOMA imekuwa nzito kwetu kuchezeka kwenye michuano ya Afcon ambayo kufuzu kwetu ilikuwa ni kwa mahesabu makali na tukafanikiwa kushinda mbele ya jirani zetu Uganda kwa ushindi mnono wa mabao 3-0.

Kazi ilikuwa ni ngumu kwa wachezaji ambao walipambana kwa hali na mali kutafuta matokeo uwanjani ila ilikuwa ngumu kutokana na mfumo ambao tumekuwa nao muda mrefu.

Imekuwa jadi yetu kuwa waongeaji wazuri mdomoni kuliko kuweka mambo tunayoyaongea kwenye vitendo jambo ambalo limekuwa likituangusha wakati mwingi kwenye michuano mingi.

Kwa hapa tulipofikia ni wakati muafaka sasa wa viongozi wa mpira kuketi chini na kutazama wapi ambapo tulishindwa kutendea haki yale maneno ambayo tuliyazungumza na kuishia kuwa wasindikizaji kwenye michuano mikubwa.

Ukweli usiopingika ni kwamba hatukujiandaa kushinda tulijiandaa kusindikiza na ndio maana hata maandalizi yetu yalikuwa ni ya kusuasua kama hakuna kitu ambacho kinakwenda kutokea.

Yote kwa yote, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa liangalie michuano hii kwa jicho la kipekee na sio kuishia kushiriki kisha mipango ikazikwa moja kwa moja itatugharimu zaidi.

Tutazame wenzetu ambao wanafanya vizuri wao wanafanya nini nasi tunafanya nini hasa kwa kuanzia kwenye ligi ya ndani pamoja na maandalizi ya mwisho.

Kidogo tuwazungumzie majirani zetu Kenya namna walivyotupa adabu wao walifanya nini tukianza kwenye hamasa nini kilitokea kwao kabla ya mchezo.

Ukiangalia kwa ukaribu utagundua kwamba wao waliwaita watu maalumu ambao wana uwezo kwenye soka na wanalitambua soka la Afrika pamoja na mbinu za kushinda michuano ya Afcon.

Hawa ndio waliotumika kuwapa sumu ya ushindi wachezaji wao wa Kenya mwisho wa siku wakatumaliza ilihali tulianza kuwadhibiti kipindi cha kwanza.

Tukigeuka kwenye kambi ya timu yetu ya Taifa ya Tanzania hapo ndipo utaona utofauti mkubwa wa maandalizi, watu waliokuwa wakipewa nafasi walikuwa ni wanasiasa.

Kuna yule mmoja alikuwa ni mchekeshaji, hata namna ya kupanga kikosi haelewi anapoongea na waandishi anakazana kusema katikati na nyuma wamepoteana hapa ndipo tulipoanza kufeli.

TFF inapaswa ichague watu makini ambao wanaweza kutoa morali ya kweli na mchezaji akapata uchungu kwa namna ambavyo ataelezwa tofauti na kupeleka orodha ya wanasiasa ambao wao wapo kwa maslahi yao binafsi.

Mpira sio siasa ni sayansi ambayo inajengwa na kukuzwa na wale ambao wanaitambua vema sasa kama watu wapo kwenye kamati ya hamasa basi wapewe nafasi zao kisha wanaoongea na wachezaji nao wapewe nafasi zao.

Wakati mwingine itakuwa vema kama TFF itaandaa watu maalumu ambao watakuwa karibu na timu kutoa hamasa na kuwapa wachezaji sumu za kuwaangamiza wachezaji wao zile za kisayansi ambazo zinafanya kazi uwanjani.

Wanasiasa ni watu wazuri majukwaani ukiwapeleka uwanjani wanajaza porojo kibao na ahadi ambazo wakati mwingine huwa ngumu kutimilika hasa uwanjani ni muda wa kubadilika.

Uwekezaji uwe wa kweli kwa kuanza na ngazi za chini ambako wachezaji wanatengenezwa hivyo ni muda mzuri kuwa na vituo vingi vya wachezaji chipukizi na vijana wenye uwezo.

Ligi ya vijana ipewe kipaumbele na itazamwe kwa jicho la karibu isiwe tia maji tia maji maumivu tutayatengeneza sisi wenyewe tunapaswa tupige hatua moja kwenda mbele na sio kuanza kurejea nyuma.

Hakuna ambaye atakuja kuboresha mpira wetu kama sisi wenyewe tutaamua kupeleka mambo ndivyo sivyo maumivu yanarejea kwetu wenyewe.

Afcon ituondolee lile gundu la kutoshiriki kwa miaka 39 sasa iwe ni mwendelezo muda wote kwa kuwa tayari tumeonja utamu wa michuano hii mikubwa.

Ramani yetu ya soka sasa inaanza kufunguka na kwa wachezaji wenye kujielewa wanatambua thamani ya kushiriki michuano hii mikubwa.

Kila mmoja na awe balozi mzuri kwa ajili ya kujenga timu bora msimu ujao ambayo itasaidia kukuza soka letu kwa kututoa hapa tulipo.

1 COMMENTS:

  1. Timu ya Taifa inatolewa AFCON....Turudi sasa kwenye "vumbi letu na usajili wa magazeti na mihemko ya ushabiki wa timu za Kariakoo zinazodumaza soka letu"

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic