MWA MWA MWAIKIMBA... |
Baada ya mshambuliaji wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba, kuiongoza timu
hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting, juzi Alhamisi,
uongozi wa Azam umefunguka kuwa Mwaikimba ana thamani kubwa zaidi ya
mshambuliaji wa Yanga, Mganda, Emmanuel Okwi.
Mwaikimba aliiongoza Azam kupata ushindi huo na kuukaribia ubingwa wa
Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, amesema kuwa, Okwi
ni mchezaji mzuri lakini thamani yake katika soka la Tanzania ipo chini
ukilinganisha na Mwaikimba.
“Hao wachezaji wengine wanaotamba hapa nchini ni wachache sana ambao
wanaweza kupambana katika viwanja vya mikoani, kwani wao ni hodari kwa viwanja
vizuri kama ule wa Taifa na Chamazi ambavyo sehemu yake ya kuchezea ni nzuri.
“Lakini kwa Mwaikimba ni tofauti, yeye anafanya vizuri katika viwanja
vya mikoani ambavyo sehemu yake ya kuchezea ni mbaya, hata hivyo baada ya
kuligundua hilo ndiyo maana Mwaikimba tukaamua kuwa yeye atakuwa akicheza
mikoani na Dar es Salaam watacheza wengine.
“Kutokana na hali hiyo, Mwaikimba kwetu sisi ana thamani kubwa zaidi
ya wachezaji hao wanaotajwa kuwa na thamani kubwa hapa nchini akiwemo Okwi na
wengine wengi,” alisema Nassor.
Wakati huohuo, Mwaikimba
amesema kuwa ana imani timu yake itashinda mechi dhidi ya Mbeya City
inayotarajiwa kupigwa kesho kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
“Kufika hapa tulipo tulijipanga vizuri, nina imani hata mechi ya Mbeya
City tutashinda,” alisema Mwaikimba.
0 COMMENTS:
Post a Comment