WIKI iliyopita tuliishia wakati Madee yupo kwenye tamasha lake jijini Dodoma na kwa bahati mbaya anakutana na tukio la kupopolewa mawe na chupa za mkojo jukwaani. Je, ungependa kujua ilivyoendelea?
SONGA NAYO…
“BAADA ya kurushiwa mawe na kuvunjwavunjwa vioo kibao vya pale ukumbini huku mimi nikitafuta mlango wa kutokea, ghafla DJ wangu naye akapigwa jiwe akaamua kutoka nduki kusikojulikana na kuniacha mwenyewe nikihangaika kutazama wapi mahali salama ambapo ningeweza kuingia na kutuliza nafsi yangu ili nisidhurike.
“Wakati naendelea kuangaza huku na kule vurugu zikizidi kushamiri ukumbini pale, nilisikia mtu akiniambia, ingia huku, kugeuka kumbe nyuma ya steji nilikuwa nimesahau kabisa kama kulikuwa na chumba cha wasanii ambacho hutumika kupumzika kabla ya kuanza shoo, basi baada ya kukiona nilitoka nduki na
kuzama ndani ya chumba hicho na kujifungia.
Wakati nipo nimejifungia chumbani mle ndipo baadhi ya watu wakawapigia simu polisi waliokuja kunichukua huku ukumbi ukiwa umezizima kwa fujo na kunipeleka moja kwa moja katika gari lao kama wanaelekea kituoni ikiwa ni moja ya mbinu ya kuwazuga watu wasijue nilipoelekea, kisha wakanipeleka katika “lodge” niliyokuwa nimefikia na kunitaka kesho yake asubuhi niamke mapema kabla watu hawajaamka na niondoke Dodoma ili wasinifanyizie kitu mbaya.
“Basi kweli ilipofika kama saa 11 alfajiri hivi nilinyanyuka zangu nikiwa na Tale ambaye tulikuwa wote ukumbini na kwenda stendi kisha tukapanda gari bila hata ya kukata tiketi kwanza, maana nakumbuka tiketi hatukuwa tumekata, hivyo tukalazimika kulipa tukiwa ndani ya gari japo wasiwasi ulikuwa mkubwa sana kwetu kutokana na kuwa na hofu ya kukutana na wengine kwenye basi.
“Nashukuru sana safari yetu tulianza salama kwani hadi tunafika hakukuwa na mtu yeyote wa fujo aliyekuwemo ndani ya gari hilo, hivyo baada ya kufika Dar es Salaam nakumbuka nilifika tu tukaanza maandalizi ya shoo ya Tigo ambao kipindi hicho ndiyo walikuwa wanaanzaanza kufanya shoo za promosheni yao, lakini kabla sijaendelea kukueleza hilo nakumbuka mchana ule baada ya kufika kuna mtu alinipigia akinichimba mkwara wa nguvu akiniambia niachane na ngoma hiyo.
“Ila hali Hiyo haikuishia hapo tu baadaye tena nikapokea simu nyingine jamaa akiniambia wewe ndiyo nini sasa unaimbaimba wimbo wa ajabuajabu kama huo tena unaitukana Hip hop, lakini wakati huo Bonge tayari alikuwa ameshaniambia kama kuna mtu atakupigia simu ya kukutishia niambie mimi yuko wapi tumfuate, sasa Bonge akawa amenipa ujasiri hivyo nikamuuliza niambie upo wapi nikufuate.
“Jamaa akaniambia njoo nipo zangu hapa Bamaga karibu na kwa P-Funk, lakini tulipoanza kwenda tukawa tunamsikia anaelekeza kama yupo karibu kabisa na pale Bamaga zilipokuwa ofisi zenu za Global Publishers kabla hamjahama pale, basi wakati tunaendelea kwenda mara akapiga tena simu akiniambia acha ujinga wewe Chid Benz hapa!
Nikamwambia dah! Chid vipi, akanicheka akaniambia duuh mwanangu kweli umekaza, ulitaka kuja kweli kunidunda hata huogopi basi mimi baada ya kuniambia vile safari ya kumfuata ikaishia pale nikaendelea na mishemishe nyingine.
“Basi matukio ya kutishiwa yalizidi lakini mimi sikuyajali tena, zaidi wakaanza mtindo wa kila msanii wa Hip Hop akitoa wimbo lazima kuwe na vesi ya kuniponda juu ya wimbo huo ikiwa kama njia ya kunikomoa lakini mimi hali hiyo ilinijenga sana kiasi kwamba nikawa siogopi tena kuifanyia shoo nyimbo (wimbo) hiyo.
“Nakumbuka tu siku moja katika orodha ya wasanii walioimba na kunitaja kwa kuniponda nilimpigia Fid Q kumuuliza maana kuna wimbo wake aliachia na ndani yake kuna vesi aliimba akisema kuwa “Kuna wasanii wengine hawapendi Hip Hop kama Madee wa Tip Top, basi mimi kwa kuwa wimbo ule niliupenda ilibidi nimpigie simu na kumuuliza vipi bro kwenye mstari huo ulikuwa unamaanisha nini labda?
“Basi bila kinyongo yeye akanielewesha kuwa imebainika kuwa Hip Hop inanilipa mimi tu lakini kuna wasanii wengine wengi hawaipendi na haiwalipi kama wewe na ndiyo maana ukaamua kusema hadharani kupitia wimbo wako huo wa Hip Hop Haiuzi, basi aliponielewesha mimi nikacheka nikapata jibu lake tu na wimbo huo nikawa naupenda sana hivyo wengine wakawa wanaimbaimba tu mimi siwajali.
“Baada ya hapo sasa ndiyo kesho yake tukaenda zetu Arusha kwenye shoo hiyo ya Tigo na nakumbuka shoo yenyewe ilifanyikia nje ya Ukumbi wa Triple A pale, nikiwa zangu nimekaa na Bonge na wasanii wengine wa Tip Top akiwemo Tunda, Z-Anto na watu wa TMK ambapo alikuwepo Chege, Temba na wengine wengi wengi.
“Mara akatokea mtoto mmoja hadi kwenye dirisha la gari yetu akamfuata Tunda Man akamwambia bro bwana mimi narap bwana, Tunda bila kumpa nafasi ya kumsikia akaanza kumtimua akimwambia hebu tutokee hapa bwana unatuzingua, nenda kwa rapa mwenzio kule Madee ukamwambie ishu hizo, kweli kijana akaja upande wangu akaniambia bro mimi naimba bwana huku akionekana kwa pembeni ana wafuasi kibao yaani.”
0 COMMENTS:
Post a Comment