July 9, 2019


Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, hali ya mambo ilivyo hivi sasa huko mitaani baada ya timu za Simba na Yanga kuwa mbioni kuhitimisha usajili wake.

Hata hivyo, hivi sasa habari mpya ni kwamba kutokana na usajili ambao tayari timu hizo zimeufanya, kila shabiki wa timu hiyo akili yake inafikiria siku ambayo timu hizo zitakutana uwanjani mambo yatakuwaje. Timu hizo kila moja inaonekana kufanya usajili wa nguvu ambao mpaka sasa umepokelewa vizuri na mashabiki wa timu hizo.

Hata hivyo, kazi iliyobaki sasa ni kwa makocha wa timu hizo kuhakikisha wanapata vikosi vya kwanza vya nguvu ambavyo watakuwa wakivitumia katika michuamo ya Ligi Kuu Bara pamoja na ile ya kimataifa msimu ujao ambapo timu hizo kwa pamoja zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mpaka kufikia jana, Yanga ilikuwa tayari imeshatangaza kusajili wachezaji wapya 12 wakati Simba kwa upande wake yenyewe ikiwa imesajili wachezaji wapya tisa.

Wachezaji hao wa Yanga ni kipa Farouk Shikhalo (Kenya), Lamine Moro (Ghana), Juma Balinya (Uganda), Maybin Kalengo (Zambia), Mustapha Suleiman (Burundi), Issa Bigirimana ‘Walcott’ na Patrick ‘Papy’ Sibomana wote raia wa Rwanda.

Kwa wazawa ni Ally Ally ‘Mpemba’ kutoka KMC, Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli), Abdulaziz Makame (Mafunzo FC), Balama Mapinduzi (Alliance) na Muharami Issa Said (Malindi).

Wachezaji hao wataungana na nyota wa zamani wa timu hiyo ambao wao wameepukana na panga la kuachwa la kocha mkuu wa timu hiyo, Mkongomani Mwinyi Zahera kuhakikisha wanarejesha furaha ya mashabiki wao iliyopotea kwa muda mrefu.

Wachezaji hao ni kipa Radhani Kambwili, Juma  Abdul, Paul Godfrey ‘Boxer’, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Rafael Daud, Pappy Tshishimbi, Mrisho Ngassa, Juma Mahadhi, Feisal Salum ‘Fei Toto’ pamoja na Mohammed Issa Banka.

Kwa upande wa Simba wachezaji ambao mpaka sasa imewasajili ukiwaondoa wale wa zamani walioongezwa mikataba ni Francis Kahata (Kenya), Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Viera, Wilker Henrique da Silva (Brazil), Sharaf Eldin Shiboub (Sudan), Deo Kanda (DR Congo).

Wachezaji wa ndani ni Ibrahim Ajibu na Beno Kakolanya waliotokea Yanga pamoja na Kennedy Juma kutoka Singida United.

Wachezaji hao wataungana na nyota wa zamani wa timu hiyo kama vile John Bocco, Pascal Wawa, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Clatous Chama, Jonas Mkude, Rashid Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Dilunga, Said Ndemla na Mzamiru Yassin.

Kutokana na hali hiyo, mashabiki wa timu hizo mbili wana shauku kubwa ya kutaka kuziona timu hizo zikitifuana uwanjani ili kujua nani atakuwa mbabe wa mwenzake msimu ujao ukianza.

Kocha Zahera ameliambia Championi Jumatatu, kuwa usajili wake huo ameufanya kulingana na upungufu aliouona msimu uliopita, hivyo anaamini kabisa kila kitu kimeenda kama kilivyotakiwa, kwa hiyo Simba pamoja na timu nyingine zitakazokutana na kikosi chake zijipange vilivyo kukabiliana nacho.

“Kwa hiyo kazi kubwa ambayo nitakuwa nayo mimi ni kuhakikisha nawaunganisha vilivyo wachezaji hao ili waweze kuwa fiti na yeyote awe na uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza bila ya tatizo lolote,” alisema Zahera.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems alipotafutwa ili aweze kuzungumzia usajili huo lakini pia mipango yake ya jinsi gani atakiunganisha kikosi hicho baada ya kuwa na sura mpya, hakupatikana japokuwa huko nyuma aliwahi kusema atakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha mafanikio waliyopata msimu uliopita yanakuwa zaidi msimu ujao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic