TUMEONA Timu ya Taifa ya Tanzania imewatoa
kimasomaso mashabiki wake hasa kwa ushindi ambao wameupata kwenye michuano inayowahushisha
wachezaji wa ndani maarufu kama Chan mbele ya Kenya.
Stars
inahitaji pongezi licha ya kupata matokeo kwa njia ya penalti bado kwenye mchezo
kitu cha mwisho kinachoangaliwa ni matokeo kwani wachezaji walionyesha nia ya
dhati kupambana na kuamini lazima wapeperushe Bendera ya Taifa.
Timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20
‘Tanzanite’ nao wamepata fursa ya kutinga hatua ya fainali kwenye michuano
ya COSAFA inayoendelea nchini Afrika Kusini.
Kwa hatua
ambayo wameifikia nao wanapaswa pongezi kwani kazi kubwa ya kupata matokeo tena
ugenini inaleta picha mpya kwamba tayari imeanza kutambua thamani ya Bendera ya
Taifa.
Leo itacheza mchezo wake wa fainali dhidi ya Zambia hivyo wanapaswa wapambane kupata matokeo chanya.
Kabla
sijaendelea na maada yangu pia nitumie muda huu kuwapa pongezi Yanga na Simba
kwa kujitoa kwa ajili ya jamii, hakika mnastahili pongezi kwa matendo haya
mema.
Mwanzo huu
usiwe na mwisho bali uendelee kuishi kwa kila mmoja na uwe utamaduni wa kila
shabiki na mwanamichezo.
Kujitoa kuna
raha yake hasa unapowasiadia wengine ambao wapo kwenye uhitaji jambo jema
ambalo kwa hatua na ukubwa wa timu zetu zinajenga picha nzuri kwa mashabiki na
Taifa.
Pia kwa kupambana kwenye michuano ya kimataifa ambapo wote wamelazimisha sare walianza Simba kwa kulazimisha sare ya kutofungana huku Yanga nao wakilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Township Rollers uwanja wa Taifa.
Turudi kwenye maada sasa ya leo, kazi kubwa ni
kwa timu zetu za Taifa kuweka nguvu kwenye michezo yao ya mbele inayofuata.
Kwenye
ulimwengu wa michezo kila kitu ambacho wachezaji wataamua kukifanya kwa nia
moja siku zote hutimia na hata kuvunja rekodi ambazo awali zilikwekwa.
Kwa sasa
kazi ni moja tu kwa timu zetu kufanya vizuri hivyo hilo lipo mikononi mwa kila
mchezaji kuamua kutimiza nia ambayo wameiweka kwa dhati.
Kujiamini ni
jambo la msingi kwani kama mchezaji atakuwa na hofu inakuwa ngumu kwakwe
kufanya maamuzi sahihi yatakayoleta matokeo chanya kwenye mchezo ambao
anacheza.
Tatizo hili
likuwa linawakumbuka wachezaji wa Tanzanite ila mwisho wa siku lilipata dawa na
hatimaye timu ikapata matokeo chanya kwenye mechi zake mbili za awali ni kitu
kizuri na baadaye kutinga hatua ya fainali.
Kwa upande
wa Stars wao walikuwa wanakumbwa na tatizo la kushindwa kumalizia nafasi ambazo
wanazitengeneza ndani ya uwanja na bado limeendelea kuwatafuna.
Hilo
limekuwa wazi kwani hata ushindi ambao wameupata ni kwa njia ya mikwaju ya penalti hivyo bado benchi la ufundi lina kazi ya msingi kulimaliza hili tatizo.
Kuna umuhimu
wa wachezaji kujiamini na kumaliza mchezo mapema kabla ya kutegemea kupenya kwa
penalti ambazo wakati mwingine hazina mwenyewe kama ambavyo jirani zetu Kenya
imewatokea.
Kufuata
maelekezo ya mwalimu ni kitu cha msingi kwa wachezaji wote wakiwa uwanjani
kwani ule ndio mpango kazi wa kwanza ambao unatakiwa utekelezwe, kisha kama
mbinu itafeli ndipo akili ya ziada kwa wachezaji inapaswa itumike.
Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) linapaswa liwe na mikakati mipana kwa ajili ya
kuendeleza vipaji na kukuza soka letu hasa kwa wachezaji wa ndani pamoja na
wale wa nje.
Muda ambao
tupo kwa sasa ni muhimu kutengeneza wachezaji ambao kesho watakuwa na misingi
imara na watakuwa wamelelewa kwa muda mrefu kabla ya kuanza kuhangaika kutafuta
wachezaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment