August 26, 2019




Na Saleh Ally
MSIMU mmoja bila ya kuwa na wadhamini wakuu imeonekana kuwakwaza kwa kiasi kikubwa wachezaji, viongozi wa soka na mashabiki wao.

Lawama zimekuwa nyingi na karibu zote zilisukumwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huku Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wakisahaulika kuwa nao ndio wahusika wakuu.


Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Vodacom, iliamua kuachia ngazi kwa kile ambacho tulielezwa TFF, kuamua kuongeza timu kutoka 16 hadi 20 bila ya kuwa na mazungumzo sahihi.


TFF wakati wa Jamal Malinzi ilichukua hatua hiyo ingawa utekelezaji ukafanyika wakati tayari kuna uongozi mpya chini ya Wallace Karia.

Tulielezwa Vodacom hawakuwa wamejiandaa kwa timu 20, lakini kwa kuwa siasa za mpira zilikuwa zinalazimisha kuongezeka ili iwe msaada wakati wa uchaguzi, likafanyika hilo na wadhamini wakajitoa.


Msimu uliopita licha ya kuwa bora kwa maana ya ushindani huku timu moja ya Tanzania ambayo ni Simba ikifanya vema kabisa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufika hatua ya robo fainali, bado kulikuwa na vilio vingi.

Viongozi wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara wanajua machungu waliyoyapata kuhusiana na usafiri kutoka kituo kimoja kwenda kingine. Wanajua namna ambavyo walisumbuka na gharama ambazo wakati mwingi zilikuwa zikitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu Bara ambaye ni Vodacom.


Hadi leo hatujaona sherehe ya Simba kukabidhiwa zawadi, nani mchezaji bora au zawadi aliyopewa mfungaji bora. Hakika mambo yalikwenda “Kiswahili” tu hadi kiasi kikubwa imepoteza maana na thamani ya ligi hiyo.


Lazima tutakuwa tumejifunza na kuachana na zile tabia za kuwachukulia watu poa. Kwamba Vodacom walikuwa wanaonekana kama wapowapo tu na hata wakitaka waondoke. Walipoondoka, ukali wa maisha bila ya wao umeonekana.


Sasa hakuna sababu tena ya kutaka kurudia makosa yaleyale. Kwanza tuwe waungwana na kukubali kuwa Vodacom ni muhimu na ndio maana mlikuwa mnalialia kuhusiana na mambo kadhaa ambayo walikuwa wakiyafanyia kazi na yakaenda vizuri wakiwa wadhamini.


Sasa wamekubali kurejea, hili ni jambo jema sana. Hatujui kila kitu ndani ya mkataba wao na TFF na TPLB uko vipi, lakini tunajua kilichowarudisha wanataka kujitangaza.


Kama ni hivyo, basi muwe na heshima na mkataba huo na kufanya mambo kitaalamu, kwa kufuata weledi ili kuwashawishi Vodacom ambao wameingia mkataba wa miaka mitatu, wakimwaga Sh bilioni 3 kila mwaka, waone kuwa wanatakiwa kuongeza baada ya kumalizika kwa mkataba huu.


Lazima mjifunze, Vodacom hawatoi sadaka. Jifunzeni thamani ya fedha wanayotoa na mtambue kutokuwepo kwao, kunawaumiza wakati wao wanaweza wakawa hawaumii.


Tuachane na yale yasiyokuwa na sababu za msingi, mfano baadhi ya klabu kutaka kuanza kugomea. Nawashauri mfano Yanga waheshimu nembo za Vodacom, yale mambo kwenye jezi yetu hatuweki logo nyekundu yamepitwa na wakati.


Vodacom rangi zao ni nyekundu na nyeupe. Wapeni nafasi wajitangaze kama ambavyo mnatakiwa kufanya na kuwa na logo ya rangi hizo hakutaibadilisha Yanga.


Rangi za njano na kijani si za Yanga pekee, wala nyekundu na nyeupe si za Simba pekee. Tubadilike na kuonekana ni viumbe tulio katika karne au miaka tofauti na waliofikiri taratibu na kuwaza taratibu.

Kuna ile tabia baadhi ya timu zimekuwa zikicheza mechi bila ya kuwa na logo ya Vodacom zikisema kwanza si mdhamini wao maana anaidhamini TFF kwenye ligi.


Kwenye kuchukua fedha zao, wanakunja kama kawaida na hawasemi wanawadhamini TFF. Ushauri wangu Bodi ya Ligi na TFF wanapaswa kuwa wakali na kulisimamia hili ili mwisho, Vodacom wapate wanachotaka na kushawishika kuendelea na kuongeza mkwanja zaidi.


Kama Vodacom hawatalalamika, hata wadhamini wengine watashawishika kujitokeza kuwatoa Vodacom na kuongeza fedha au kuwekeza hata katika timu nyingine za Ligi Kuu Bara.

Iwapo mambo yatakwenda kwa kufuata weledi, wadhamini wengine wanaweza kushawishika na kujitokeza kudhamini Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa wataona kuna faida.


Wakati Vodacom wakiwa wadhamini, kuna wale watakaokuwa wamekaa pembeni wakiangalia namna ya kuingia. Hivyo lazima kuwaonyesha Vodacom wamefaidika na wakati huo mpira wa Tanzania utakuwa unafaidika na timu zitapunguza gharama za uendeshaji au kulainisha ugumu unaotokana na gharama.



Kumbukeni, Vodacom wamerejea kwa kuwa wanajua umuhimu wa Ligi Kuu Bara, sasa nanyi muonyeshe mnaujua umuhimu wao na kufuata pia kutimiza vipengele na TFF na TPLB wanapaswa kulisimamia hilo kwa kuwa kama wakati mwingine wakishindwa na kujiondoa, basi mchawi atakuwa anatokea ndani yetu yaani TPLB, TFF au timu shiriki, hivyo msije mkamtafuta mchawi mwingine na mwisho muanze kulialia kuzidiwa na gharama za uendeshaji wakati wapo wanaoweka fedha zao na nyie mnawafanyia ya kubabaisha.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic