FEDHA ZA EMMANUEL OKWI ZAIBULIWA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU, KAZI IPO
Wiki jana kwenye Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu palikuwa pa moto. Fedha za mauzo ya Emmanuel Okwi kwenda Etoile du Sahel zilizidi kuibua mambo mapya kupitia mashahidi mbalimbali mbele ya Mahakama.
Kesi hiyo inawakabili waliokuwa viongozi Simba, Rais Evans Aveva na makamu wake Godfrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope.
Mashahidi wawili waliunguruma wiki hii kuelezea jinsi mchakato wa dola 300,000(zaidi ya Sh.mil 600) zilivyotumika.
SHAHIDI WA TAKUKURU
Huyu ni shahidi namba saba,Frank Mkilanya Mchunguzi kutoka Takukuru na namba nane Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Kassim Dewji. Mkilanya alisema kuwa yeye alipewa kazi ya kuchunguza fedha kiasi cha dola 300,000.
Aliiambia mahakama kuwa fedha hizo sehemu ilitumika katika ujenzi wa Uwanja wa Bunju ambapo mkandarasi alipewa kiasi cha dola 50,000 na dola 60,000 kwa ajili ya
ununuzi wa nyasi hizo bandia. Lakini pia alisema fedha ambazo zilisalia Aveva alitumia kwenye mambo yake binafsi,ila shahidi huyo alidai hakuwahi kupitia hesabu zozote za Simba.
KASSIM DEWJI
Kigogo wa Simba, Kassim Dewji kwenye ushahidi wake aliielezea Mahakama akiwa kama mjumbe wa kamati ya utendaji zilipofika fedha za Okwi waliitwa kama kamati wajadili kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Akasema kwa kuwa Simba ilikuwa ina madeni kwanza walilipa deni la Zacharia Hans Pope (Mtuhumiwa namba tatu) ambazo ni dola 17,000(zaidi ya Sh.Mil39) na fedha zilizobaki walikubaliana ifunguliwe akaunti maalumu ambapo fedha hizo zitakuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja.
Hivyo Rais (Aveva) na Mhasibu (Amos) ndiyo walitakiwa kushughulikia hiyo na kamati iliundwa ambayo itasimamia ujenzi huo wa Bunju Project lakini akasema hakufahamu kama akaunti ilifunguliwa.
KESI ITAENDELEA
Kesi hiyo itaendelea Jumatano hii ambapo shahidi mpya ataunguruma mahakamani hapo. Mashitaka yanayowakabili watuhumiwa mbali na lile la kutakatisha fedha ni kuwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577(zaidi ya Sh.Mil 93).
wafungwe tu maana wamezidi kutuadaa
ReplyDelete