KAMA UNAMSEMA VIBAYA FALCAO HUYU HAPA ZAHERA AJA KIVINGINE
Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, amesema kuwa bao alilolifunga mshambuliaji wake David Molinga 'Falcao' litamuongezea hali ya kujiamini.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mshambuliaji huyo kufunga bao lake la kwanza tangu atue kuichezea timu hiyo wakati walipocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba FC ya Mwanza juzi CCM Kirumba.
Mshambuliaji huyo mwenye umbile kubwa, alijiunga na timu hiyo kwenye msimu huu kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea FC Lupopo ya DR Congo.
Zahera alisema kuwa mshambuliaji huyo anatakiwa kufunga mabao mengine mawili ili aongeze hali ya kujiamini na kufunga mabao zaidi.
Zahera alisema tatizo kubwa alilokuwa nalo Molinga ni kutocheza mechi nyingi za kimashindano, hivyo michezo ya kirafiki anayoendelea kuicheza itazidi kumuimarisha.
Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo bado anaendelea na programu ya kupunguza uzito ambao anatakiwa kupungua kilo nne.
“Molinga bado anahitaji kupunguza kilo nne ili kurejesha makali yake ya kufunga mabao, hiyo ni baada ya kukaa nje ya uwanja muda mrefu bila ya mazoezi mara baada ya ligi kumalizika.
“Ni matarajio yangu kumuona Molinga akiendelea kufunga mabao zaidi baada ya leo (juzi) kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Yanga ambalo ninaamini litamuongezea hali ya kujiamini.
“Hivyo, naomba mashabiki waendelee kumsapoti Molinga akiwa uwanjani ili aongeze hali ya kujiamini, nina imani kubwa na Molinga, ni suala la muda pekee,” alisema Zahera.
Zahera ambaye ndiye aliyependekeza usajili wa straika huyo anayevaa namba 22, amesema kuwa ana imani kuwa atakuwa tishio kubwa kwenye ligi ya Bongo na kimataifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment