September 3, 2019








Na Saleh Ally
HAPO kabla ni aghalabu sana kuona timu zikitoa nafasi kwa wachezaji wake wa zamani kuwa makocha. Ilikuwa ikifanyika kwa nadra kwa kuwa wazalendo hawaaminiki.

Ziko timu zilijitahidi kiasi fulani, mfano Simba walitoa nafasi kwa nyota wao kama akina Abdallah Kibadeni, Jamhuri Kihwelo na wengine na Yanga wakafanya hivyo kwa akina Charles Boniface Mkwasa maarufu kama Master, Juma Pondamali, Fred Felix Minziro ‘Baba Isaya’ na wengine.

Mwendo huo umekuwa mzuri kwa kweli maana tumeona umefanikiwa kuzalisha makocha kadhaa ambao wamekuwa msaada kwenye mpira wa Tanzania.

Wako waliopata mafanikio makubwa wakiwa makocha wakuu au wasaidizi na kuifanya Tanzania ibaki inajivunia jambo fulani.

Tatizo kubwa suala hilo limekuwa halina mwendelezo kwa maana kwamba makocha wanapewa nafasi hizo na baada ya muda wanatolewa, jambo ambalo linaonekana kuwakatisha tamaa na wanaamua kukaa kando.


Hakuwezi kuwa na mafanikio kwa kufanya kazi katika timu zao timu, wakati mwingine Yanga na Simba zinakuwa zinahitaji makocha wa kiwango cha juu zaidi kutoka nje ya nchi yetu.

Makocha hawa, wanakuwa faida kwa kuwa kwa kiasi kikubwa makocha hao wa Yanga na Simba, wanaambulia jambo ambalo watabaki nalo na kuwa msaada hapo baadaye.

Jambo ambalo linatakiwa kufanyika kwa ajili ya mwendelezo, linatakiwa kuwa la pande zote. Kuanzia kwa makocha wenyewe na upande wa klabu.

Klabu:
Upande wa klabu, lazima kuwe na mwendelezo unaoanzishwa na ushawishi kwa makocha hasa kwa wale wanaokuwa wanakwenda kustaafu, washawishiwe na kupelekwa kwenda kusoma katika kozi za ukocha.

Wakiwa mwishoni wanamalizia soka, wataendelea kusoma hadi kufikia kuwa na vyeti vinavyowaruhusu kuwa makocha wanaoweza kufundisha katika soka la ushindani.

Baada ya hapo, pale wanapostaafu tu, basi klabu zinawapa timu zao za vijana au wasichana na taratibu wanaendelea kujifunza na kufanya kazi.

Hapa kuna mambo mawili, faida kwa makocha wenyewe lakini kwa klabu pia ambayo itafaidika kwa kuwa makocha hao watakuwa na mapenzi na timu zao na wataifanya kazi kwa kujituma na hata kunapokuwa na shida au upungufu, wanaweza kuwa wavumilivu.

Upande wa makocha wenyewe, pia watafaidika kwa kuwa watakuwa wanaifundisha timu wanayojua mazingira na watakuwa tayari kupambana hata kunapokuwa na hali ngumu na hii husaidia uvumilivu unaweza kuzalisha mambo mazuri.


Makocha:
Iwapo makocha wakipata nafasi ya kujiendeleza kuanzia katika klabu zao, basi hawana sababu ya kusita inapofikia wameondolewa kwa kuwa mchezo wa mpira unapoajiriwa, basi ujue kufukuzwa hakuko mbali.

Baada ya Simba au Yanga basi unaweza kutafuta nafasi nyingine. Kati ya makocha wamekuwa mfano wa kuigwa ni Selemani Matola ambaye baada ya kuondoka Simba, ameendelea kupambana bila ya kusimama au kuchoka.

Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ pia, amefundisha timu kadha wa kadha na kazi yake imeonekana, hata kama kuna upungufu lakini kuna mazuri yake ambayo ni mfano wa kuigwa kutokana na kazi yake.

Mtibwa Sugar, ndio huenda imekuwa na mfumo mzuri zaidi wa kutoa nafasi kwa wachezaji wake wastaafu na unaona Mecky Maxime hata baada ya kuondoka Mtibwa Sugar, ameendelea na Kagera Sugar na ana nafasi ya kufanya vizuri zaidi.


Lazima makocha wakubali changamoto na upigaji hatua na klabu zianze kuwajenga mapema na wao wakubali kufanya kazi katika mazingira waliyoyazoea lakini mazingira mapya zaidi.

Kwa namna Ligi Kuu Bara ilivyo, kama wachezaji wengi wanaokwenda kustaafu wangekuwa wanaingia kwa wingi katika ukocha, bila shaka Tanzania ingekuwa inaongoza kwa makocha wengi zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambao wangekuwa wamesambaa karibu katika kila nchi.


1 COMMENTS:

  1. Vita dhidi ya Yanga si ndogo....sasa tusubiri reaction ya wapenzi wa soka wa timu ya wananchi ....vurugu yake si haba ....itajengengeka dhana kuwa sheria na kanuni ziliundwa zikiwa na kusudio kwa mlengwa wa adhabu....Kuongoza Soka kwa chuki si "afya" kwa maendeleo ya mpira wa Tanzania....mapungufu ya kiutendaji na kiutawala yanapoainishwa na kusemwa inakuwa makosa....uhuru wa kukosoa na kutoa maoni ni uhuru wa kikatiba ambao kila mtu anao uhuru huu usikandamizwe kwa kutunga kanuni na sheria...ili kuzuia watu kukosoa mapungufu yanayotokea katika uendeshaji na usimamizi wa tasnia ya mchezo wa soka hapa Tanzania.

    USHAURI
    Yanga msitoke nje ya reli jiandaeni na Zesco mashabiki waujaze uwanja wa Taifa..ili muudhihirishie umma Yanga ni baba lao

    Ahsante

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic