September 3, 2019



MAMBO yanazidi kupamba moto kwenye michuano ya kimataifa ambapo wale wawakilishi wetu kimataifa wameweza kuzijua mbivu na mbichi baada ya kukamilisha michezo yao miwili ya hatua ya awali.

Ukubwa wa michuano hii unafanya kila timu kutafuta matokeo ndani ya uwanja na mwisho wa siku kilichopatikana ni matokeo ambayo hatuwezi kuyakataa zaidi ya kuyakubali.

Kuna vitu vingi ambavyo timu zetu zinatakiwa kujifunza na kufanyia kazi kwa umakini bila kujali ni aina ipi ya mashindano ambayo wanashiriki iwe ni kitaifa ama kimataifa ni kazi ya timu kiujumla kutafuta ushindi.

Nilizungumzia kuhusu Yanga kwa namna mashabiki ambavyo walikuwa wameitoa kwenye alama za ushindani na kuamua kutoipa nafasi ya kusonga mbele.

Pia sikuacha kutoa tahadhari kwa timu ambazo zililazimisha sare ugenini kuona ni namna gani zitawaheshimu wapinzani wake watakapokuwa kweye michezo ya marudiano nyumbani.

Kwa zile ambazo zilikuwa ugenini ilikuwa wazi kwamba hawatakuwa na presha watacheza mchezo wa kutafuta matokeo na wakifanikiwa kushinda mapema kazi inakuwa imemalizika.

Ndivyo ilivyotokea mwisho wa siku tunaona timu zililizolazimisha sare zimekubali kupoteza kwenye michezo yao ya marudiano.

Tukianza na KMC wao waliponzwa na hofu ya kushiriki michuano mikubwa pamoja na zile ahadi ambazo waliziweka kwa mashabiki wao kwamba wanapindua meza kibabe mwisho wa siku mchezo ukawa mkubwa kwao.

Licha ya kutengeneza nafasi bado walishindwa kufanya maajabu wakapoteza Uwanja wa Taifa mbele ya mashabiki zao kwa kufungwa mabao 2-1 ni maumivu ndani ya matokeo.

Hapa kwa KMC wana kazi ya kuanza upya kwa ajili ya msimu ujao na kuyafanyia kazi yale makosa ambayo yameonekana kwenye michuano hii ya kimataifa.

Simba ambao msimu uliopita walitinga hatua ya robo fainali kwenye michuano hii mikubwa Afrika wao pia wamepoteza na kufungashiwa virago jumla na wapinzani wao UD do Songo kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo kuwa  1-1.

Hapa wao walipoteza kwa kujiamini kupita kiasi kutokana na rekodi zao za msimu uliopita kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa Taifa.

Kupoteza mbele ya mashabiki wao pamoja na ubora wa kikosi chao ambacho wamekisajili kwa gharama kunapoteza furaha kwa mashabiki na kuwafanya wawe na maumivu.

Kikubwa ambacho kwa sasa mashabiki, benchi la ufundi pamoja na viongozi wanachotakiwa kufanya ni kukubali matokeo na kuanza upya kujipanga kwa wakati ujao.

Licha ya kufanya usajili wa kimataifa na kuhitaji wachezaji wao waweze kucheza michuano ya kimataifa safari yao imefika tamati wanapaswa wakubaliane na hilo kwanza ili maisha yaendelee wasianze kutafuta sababu.

Mpira hauna kanuni ya kukataa matokeo bali kanuni yake ni kukubali matokeo na kuyafanyia kazi yale makosa ambayo yamesabisha kushindwa kufikia malengo.

Kupoteza kwa Simba na KMC iwe funzo kwa wengine ambao 
wamepenya hatua ya awali na kutinga hatua ya mtoano kwenye michuano ya kimataifa.

Msimu ujao iwe ni wakati mzuri kwa Simba na KMC kujipanga 
kufanya vema na kufikia malengo ambayo walikuwa wamejiweka awali, wasife moyo ama kukata tamaa itawamaliza na kuwapotezea dira yao.

Mashabiki kwa kujitokeza pamoja na viongozi wote tuna kila 
sababu ya kuzipa pongezi timu zetu ambazo zimetutoa kimasomaso ambapo kwa upande wa kombe la Shirikisho  Azam wao wamepenya hatua ya awali huku Yanga nao wakipenya kwa upande wa Ligi ya Mabingwa.

Timu zote zilizoshinda zilitambua  kitu gani ambacho zinahitaji kwenye michuano ya kimataifa zikatambua kwamba ni aina gani ya mbinu ambazo zingewasaidia kupata ushindi mapema na mwisho wa siku ikawezekana.

Kazi bado inaendelea kwani safari moja huanzisha safari nyingine hakuna muda wa kupumzika zaidi kinachotakiwa ni maandalizi kwa ajili ya hatua ambazo zinafuata kwenye michuano ya kimataifa.

Raha ya mashabiki na Taifa kiujumla ni kuona wawakilishi wa kimataifa wanapata matokeo chanya kwenye michuano ya kimataifa na kila kitu kinawezekana endapo kutakuwa na mipango makini kwa kila mchezaji pamoja na benchi la ufundi.

Bado kazi inaendelea kwa wawakilishi wetu kimataifa na Taifa linawategemea katika kutafuta ushindi hasa kwenye michuano hii mikubwa ambayo inatarajiwa kuendela mwezi ujao.

Tayari wapinzani wa Yanga wameshajulikana kwamba watakuwa ni Zesco ya Zimbabwe hapa kazi ipo kutokana na ukweli kwamba timu hiyo ipo chini ya Kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina jambo linaloongeza ugumu katika michuano hii.

Azam wao wanakwenda kumenyana na Triangle FC na safari hii wao wataanzia nyumbani hapo ni muhimu kuona wanapata ushindi kwenye mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani na kwenda kumaliza hesabu ugenini.

Wachezaji wasijisahua kwa kupata ushindi wa kwanza nyumbani wakaamini kwamba itakuwa rahisi kushinda hakuna kitu kama hicho kila timu inahitaji ushindi na ile ambayo itashinda ni ile iliyojiandaa kufanya vema.

Tunaamini kila mchezaji atatumia uwezo alionao kutafuta matokeo chanya ambayo  yataipandisha timu na Taifa kwenye chati ya michuano ya kimataifa.

Na zile ambazo zimeyaaga mashindano zitapata utulivu wa kisaikolojia kwa kuyakubali matokeo na kuruhusu utulivu ndani ya timu bila kujali ainia ya usajili ambao wameufanya na malengo yao kuyeyuka mapema.

Endapo Simba itashindwa kuwa na utulivu kwa sasa na kuanza kuhangaika kutafuta sababu ya kushindwa ilihali huu ni mpira basi anguko lao msimu ujao kwenye soka litakuwa kubwa kupindukia,


1 COMMENTS:

  1. kwani umeona simba haina utulivu, umesikia wamemlalamikia mtu?, Simba imeshajua nini maana ya mpira kwa hiy usitarajie simba inavurugika kwani bado wananafasi ya kurudi mwakani hapo upo salehe?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic