BAADA ya kazi kubwa iliyofanywa na Taifa Stars Jumapili
ilipocheza dhidi ya Burundi mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la
Dunia 2022 nchini Qatar, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),limeanza
mikakati mipya ya kuona timu inafanya vema dhidi ya Sudan hivi
karibuni.
Taifa Stars itapambana na Sudan katika mchezo wa kuwania kufuzu
kushiriki Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika
mwakani nchini Cameroon.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kuwapongeza
wanakamati wote waliohusika katika kuhamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi
uwanjani kuiunga mkono Taifa Stars dhidi ya Burundi iliyofanyika katika Hoteli
ya Seacliff jijini Dar, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amesema kuwa mikakati
kwa ajili ya mchezo dhidi ya Sudan tayari imeshaanza.
“Kwanza kabisa niwapongeza mashabiki kwa kazi kubwa
ya kuiunga mkono Taifa Stars waliyoifanya dhidi ya Burundi, hakika ilikuwa ni
ya aina yake na ambayo sikuwahi kuiona.
“Hata hivyo, baada ya mechi hiyo sasa tunajipanga kwa ajili
mechi yetu ijayo ya Chan dhidi ya Sudan ambayo tutashiriki hivi karibuni.
“Tukifanikiwa kuwatoa Sudan basi tutakwenda katika fainali hizo
na tutakuwa tumeandika historia ya kushiriki fainali zote kubwa za Afrika ndani
ya kipindi kifupi,” amesema Kidau.
Katika hatua nyinge, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Hamasa ya
Taifa Stars, Haji Manara amesema: “Kwa upande wetu tumejipanga vilivyo kwa
ajili ya kutimiza majukumu yetu lakini pia niwaombe tu Watanzania wote
kuendeleza utamaduni wa kuja kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuiunga mkono timu
yetu ya taifa.
“Tulichofanya dhidi ya Burundi basi kiwe mara mbili zaidi
tutakapokutana na Sudan hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa," amesema.
0 COMMENTS:
Post a Comment