August 7, 2020

 TUMESHUHUDIA fainali ya Kombe la Shirikisho ikikamilika kwa bingwa kupatikana kwenye mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa pale Uwanja wa Nelson Mandela.

Nelson Mandela ilikuwa na kazi kubwa kutokana na fainali kuwa ngumu kwa timu zote mbili huku mashabiki wakijitokeza kwa wingi kuona namna kazi inavyofanyika uwanjani.

Pongezi nyingi kwa waandaaji pamoja na mashabiki bila kuwasahau mashabiki ambao walikuwa mstari wa mbele kuzipa sapoti timu zao ndani ya uwanja hili ni jambo jema.

Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) wanastahili pongezi kwa kuweka usimamizi mzuri na kufanya kila kitu kiwe sawa kwenye upande wa majukumu yao mpaka mwisho wa siku mshindi anapatikana.

Azam ambao ni wadhamini wakuu pia wamekuwa wabunifu kila wakati wanafanya mpira wetu unazidi kukua na kufungua wigo zaidi kitaifa na kimataifa.

Nimekuwa nikiwasiliana na marafiki zangu wengi kutoka nje ya nchi ambao wanatupa pongezi nyingi kwa kuwa na maendeleo kwenye suala la mpira kwa kuwa wanaona kupitia Azam TV.

Hili ni jambo la kujifunza pia kwa wachezaji wetu kuzidi kuonyesha ule uwezo wao wa asili pale wanapopewa nafasi ya kuanza ndani ya timu jambo litakalowaweka sokoni kwa wakati ujao.

Ndivyo ambavyo ilikuwa kwa timu zilizokuwa uwanjani pale Nelson Mandela kusaka ushindi kwenye mchezo wa fainali uliokuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa.

Namungo ilikuwa ikipambana na Simba pale na dunia nzima imeweza kushuhidia namna mambo yalivyokuwa kwa kuwa kwa sasa kila kitu ni teknolojia na mambo yanakwenda kwa kasi.

Msimu wa 2019/20 umefungwa huku Simba wakiwa ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa mabao 2-1 wanastahili pongezi kwa kuwa walipambana hata wapinzani wao pia Namungo nao wanastahili pongezi.

Kwa kushiriki fainali tu kwa timu zote inamaanisha kwamba zilikuwa na mipango tangu awali na hazijafika kwa bahati mbaya hivyo ni wakati mwingine kuendelea kupambana ili kuwa bora zaidi.

Yote kwa yote bado ninaona kwamba Uwanja wa Nelson Mandela ulikuwa mzuri ila changamoto kubwa sehemu ya kuchezea hasa kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho.

Ipo wazi kwamba  TFF inapenda kuona watu wake wakishuhudia mpira na kuwa karibu na burudani ila kuna jambo la msingi la kujiuliza gharama za matengenezo za ule uwanja ni namna gani zitadumu pale?

 

Nani ataendelea kuutumia Uwanja wa Nelson Mandela kwa sasa baada ya fainali ilihali gharama zimetumika katika kufanya maboresho?

Kitu kizuri TFF wamefanya kwani kwa sasa maboresho ambayo yamefanyika ni makubwa na mazuri hasa kwa upande wa vyumba vya kubadilishia nguo hapo wanastahili pongezi.

Wasiwasi wangu mimi ni kwa upande wa matunzo ya uwanja wenyewe namna utakavyokuwa usishangae mpaka msimu ujao utatelekezwa na usitumike hii ni hasara kubwa itakuwa.

Nikukumbushe kuwa msimu uliopita bingwa alipatikana kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi ilikuwa ngumu sana kupatikana kwa bingwa kutokana na sehemu ya kuchezea kutokuwa rafiki.

Mbali na sehemu ya kuchezea pia kule Lindi ilikuwa na changamoto kwa upande wa huduma jambo ambalo lilifanya fainali kuanza kuwa ngumu kabla ya wachezaji kuingia uwanjani.

Fikiria pia kuhusu gharama zilizotumika kukikarabati kiwanja cha Ilulu kwa ajili ya fainali ya siku moja nini kimetokea kwa sasa? Hakuna timu ambayo inatumia kiwanja kile baada ya fainali.

Hiki ndicho ambacho ninaona kinakwenda kutokea kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ni ngumu kuamini kwamba kazi yake imekwisha licha ya maandalizi kuwa mazuri.

Ushauri wangu kwa waandaaji kuna umuhimu wa kuweka  usawa katika maandalizi ya fainali ya Kombe la Shirikisho hasa kwa kuwa na sehemu moja ambayo itakuwa inajulikana na kila mchezaji tangu mwanzo wa mashindano.

Ipo wazi mashindano yana hadhi ya kimataifa na mshindi pia anapata nafasi ya kushiriki michuano mikubwa ya kimataifa hivyo itapendeza maboresho katika sehemu ya kuchezea fainali.

Wakazi wa Sumbawanga wamepata burudani na wamefurahi kuiona fainali kwa muda wa dakika 90 ambayo kwa sasa imekwisha kamilika kipi kitafuatia wakati ujao kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

Jambo la msingi pia ni kuona kwamba mamlaka husika zitaendelea kuutunza Uwanja wa Nelson Mandela ili uwe bora na imara zaidi wakati wote.

Bado tatizo la viwanja kwa timu zetu Bongo ni mkubwa hivyo kuna umuhimu wa kufanyia maboresho viwanja vyetu ili kushuhudia ushindani mkubwa kwa kila mchezaji pamoja na timu kutimiza majukumu yake kwenye sehemu ambazo wanazifurahia.

Yote kwa yote ninaamini kwamba fainali imeonakena na namna uwanja ulivyokuwa na shida kwa wachezaji kupambana kusaka ushindi hapo sasa ni wakati wa kulitazama suala la sehemu ya kuchezea fainali kwa umakini.

Kuiga sio jambo baya wala haina makosa ila kwa mambo mazuri tuone namna wenzetu ulaya namna wanavyoendesha mashindano haya licha ya kwamba sisi tupo zetu Bongo huku.

Wachezaji wanaanza kupambana na mambo mawili huko Ulaya, kwanza kupata nafasi ya kushiriki Kombe la FA ndani ya Uwanja wa Wembley ambao una hadhi ya kimataifa na ni uwanja mzuri pili kuweza kunyanyua taji ambalo hawataweza kulipata ikiwa hawatafika pale Wembeley kwa kutinga hatua ya fainali.

Mashindano ni mazuri na yanaushindani mkubwa muhimu tu kuangalia namna nyingine ambayo itapendeza kwenye upande wa kuwa na uwanja maalumu kwa ajili ya fainali tu ya Kombe la FA kisha mambo mengine yataendelea kama kawaida.Mbali na kwamba kwa sasa Uwanja wa Nelson Mandela umefanyiwa maborsho basi usiachwe hivihivi ni muhimu kuendelea kuutunza pia

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic