NA SALEH ALLY
MIAKA nenda rudi tumepambana na kuzungumza kuhusiana na namna ambavyo wachezaji wa Tanzania wamekuwa waoga kutoka nje ya nchi kupambana kutafuta maisha.
Tumezungumza kuhusiana na wachezaji kuboresha viwango vyao kwa kupata changamoto tofauti na nje ya nchi yetu.
Hakuna sababu ya ubishi kwa kuwa ni lazima kufanya hivyo kwa maana, hakuwezi kuwa na ubora kama wachezaji wetu wanakuwa na mawazo ya hapa nyumbani tu.
Changamoto mpya zinawaboresha, zinawabadilisha mawazo na aina wanayokuwa nayo wanapokuwa wameendelea kubaki hapa nyumbani.
Utaona tulilolipigia kelele sasa linaleta mabadiliko makubwa katika mpira wa Tanzania kwa kuwa tayari tuna wachezaji zaidi ya kikosi kizima wanaocheza nje ya Tanzania. Si lazima kwenda Ulaya tu, nje ya Tanzania hata kama itakuwa Kenya, Uganda, Burundi na kwingineko, bado ni nje tu.
Unapokutana na watu tofauti kutoka katika nchi na utamaduni tofauti, kupitia ushindani lazima kutaboresha kile ulichonacho kwa maana ya kutaka zaidi na hasa suala la mafanikio.
Ushindani unatengeneza ubora na unapokuwa nje ya nyumbani, aina ya upambanaji inakuwa juu zaidi kwa kuwa unajua umesafiri mbali kwenda kutafuta mafanikio na huenda unaanza kuyaona yakikufuata kila unapozidi kupambana.
Timu ya taifa leo inaita wachezaji zaidi ya sita, saba kutoka nje ya nchi katika kikosi chake kinapokuwa kinacheza. Wengine zaidi ya kumi wanakuwa hawajaitwa na lazima wanapambana nao wapate nafasi.
Hii tayari ni njia mpya ambayo inapaswa kushikiliwa hasa kutengeneza ubora unaojengwa na ushindani, jambo ambalo leo kwa mara nyingine nalirudisha upande wa walimu wa soka, yaani makocha.
Hapa nyumbani Tanzania tuna makocha wengi sana na wana uwezo mzuri sana. Lakini wamekuwa hawajiamini na muda mwingi si watu walio tayari kuchukua changamoto nje ya nchi yetu.
Wachache sana wamekuwa wakijaribu na bahati nzuri wanafanikiwa. Mfano, angalia Kocha Msaidizi wa Simba, Denis Kitambi, huyu ameajiriwa na Simba akitokea Kenya ambako alikuwa Kocha Mkuu wa AFC Leopards, moja ya timu kongwe za Kenya na Afrika Mashariki.
Kitambi alitokea Ndanda FC, baadaye Azam FC na akajaribu. Leo unaona amerejea Simba lakini tayari ni kocha mwenye jina na wigo wake wa ajira tayari ni mkubwa kwa kuwa anaweza kukubalika Kenya kwa urahisi sana kama ilivyo nchini lakini kwa nchi nyingine, hawawezi kusita kumpa kazi.
Makocha wengi wa Tanzania si watu wa kuthubutu ndiyo maana leo unaona, mfano msimu uliopita na uliopita, makocha kutoka Burundi walitawala Tanzania.
Nchi kama Burundi leo inaweza kuwa na makocha wengi zaidi nje ya nchi yao kuliko sisi Watanzania ambao tuna makocha wengi sana wenye elimu ya kufundisha, wakiwemo wale waliocheza katika kiwango cha juu.
Kuna kila sababu ya sasa kuanza kujiamini, makocha waendelee kujifunza hapa nyumbani, wajipatie elimu zaidi na baada ya hapo wasonge mbele kutafuta changamoto zitakazoboresha ubora wao zaidi.
Kama makocha wa Kenya na Uganda wamekuwa ndio tegemeo hapa kwetu, baadaye tumeona hata Warundi na Wanyarwanda nao wanajiamini. Vipi nchi kama yetu, yenye ligi bora na ushindani, changamoto nyingi tushindwe?
Ugenini hakuwezi kuwa sawa na nyumbani kwa maana ya kufanya kazi. Lakini kama tunataka maendeleo, lazima kukubali changamoto ili kutengeneza ubora wa baadaye.
Makocha wasiishie kulalamika kwamba wao ni wazalendo na hawaaminiki kama wageni. Kama wameona hivyo, basi wakapambane nje na hasa kwa wale ambao CV zao zimeanza kujitosheleza ili malalamiko yasije kuwa msingi wa maisha ya baadaye. Mkiamua inawezekana na italeta mabadiliko.
0 COMMENTS:
Post a Comment