Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli wikiendi iliyopita alimshauri Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Maganga kuangalia upya ishu ya watuhumiwa wa makosa ya utakatishaji fedha walioko mahabusu.
Miongoni mwa mahabusu hao ni viongozi mbalimbali wa michezo ambao jumla ya fedha wanazotuhumiwa nazo ni zaidi ya Sh.Bil 1.3. Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rais watuhumiwa hao wamepewa mpaka Jumamosi tu kuomba msamaha vinginevyo wataendeleza kusota.
Rais Magufuli alimshauri DPP kwamba ndani ya wiki moja kuanzia Jumatatu wiki hii mpaka keshokutwa Jumamosi kwa mtuhumiwa yeyote ambaye atakuwa tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha alizotakatisha asikilizwe na uangaliwe utaratibu wa kumsamehe arudi uraiani kuchapa kazi na kujenga uchumi wa nchi.
“Wapo watu kule wanateseka, unawaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli, inatia huruma inaumiza.
“Lakini inawezekana kuna wale walipenda kuomba msamaha, waje kwako wewe DPP wasimamie hilo upange utaratibu wa kurudisha hizo fedha ili waje kushiriki kujenga taifa,” alisema Rais Magufuli.
“Unamkuta mwingine alishindwa kulipa kodi akafoji, anadaiwa labda Bilioni 2 aombe msamaha sitafoji tena alipe hizo fedha,”alisisitiza.
“Wapo wengine walikuwa na fedha za kutakatisha, atubu kwamba sitatakatisha tena, nitakuwa nataka katika kufanya biashara ya kweli. Kwamba dhambi ya kutakata nimeiacha, aje atoke kule alipe hiyo hela anayodaiwa, haya ni mapendekezo sijaingilia mahakama, ninapendekeza hivyo,” alisisitiza Rais Magufuli.
Kauli hizo za msamaha za Rais Magufuli huenda zikawanufaisha viongozi wa michezo walioko mahabusu na wanaoteseka kama watakuwa tayari kuomba msamaha na kuwa tayari kulipa. Lakini wakishindwa kufanya hivyo mpaka kufikia Jumamosi nafasi hiyo itafungwa.
Makosa hayo yamesababisha viongozi hao kuendelea kusota ndani kutokana na kukosa dhamana.
- Jamali Malinzi na wenzake
Katika kesi hii inayomjuisha aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Jamal Malinzi na katibu wake Celestine Mwesigwa, Mhasibu Nsiande Mwanga, na Karani, Flora Rauya.
Washitakiwa hawa awali kabisa walisomewa mashitaka yapatayo 28. Katika makosa hayo baadhi ni ya utakatishaji fedha ambayo yaliwaweka ndani. Isipokuwa washitakiwa wawili Flora Rauya na Miriam Zayumba ambaye tayari aliondolewa kwenye kesi hiyo baada ya kukutwa hana kesi ya kujibu.
Washitakiwa hao wote ambao kwa sasa wapo kwenye hatua ya kujitetea na tayari Malinzi amekamilisha zoezi hilo kama mshitakiwa namba moja na Mwesigwa ndiyo anaendelea kuhojiwa.
Katika mashitaka yale 28 ambayo yalisomwa katika kesi hii ya kina Malinzi moja wapo lilikuwa ni kosa la utakatishaji fedha.
Katika yale mashitaka, shitaka namba 26 inadaiwa kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, Malinzi, Mwesigwa na Nsiande Mwanga kwa pamoja walitakatisha fedha kiasi cha dola 375, 418(zaidi ya Sh.Mil 860).
Shitaka la 28 Nsiande Mwanga anadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, 2016 katika ofisi za TFF aliwasaidia Malinzi, Mwesigwa kujipatia kiasi dola 375, 418 (zaidi ya Sh.Mil 860).
- Kesi ya Evans Aveva, Geofrey Nyange na Zachariah Hans Poppe
Ni kesi ambayo kwa sasa imeteka akili za wengi hususan mashabiki na wapenzi wa klabu ya Simba pamoja na familia za washitakiwa.
Hii ni kutokana na utata ulioibuka wiki iliyopita ambapo Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alitoa uamuzi juu ya kesi hiyo na kuwa washitakiwa Aveva na Nyange makosa yao mawili ya utakatishaji fedha walifutiwa na walikuwa na uwezo wa kupata dhamana.
Lakini serikali imekata rufaa juu ya uamuzi huo wa mahakama kuhusu kufutiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha hivyo uamuzi mwingine unasubiriwa kesho Ijumaa mahakamani.
Aveva na Nyange wanakabiliwa na mashitaka tisa, mawili yalikuwa ya utakatishaji fedha.
Shtaka la tano, Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za Kimarekani 187,817(zaidi ya Sh.Mil 430) wakati akijua zimetokana na kughushi.
- Michael Wambura
Alikuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini alivuliwa nyadhifa zote za soka na Fifa baada ya kubaini alifanya makosa.
Kesi yake ilifunguliwa mwaka huu na mpaka sasa haijaanza kusikilizwa kutokana na upelelezi kushindwa kukamilika na jalada lake liko kufanyiwa marekebisho kwa DPP.
Alishitakiwa na makosa 17 ambayo mpaka sasa hajaanza kusikilizwa lakini katika mashitaka hayo yanayomkabili kigogo huyo inadaiwa kuwa alitakatisha fedha.
Inadaiwa kuwa Wambura alitakatisha fedha kiasi cha Sh.Mil 75 wakati akilitumikia shirikisho hilo.
0 COMMENTS:
Post a Comment