HARUNA
Shamte, mtaalamu wa mipira iliyokufa ambaye msimu uliopita alikuwa ndani ya
Lipuli sasa ujuzi wake huo utaonekana ndani ya kikosi cha Mabingwa watetezi
Simba.
Ana uwezo mkubwa
wa kutumia mguu wa kulia ambapo amefunga jumla ya mabao matano alipokuwa Lipuli
na yote ilikuwa ni mipira ya nje ya 18 tena ya adhabu.
Katika mabao
hayo mawili alifunga kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo ilichezwa Uwanja wa
Samora kwenye mechi dhidi ya Singida United pamoja na mchezo wao dhidi ya Yanga
ambapo Klaus Kindoki alikuwa langoni.
Mabao
mengine matatu alifunga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na alitimiza
wajibu wake kwa kuipeleka timu ya Lipuli hatua ya fainali na ilipoteza mbele ya
Azam FC.
Amewahi
kuzitumikia timu mbalimbali Bongo ikiwa ni pamoja na Mbeya City, JKT Ruvu na Simba msimu wa 2014/15 sasa amerejea nyumbani ambapo anakutana na
mabeki kama Pascal Wawa, Yusuph Mlipili, Gadiel Michael, Mohamed Hussen na
mkongwe Erasto Nyoni, huyu hapa anafunguka:-
“Kazi kubwa
ambayo nimekuwa nikifanya uwanjani wengi wameipokea vizuri na imenipa matokeo
mazuri ambayo kwa sasa yanaonekana hivyo kwangu ni kitu cha kujivunia na
ninafurahi kufanya hivyo.
Polisi Tanzania walikuwa wanakuhitaji
dili iliishia wapi?
“Kweli
ilikuwa inasemwa hivyo na ukiangalia kwamba kwa sasa pale mwalimu wao ni
mwalimu wangu wa timu ya zamani (Seleman Matola) namheshimu na ninamkubali ila
mwisho wa siku nimetua Simba na maisha yanaendelea.
Kwa nini umechagua kutua Simba?
“Kazi yangu
mimi ni mpira kikubwa ambacho ninaangalia ni dau, niliwekewa dau kubwa
nikakubali kusaini hivyo sina mashaka na chaguo langu kwa sasa ambalo nimelifanya.
Unadhani kipi unachohofia ndani ya
Simba?
“Kwa sasa
bado kwa kuwa ligi bado mbichi ila tuna kazi kubwa ya kufanya na mambo ni
mengi kwa sasa hivyo suala la hofu kwangu hakuna kitu kama hicho kwa kuwa yote
ambayo yanatokea ni mipango ya Mungu.
Ulikuwa na uhakika wa namba ndani ya
Lipuli je nafasi yako ndani ya Simba unaionaje?
“Kuanza ama
kutokuanza ni maandalizi tu, naona kuna wachezaji wengi wazuri ambao
wamesajiliwa hilo sio jambo baya kwani hata nilikotoka Lipuli kulikuwa na
mabeki wazuri wachezaji wazuri ambao tulikuwa tunafanya vizuri ila mwisho wa
siku kazi ya kupanga kikosi ipo chini ya mwalimu.
Wingi wa mashabiki na ukubwa wa timu
ya Simba kwako unakupa picha gani?
“Natambua ni
timu kubwa ila nimewahi kuitumikia zamani hivyo sina mashaka na presha ambazo
zipo ninachokifanya kwa sasa ni kujiaandaa vema na kupambana ili kuwa bora.
“Mashabiki
ni watu muhimu kwenye soka kwani ni mchezaji wa 12 hivyo wingi wao na sapoti
yao kwetu ni muhimu katika kila jambo.
Umesajiliwa dakika za mwisho je
unaamini ulikuwa kwenye mpango wa Simba?
“Kuwa kwenye
mpango ama kutokuwa ndani ya mpango hilo mimi sijui, ninachojua kwa sasa
mipango imetimia na nipo ndani ya Simba kwa sasa.
“Kikubwa kwa
mchezaji anachotazama ni sehemu ambayo anakwenda kucheza pamoja na thamani yake
hivyo kama nimepata dili la kujiunga na Simba sikuwa na namna ya kugoma eti kwa
sababu nimechelewa kusajiliwa.
Mashabiki wa Simba unawaambia nini?
“Mshikamano
na umoja ni vitu vya msingi, sapoti yao ni kubwa na wanaonyesha kwa vitendo
hivyo napenda kuwaomba waendelee na moyo huo kwa ajili ya kuipa sapoti timu.
Mabao yako mengi ni mipira iliyokufa
kwa nini?
“Wakati ule
mwalimu (Matola) alikuwa ananipa kazi ya kufanya na nikiwa mazoezini nilikuwa
nafunga mengi, hivyo mbinu bado ipo na ujuzi haupotei ni jambo la kusubiri na
kuona kikubwa subira na dua,” anamalizia Shamte.
0 COMMENTS:
Post a Comment