MCHEZAJI SIMBA AMTAKA NDAYIRAGIJE KUMUITA TEGETE STARS
Aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Simba, Dua Said, amemtaka Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mrundi, Etienne Ndayiragije, kuhakikisha anamuongeza straika wa Alliance FC, Jerryson Tegete aliyewahi kuichezea Yanga, ili kuipa nguvu safu ya ushambuliaji.
Kauli ya Dua imekuja kufuatia safu ya ushambuliaji katika kikosi cha Stars kuonekana na mapungufu ambayo anaamini kama Tegete atarejeshwa, ataweza kusaidia kufunga mipira ya vichwa ambayo imekuwa ikipotea bila kufanyiwa kazi.
Mchezaji huyo aliyeitendea haki nafasi yake wakati akiichezea Simba miaka ya tisini, ameeleza safu ya ushambuliaji ya Stars imekuwa ikipoteza mipira ya krosi za juu ambayo inaweza kufanyiwa kazi na mtu kama Tegete kutokana na urefu wa umbile lake.
Said amefunguka akieleza namna ambavyo Stars ilishindwa kutumia mipira hiyo katika mchezo wa kuwania kufuzu CHAN dhidi ya Sudan uliopigwa Jumapili iliyopita huku ikifungwa bao 1-0, akiamini pengine kama Tegete angekuwepo angeweza kufunga.
"Kikosi chetu kimekuwa na upungufu katika safu ya ushambuliaji, pengine tungekuwa na mtu kama Tegete pale mbele tungeweza kufunga.
"Tegete ni mrefu na naijua kazi yake tangu akiwa na Yanga, hata huyu wa Alliance ni mzuri ambaye mimi naamini akiitwa lazima aingie kambani.
"Ukiiangalia timu vizuri unaona kabisa pale mbele hakuna mpigaji wa mipira ya vichwa mzuri, laiti kama Ndayiragije akimuongeza Tegete, hiyo nafasi ataitendea haki vizuri," alisema.
Na George Mganga
0 COMMENTS:
Post a Comment