September 27, 2019


Mabosi wa Yanga wamepokea barua ya kuondoka kiungo wao mkabaji Mkongomani, Papy Tshishimbi kuhitajika na moja ya klabu ya nchini China.

Bado majadiliano baina mchezaji huyo na klabu yanaendelea lakini huenda akawashtua mashabiki wa Yanga kwani anaweza kuondoka kabla ya mechi ya watani Januari mwakani.

Staa huyo ni kati ya wachezaji tegemeo hivi sasa wanaounda safu ya kiungo na hivi karibuni aliongezewa mkataba wa miaka miwili ingawa yeye alikuwa akishinikiza miezi sita kwa vile alishasikia harufu ya dili hilo.

Tshishimbi kwenye usajili wa msimu huu alikuwa akitajwa kutua Simba kabla ya Yanga kumuwahi na kumuongezea mkataba huo ambao yeye alikuwa hataki mrefu lakini Kocha Mwinyi Zahera akasisitiza iwe hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, barua hiyo ya kumuhitaji Tshishimbi ilitua hivi karibuni na baada ya mechi ya Zesco wanaweza kufanya uamuzi wa mwisho.

Habari zinasema uongozi umekuwa ukisisitiza kumalizia mzunguko wa kwanza au kusubiri mpaka dirisha dogo ili wapate nafasi ya kujaza pengo lake lakini bado hawajafikia muafaka ila uwezekano wa kuondoka kabla ya mechi ya Simba Januari mwakani ni mkubwa.

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema kuwa “Hilo suala lipo kwa viongozi bado linaendelea kujadiliwa, hivyo ni ngumu kuliweka wazi muda huu.”

“Kama unavyofahamu hivi sasa tupo bize na mchezo wetu wa marudiano, tusubirie mechi hii imalizike kwanza ndiyo nitakuwa kwenye sehemu nzuri ya kulizungumzia hilo,”alitamka kwa kifupi kiongozi huyo wa zamani wa TFF na Mtibwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic