September 26, 2019


MICHUANO ya kimataifa inazidi kusonga mbele na tayari  wawakilishi wetu kimataifa wameweza kuvuna kile ambacho wamekipanda kwenye hatua ya kwanza ya michuano hii ambayo imeanza kwa kasi.

Ugumu wa michuano hii unafanya kila timu kujivunia kutafuta matokeo ndani ya uwanja hasa wanapokuwa nyumbani kutokana na kuwa na mashabiki wao pamoja na uzoefu wa uwanja wanaoutumia.

Kwa wawakilishi wetu kimataifa ambao ni Yanga na Azam FC kwao imekuwa ni tofauti kidogo mambo yamegeuka chini juu juu chini inasikitisha ila ndio mpira namna ulivyo.

Kuna mengi ambayo timu zetu zinatakiwa kujifunza na kufanyia kazi upesi bila kutazama  aina ya matokeo ambayo wameyapata kwa sasa kwenye michezo yao ya kwanza wakiwa nyumbani.

 Tunaona wakiwa uwanja wa nyumabi wawakilishi kwenye Kombe la Shirikisho, Azam FC wao wamekubali kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 mbele ya Triangle United baada ya dakika tisini za awali.

Kwa upande wa wawakilishi wetu kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga wao pia walilazimisha sare kwenye mchezo wao dhidi ya Zesco United wakiwa uwanja wa Taifa.

Kufungana bao 1-1 kwenye michuano ya kimataifa sio kitu chepesi inaamaanisha kazi ilikuwa nzito na mwisho wa siku kila timu imepata faida kutokana na uzembe wa timu fulani ndio maana imepata goli.

Tunaona timu zote zimepata aina ya matokeo ambayo yanafanana kama walipoanza kwenye hatua ya awali hii inamaanisha kwamba 
bado mbinu za walimu hazijabadilika kwenye kutafuta matokeo.

Ikumbukwe kwamba wakati wa michezo ya awali Azam wao walikuwa ugenini na walicheza na Fasil Kenema nchini Ethiopia ambapo walifungwa bao 1-0 kabla ya kupindua meza kibabe nyumbani.

Yanga nao pia walianza uwanja wa Taifa kwa kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Township Roller kabla ya kwenda ugenini na kupindua meza kibabe.

Tofauti hapa imekuja kwa Azam tu ambao wapo kwenye hatua ya Kombe la Shirikisho ambapo safari hii wameanza kupoteza kwenye uwanja wao wa nyumbani ambao walipindulia meza mbele ya wapinzani wao kutoka Ethiopia.

Kwa matokeo ambayo yametokea kwa wakati huu hakuna muda wa kuanza kupoteza kwa kulalamika ama kujilaumu tayari matokeo yameshatokea hakuna atakayeweza kuyabadilisha.

Kinachotakiwa ni kupanga mikakati upya ya kwenda kumaliza mchezo ugenini kwa kuwa kwenye michuano ya kimataifa mchezo wa kwanza ni sehemu ya kwanza na sehemu ya mwisho inakamilika baada ya mchezo wa pili.

Huku dakika 90 zinagawanywa mara mbili za awali nyumbani kisha zinazokamilika kabisa ni baada ya filimbi ya mwamuzi mchezo wa pili hapo ndipo hatma ya timu husika inakuwa wazi.

Azam FC wana kazi ya kutafuta ushindi ugenini kimataifa sawa na Yanga na inawezekana kupindua meza kibabe kama ilivyokuwa awali na mashabiki na wale ambao walikuwa wamekata tamaa hawataamini macho yao.

Jambo la msingi kwa wachezaji na viongozi bila kusahau mashabiki ni kutambua kwamba mpira kwa sasa umebadilika tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kila kitu kimekuwa wazi sana jambo ambalo linafanya timu nyingi kupata ushindi na matokeo sehemu yoyote kwa namna ambavyo zinataka ila ni pale tu ambapo zinakuwa zimejiandaa kufanya hivyo.

Wachezaji wanapaswa kujipa majukumu upya na kutambua kwamba wanafanya kazi kwa ajili ya Taifa la Tanzania kiujumla sio kazi ya klabu pekee waliyonayo kwa sasa.

 Kupoteza mbele ya mashabiki kwenye uwanja wa nyumbani ama kulazimisha sare kunapoteza furaha kwa mashabiki na kuwafanya wawe na maumivu sasa muda wa kuwatibu ni kwenye mchezo wa marudio.

 Mashabiki, benchi la ufundi pamoja na viongozi wanajukumu la kukubali matokeo na kuanza kupiga hesabu za mbele kwenye mchezo wa marudio namna watakavyokwenda kupeperusha bendera kimataifa.

Sheria ya kukataa matokeo kwenye mpira haipo na haijawahi kutokea ila cha msingi ni kuyapokea matokeo na kufanya hesabu kuona wapi ambapo timu ilikwama kupata kile ambacho kilikuwa kinastahili kwa wakati.

Kupoteza kwa Azam iwe funzo kwao kwamba rekodi zimewekwa ili zivunjwe na wao sasa wana kazi ya kwenda kuvunja rekodi ugenini kwa kupata ushindi.

Ukweli ni kwamba Azam FC kwenye michuano ya kimataifa walikuwa hawajawahi kupoteza mchezo hata mmoja nyumbani ila imewezekana na ulimwengu umeshuhudia ikifungwa bao 1-0 tena dakika za kipindi cha kwanza.

Kama wapinzani wameweza kupata matokeo kwenye uwanja wenye histotia kwenye michuano ya kimataifa sasa je nini ambacho Azam itashindwa ikiwa ugenini kupata matokeo chanya?

Kila kitu kinawezekana kinachotakiwa kwa muda huu ni kufanya maandalizi ya nguvu mwanzo mwisho bila kujali matokeo ya mwanzo, yale makosa ambayo yametokea ni ya kufanyia kazi.

Inaonekana kuna tatizo kubwa kwenye safu ya ushambuliaji hasa kwa kushindwa kumaliza nafasi ambazo zinatengenezwa wakiwa uwanjani.

Hili lipo wazi tunaona namna ambavyo Azam FC wao waliweza kumilika mpira kisha wakashindwa kulimiki goli la mpinzani hapa kuna jambo la ziada inabidi lifanyike.

Washambuliaji wajitathimini na watambue kwamba timu inahitaji ushindi na wao wana jukumu hilo, kwenye safu ya ulinzi nako pia kuna jambo linapaswa lifanyike ila huku sio kubwa sana kama ilivyo kwenye safu ya ushambuliaji.

Yanga wao wamekuwa na tatizo la kujisahau mara wanapopata ushindi hasa dakika za mwisho kwa kuamini kwamba mpira umekwisha hili ni kosa kubwa ambalo linaigharimu timu.

Pia umakini wa wachezaji wakiwa ndani ya uwanja unapungua kadri muda unavyozidi kwenda, hapa kuna umuhimu wa wachezaji kutambua kwamba hawashiriki ligi, wapo kwenye michuano ya kimataifa.

Huku ni mwendo wa kukimbizana mwanzo mwisho bila kujali mpira ndo unaanza ama unaelekea ukingoni hakuna kitu kama hicho ni lazima wachezaji wabadilike kuelekea kwenye mchezo wa marudio.

Timu zote zinazoshiriki kwenye michuano ya kimataifa zikitambua kwamba ni aina gani ya mbinu ambazo ziliwasaidia kupata matokeo awali kisha kufanyia makosa pale walipofeli itawasidia kupata ushindi mapema na mwisho wa siku zikasonga mbele.

Safari moja huanzisha safari nyingine hakuna muda wa kupoteza kinachotakiwa ni maandalizi kwa ajili ya michezo ya marudio inayotarajiwa kupigwa kati ya Septemba 27-29.

Furaha ya mashabiki na Taifa kiujumla ni kuona wawakilishi wa kimataifa wanapata matokeo chanya kwenye michuano ya kimataifa na inawezekana endapo kutakuwa na mipango makini kwa kila mchezaji pamoja na benchi la ufundi.

Kwa wawakilishi wetu kimataifa wanapaswa watambue kuwa Taifa linawategemea katika kutafuta ushindi hasa kwenye michuano hii mikubwa ambayo inaendelea.

Tayari Yanga wameshajua mbinu za wapinzani wao Zesco ambao walicheza nao kwenye mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa na kuambulia sare ya kufungana bao 1-1.

George Lwandamina ambaye ni Kocha Mkuu wa Zesco anawatambua vema wapinzani wake ukizingatia kwamba amekaa nao kwa muda mrefu na falsafa zao anazijua ila hilo sio jambo la kuliogopa sana kwa sasa.

Kinachotakiwa ni kubeba ujasiri mkubwa na kuwafuata wapinzani mkiamini kwamba mnaweza kupata matokeo kama ambavyo wao walipata matokeo nyumbani kwenu mkiwa na mashabiki wenu pia.

Azam safari yao ya kuwafuata Triagle FC nchini Zimbabwe ndiyo inayofuata hapa wakiwa wana kazi ya kwenda kupindua meza ugenini ni kitu ambacho kipo mikononi mwa wachezaji wenyewe.

Wachezaji wasiwadharau wapinzani kwenye mchezo wa marudio kwa kuwa tayari wameshazijua mbinu zao za awali hapana mpira hauhitaji dharau bali umakini na hesabu kali za kutafuta ushindi.

Tunaamini kila mchezaji atatumia uwezo alionao kutafuta matokeo chanya ambayo  yataipandisha timu na Taifa kwenye chati ya michuano ya kimataifa.

Zile tambo za makocha wa kigeni kwamba wao wakiwa nyumbani ni wa moto na wanashinda michezo yao yote waliyocheza kimataifa ni za kishkaji tu na kawaida kwenye michezo.

Kama ambavyo hata makocha wa hapa awali walisema wamejiaanda vizuri na mwisho wa siku mmoja akapoteza na mwingine akaambulia sare hakuna cha ajabu.

Kila timu inatafuta matokeo na ile iliyojiaanda vema inaibuka na ushini na itasonga mbele kwa hali hiyo hata wawakilishi wetu bado nafasi ipo na Taifa linawategemea.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic