KIMATAIFA timu zetu zimeanza kwa kuwapa huzuni mashabiki hasa baada ya dakika tisini za awali kwenye michezo yao wakiwa nyumbani kwani wengi hawakutarajia iwe kama ilivyo kwa sasa.
Tumeona Yanga walianza kulazimisha sare mbele ya Zesco United wakiwa uwanja wa Taifa na nyomi la kutosha la mashabiki ambao walijitokeza kuwapa sapoti kimataifa hapo kuna tatizo kidogo la sio sana.
Wakaja ndugu zetu Azam FC nao kwenye hatua ya Kombe la Shirikisho wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani ambao wameuzoea wakaambulia kichapo cha bao 1-0 shida ipo ila sio sana.
Hapa tunaona kwamba licha ya mashabiki kuwa wengi uwanja wa Azam Complex na uwanja wa Taifa bado imekuwa ngumu kwa timu zetu zote mbili kuibuka na ushindi.
Inaleta picha kwamba michuano ambayo wanashiriki sio ya mchezomchezo bali ina ugumu na ili kupenya kwenye huu ugumu ni lazima timu zigangamale kwelikweli na sio kuzembea hata kidogo.
Timu zote zimeshindwa kwenda kama ambavyo wengi walikuwa wanatarajia kwani matumaini na matarajio ya wengi kwa timu hizo ilikuwa kuona zikifanya vizuri ukizingatia walikuwa nyumbani.
Matokeo ambayo wameyapata hayajawa ya kufurahisha machoni na maskioni mwa mashabiki jambo ambalo limewafanya wengi kubaki kimya wakiwa na maumivu yao.
Wapo ambao walishindwa kujizuia kwa kulia na kubaki wakilaumu huku wengine wakizimia baada ya mchezo kuisha ila mwisho wa siku maisha lazima yaendelee kwenye soka.
Kupoteza uwanja wa nyumbani kwa Azam FC kwenye michuano ya kimataifa kiukweli ni pigo kwa mashabiki na wafuatiliaji wa mpira ndani na nje ya Bongo.
Matokeo ambayo Yanga wameyapata ya kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 na Zesco nyumbani hayajawa na faida kwa Yanga kwa sasa ila ni muhimu kwa kile ambacho wamekivuna nyumbani.
Haikuwa sehemu ya mipango ya timu mwisho wa siku haya ni matokeo baada ya dakika tisini kukamilika ndani ya uwanja nyumbani na wanapaswa kupongezwa kwa kile ambacho wamekifanya mwanzo.
Kushindwa kupata matokeo chanya kwenye ardhi ya nyumbani kwa timu kupoteza ikiwa na lundo la mashabiki ni sehemu ya matokeo na mashabiki wanapaswa waelewe kwamba hakuna timu inayoingia uwanjani ikwa inapiga hesabu za kupoteza hilo halipo.
Yanga , Azam FC na Malindi wanapaswa pongezi kwa hatua ambayo wapo kwa sasa kimataifa kwani majukumu ambayo wachezaji wanayo kwa sasa ni makubwa na ni mazito kwelikweli.
Jambo kubwa na la pekee ambalo linapaswa likae vichwani mwa mashabiki kwamba mpira wa sasa umebadilika na umekuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kutafuta ushindi bila kujali inachezea wapi.
Kujitokeza kwa mashabiki kuzipa sapoti timu zao kiukweli kunaleta picha nzuri hasa kwa kuwa na mshikamano kwenye mechi zote za kimataifa zilizochezwa.
Sapoti ya mashabiki imekuwa ikionekana waziwazi kwa kila timu bila hili linapaswa liendelee kwenye mechi zote ambazo zitakuwa zinachezwa kwani mashabiki ni muhimu kwenye michezo.
Wao wanasimama wakiwa ni wachezaji wa akiba pia ni wachezaji wa ndani wakati huohuo wanakuwa makocha kwa kuwapa moyo wachezaji pale ambapo wanakuwa nje ya uwanja wakishangilia kwa nguvu mwanzo mwisho.
Hivyo ndivyo ambavyo inatakiwa kuwa kila siku hasa wakati wa mechi za kimataifa hatupaswi kufikiria uadui na kuleta utofauti wetu kwenye masuala ya kimataifa tutauchekesha ulimwengu.
Matokeo ambayo yametokea uwanjani ni ya kuyapokea kwa mashabiki wote na kukubali kwamba tumekosea na bado tuna nafasi nyingine ya kuweza kuyabadili.
Sapoti iendelee mwanzo mwisho kwani timu zetu sasa zinakwenda kurejeana na wapinzani wao na safari hii timu zetu zitakuwa ugenini.
Azam itafunga safari kwenda Zimbabwe na Yanga itafunga safari kwenda Zambia kwa wapinzani wao Zesco walio chini ya George Lwandamina.
Timu zote bado zina nafasi ya kusonga mbele endapo zitajiandaa vema na kufanyia kazi makosa ambayo yalitokea kwenye mchezo wa kwanza wakati wakiwa nyumbani na kushindwa kupata matokeo chanya.
Kila kitu kinawezekana kwenye michuano hii endapo timu zote zikaanza kufanya maandalizi mapema na kujipa muda wa kufanya vizuri na kupata mbinu za kupata ushindi.
Hatua hizi za mwanzo zina ugumu wake kwani ukiteleza kidogo mwenzako anatokea hapohapo na kusonga mbele kimataifa na kukuacha ukizubaa hujui cha kufanya.
Wawakilishi wetu kimataifa muda wao ni sasa kujipanga kupeperusha Bendera ya Taifa kwani hakuna tumaini jingine kwa timu kufanya vema zaidi ya hizi ambazo zimebaki.
Mashabiki wana imani na timu zao kimataifa na pia wanapenda kuona zinafanya vizuri sio kuishia hatua za awali itazidi kuwaumiza zaidi.
Madeni makubwa kwa mashabiki yapo kwa sasa kwa wachezaji na vitendo vinahitajika hasa uwanjani kwa kucheza kwa ushirikiano mkubwa hayo yatakuwa malipo ya deni lenu kwa mashabiki.
Tuliona namna ambavyo Yanga walikuwa wanachechemea hasa uwanja wa Taifa kwa kushindwa kufunguka kuna jambo la msingi kiufundi pale Jangwani inapaswa kufanyika ili kurejesha nafasi nne za kimataifa.
Benchi la ufundi lina kazi muda huu kuboresha mbinu za kikosi hasa kwa upande wa washambuliaji ambao wamekuwa wakibadilika mara kwa mara, tulitarajia kwenye mchezo wa nyumbani kuwe na washambuliaji zaidi ya wawili mbele mwisho wa siku mbinu ngumu zilitumika.
Kwa timu ambazo zinacheza nyumbani huwa zinakuwa hazina wasiwasi wachezaji huwa wancheza kwa kufunguka mwisho wa siku timu ilibana uwanja kuna jambo la kujifunza na kubadili mbinu.
Azam FC tatizo la kumiliki mpira na kuuchezea namna wanavyotaka hilo halipo ila wao wanakosa namna ya kumaliza hakuna ubunifu kwenye upande wa umaliziaji.
Washambuliaji wanaonekana wanatengemea mbinu ya mwalimu na pale inapofeli na akili zao zinagomea hapo hii ni mbaya na inapaswa ifanyiwe kazi.
Wachezaji pale ambapo mbinu ya mwalimu inagonga mwamba ni wakati wa kujiongeza na kufanya jambo la ziada kwa ajili ya kutafuta matokeo.
0 COMMENTS:
Post a Comment