MPIRA una matokeo ya kikatili ambayo yanapoteza furaha na kuacha ganzi kubwa ndani ya mioyo ya mashabiki, viongozi pamoja na wachezaji kwa kupata kile ambacho hawakukitaraji awali.
Tumeona namna ilivyokuwa ngumu kwa timu zetu kimataifa ambazo zimecheza michezo yake ya marudiano kwenye uwanja wa nyumbani kwa kushindwa kufurukuta licha ya sapoti kubwa na mashabiki wao pamoja na uzoefu wa matumizi ya uwanja wa nyumbani.
Timu ambazo zilikuwa zinapewa nafasi ya kusonga mbele kiulaini hasa baada ya kupata matokeo ambayo yalikuwa yanatoa matumaini kwamba uwezekano wa kusonga mbele ni mkubwa na upo mikononi mwao zimevurunda.
Simba na KMC kiukweli zimeacha mashabiki katika hali ambayo hawaamini kile ambacho wanakiona kutokana na kushindwa kutimiza yale matarajio ya wengi wakiwa uwanja wa nyumbani.
Kupoteza kwa KMC kwa kukubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya AS Kigali kulitoa imani kwa mashabiki kwamba kazi itamalizwa na Simba ambao wana uzoefu na michuano ya kimataifa na kuuwezea uwanja wa Taifa.
Mwisho wa siku nao wanapoteza kwa kukubali kufungana bao 1-1 na UD do Songo uwanja wa nyumbani wageni wanapita kwa faida ya bao la ugenini, inaumiza lakini ni lazima tujifunze kuyakubali matokeo.
Kwa kupoteza nafasi ya kusonga mbele kwa timu hizi mbili zikiwa nyumbani ni darasa tosha kwamba mpira unahitaji utulivu na umakini nje na ndani ya uwanja.
Timu zetu zilijisahau na kufikiri kwamba zimemaliza kazi mapema jambo ambalo limewapa wageni faida na kupata nafasi ya kusonga mbele hili ni darasa kwa timu zetu wakati ujao zifanye maandalizi vema.
Ukitazama kwa namna ambavyo KMC na Simba kwenye upande wa usajili namna ambavyo wameboresha vikosi vyao kwa kufanya sajili makini ambazo walitarajia zitawapa matokeo chanya na mwisho wa siku wamepotea haileti afya kwenye soka.
Haina maana kwamba hawajafanya jambo kubwa kwenye michuano ya kimataifa, hapana kisaikolojia wote kwa sasa wamepoteza ile imani na wamebaki na sononeko kubwa ndani ya moyo.
Achana na Yanga, Azam FC pamoja na Malindi hawa furaha yao ipo sawa na maisha kwao yanaendelea bila tatizo lolote isipokuwa kwa hawa ndugu zetu waliopoteza.
Rai yangu kwa sasa wanapaswa watulie waache dhana ya kuanza kufikiria kumtafuta mchawi ni nani aliyesababisha matokeo ya namna hii yatokee kwao tena kwenye uwanja wa nyumbani.
Wajipange kisaikolojia na kukubali kwamba haya ni matokeo ya mpira kama ambavyo wao waliweza kulazimisha sare ya kutofungwa wakiwa ugenini ndivyo ambavyo wageni wameweza kulazimisha kile ambacho walikuwa wakihitaji wakiwa ugenini pia.
Wasijivuruge kwa sasa na kuanza kunyooshena vidole eti kwa sababu wameshindwa kuvuka hatua inayofuata, huu ni mpira unadunda na matokeo yake yanakuwa kama ambavyo inatokea.
Ikitokea hivyo wakaruhusu kuanza kumtafuta nani ambaye amesababisha wakapoteza mchezo wao watapoteza kila kitu ambacho walikuwa nacho awali kwenye mikono yao.
Kwa Simba ambao ni mabingwa watetezi wakiruhusu mdudu huyo awatawale kichwani basi kuna uwezekano wakashindwa kufanya vema tena kwenye ligi na nafasi yao ya kulitetea taji la ubingwa itakuwa mashakani.
KMC nao uwezo wao walionao wakiruhusu mdudu huyo wa kumtafuta mchawi nani watapotezana kisaikolojia na wataikosa hata nafasi ya nne ambayo waliipata msimu uliopita ndani ya ligi ambayo imeshaanza kuwasha moto.
Azam FC, Yanga na Malindi ya visiwani Zanzibar kwa sasa zimeshikilia furaha za mashabiki zinapaswa zijifunze kupitia kwa ndugu zao ambao wameshindwa kufurukuta.
Kazi kubwa mikononi mwao ni kuona kwamba zinatinga hatua za mbali kwenye michuano hii ambapo msimu uliopita mafanikio ya Simba ambayo imetolewa kwenye michuano ya kimataifa ilikuwa ni chanzo kwao kushiriki.
Kazi yao kwa sasa itakuwa ni kufuta ile ganzi ya mashabiki wote kwa kupambana kupata matokeo chanya wakiwa ugenini na nyumbani bila kupuuzia wapinzani wao.
Makosa ambayo wameyafanya ndugu zao iwe ni darasa kwao kwa ajili ya kutafuta ushindi wasiyarudie na badala yake wayarekibishe na kuyafanyia kazi haraka.
Mpira kwa sasa umebadilika ile hofu ya kushindwa ugenini haipo tena na badala yake sayansi inatumika katika kila idara na timu iliyojiaandaa vema kisaikolojia na kiakili ina nafasi ya kushinda hasa ukizingatia kwamba mpira ni mbinu.
Wachezaji wajifunze kuwa na nidhamu kwa kila mchezo ambao watakuwa wanacheza bila kujali kwamba watakuwa nyumbani ama ugenini.
Mahabiki kukubali matokeo ya uwanjani na kuendelea kutoa sapoti kwa timu zetu kwani bado mashindano yanaendelea na wahenga wanasema kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi.
Maisha lazima yaendelee na mapambano bado hayajafika mwisho nafasi ya kujipanga kwa ajili ya wakati ujao ipo na inawezekana kurejea kwa nguvu mpya na kupata matokeo chanya kitataifa na kimataifa.
0 COMMENTS:
Post a Comment