October 27, 2019








 Na Saleh Ally
MECHI sita zilizopita za League One, PSG imeshinda tano na kupoteza moja tu, hali inayoifanya iongoze Ligi Kuu Ufaransa maarufu kama League 1 kwa tofauti ya pointi tano.

 Baada ya mechi 10, PSG ina pointi 24 kileleni ikifuatiwa na Nates yenye 19 halafu Reims inashika nafasi ya tatu ikiwa na 17, wapinzani wakubwa wa PSG, Marseille wao wa nne sawa na Angers wanaokamilisha tano bora.


PSG walimaliza utawala wa Marseille, Bordeaux, Lille na Montpellier ambao walikuwa wakichuana kila mara.
Kupunguza kasi kwa PSG kwa muda mrefu, kulifanya mambo yaende taratibu na kuonekana wababe ni walewale. Lakini kurejea kwao kumeifanya ligi hiyo ionekane kuwa ina mbabe mmoja.


League 1 ni moja ya ligi zenye mvuto sana, uchezaji wa timu nyingi za ligi hiyo ni ule utamaduni wa Kifaransa, soka lenye burudani zaidi.


Wachezaji wengi wa Kifaransa wana aina ya unyumbulifu. Burudani zaidi na unaona aina ya wachezaji wake wengi walio maarufu kama Zinedine Zidane aliyekulia Marseille na wengine, wana aina hiyo.


Kwa wale ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kuishuhudia ligi hiyo kupitia king’amuzi cha Startimes lazima watakuwa wanaijua burudani hiyo.


Startimes wamekuwa wakionyesha League 1 kwa upana zaidi kupitia chaneli zao za michezo na mechi mbalimbali zikiwemo za PSG inayoongozwa na Mbrazil Neymar ambaye amerejea kwa kasi kubwa.


Takwimu zinaonyesha kwa msimu wa 2019/20 kuna mabadiliko kidogo katika suala la utawala wa PSG ambayo mara nyingi katika mechi 10 inakuwa imeshinda zote na ikiwezekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya mabao.


Safari hii, tofauti ni pointi tano lakini kuna hofu kidogo kutokana na matokeo yake katika mechi zilizopita na namba ambavyo wamekuwa wakilazimika kujiokoa katika dakika za mwisho.



Ingawa wamekuwa na idadi tofauti kidogo ya ufungaji mabao, lakini bado ni watawala wa hilo hadi msimu huu lakini pengo la pointi si lakutisha kama ilivyokuwa katika misimu mitatu iliyopita.


PSG wamekuwa na hofu huenda Neymar akaondoka lakini pia inaonekana hata Kylian Mbappe anaweza kuona ni wakati mwafaka wa kuwaaga na kikosi chao kinaonekana kutokuwa na mwendo wa kutisha sana.


Neymar hajawa bora hivyo, ingawa alionyesha uhai akitokea kwenye majeruhi. Tayari amefunga mabao manne huku anayeongoza akiwa na mabao nane ambaye ni Wisam Ben Yedder.


Neymar ndio amecheza dakika 449. Anakimbizana na nyota mwingine Memphis Depay mwenye mabao manne pia lakini kacheza dakika 654, idadi hiyo ya mabao pia anayo Muargentina Angel Di Maria ambaye amepiga dakika 683.


Wachambuzi wa Gazeti namba moja la michezo la Le’equipe walichambua wakisema wanaona Neymar na Mbappe kama vijana wanaweza kuwa na hamu ya kwenda kujaribu sehemu nyingine.


Wanaamini wanaweza kufanya hivyo kwa kuwa hamu yao kubwa ni kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa na klabu hiyo, jambo ambalo tayari limeonekana ni gumu, hasa kwa msimu huu.


Hivyo haina ujanja, wawili hawa wana nafasi kubwa ya kuaga na huenda kutakuwa na kuyumba kwa PSG. Je, itakuwa faraja kwa wengine au PSG wataweza kuzuia hili?
Pamoja na yote, ligi hiyo bado ina mvuto sana.


Huenda timu zake zinaweza kuwa si maarufu sana kwa hapa nyumbani Tanzania. Lakini soka lao linavutia kutazama na kuna aina ya wachezaji wengi wamekwenda kuwa mastaa katika ligi nyingine kam Bundesliga, Serie A au Premier League lakini walitokea hapo League 1.


Startimes wao wamekuwa wakisisitiza kuwa wanautambua ubora wa League 1, ndiyo maana wamekuwa wakitaka Watanzania kupata burudani zaidi ya ligi hiyo kupitia king’amuzi chao chenye ubora wa juu hasa katika suala la muonekano.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic