October 23, 2019



NGOMA inayofukuta kwa sasa ni mchezo wa ligi kuu kati ya Azam FC na Simba unaotarajiwa kuchezwa leo Oktoba 23 uwanja wa Taifa utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa mafahali hawa wawili kukutana kwenye mchezo wa ligi.
Azam FC iliyo chini ya Arstica Cioba akisaidiana na Idd Cheche ina kazi kubwa ya kuipoteza safu ya ushambuliaji ya Simba yenye uchu wa mabao inayoongozwa na mnyarwanda Meddie Kagere.
Mpaka sasa timu zote mbili hakuna hata moja ambayo imepoteza huku Azam FC ikiwa imecheza mechi tatu sawa na dakika 270 na Simba imecheza jumla ya mechi nne sawa na dakika 360.
Kwenye mchezo huo ambao utakuwa ni wa kukata na shoka unatarajiwa kuteka hisia za wengi kutokana na rekodi tamu zilizowekwa na timu zote mbili cheki jinsi mambo yalivyo:-
Mifumo ya ushindi
Patrick Aussems Kocha Mkuu wa Simba alianza na mfumo wa 4-3-3 dhidi JKT Tanzania, akashinda 3-1.Mbele ya Mtibwa alikuwa na mfumo wa 4-4-2 alishinda 2-1 zote uwanja wa Uhuru.
Kagera Sugar, mfumo ulikuwa ni 4-4-2, akashinda 3-0 uwanja wa Kaitaba kisha  4-3-3 dhidi ya Biashara United, akashinda 2-0 uwanja wa Karume.
Ikiwa chini ya Etienne Ndayiragije, Kocha Mkuu wa Azam FC  ambaye kwa sasa amempa mikoba Cioaba yeye alianza na 4-3-3 dhidi ya KMC alishinda bao 1 uwanja wa Uhuru kisha mbele ya Namungo FC alitumia 4-4-2 alishinda mabao 2-1 kisha akafunga hesabu na Ndanda kwa 4-4-2 alishinda mabao 2-0.
Watupiaji nyavuni
Azam FC kwenye jumla ya mechi tatu walizocheza imefunga jumla ya mabao matano huku kinara akiwa ni Donald Ngoma ambaye ametupia jumla ya mabao mawili, Idd Suleiman ‘Naldo’, Frank Domayo na Daniel Amoah wakitupia mojamoja.
Kwa upande wa Simba kwenye michezo 4 wametupia jumla ya mabao 10 ambapo Meddie Kagere ametupia sita, Miraji Athuman ‘Sheva’ matatu na Mohamed Hussein ‘Tshabala’ moja.
Wakali wa asisti
Mpaka sasa ni Azam FC ndio ipo juu kwa kutengeneza asisiti mpishi wao mkubwa wa mabao ni beki Nicolaus Wadada ambaye ametoa tatu mpaka sasa kwenye mechi tatu, kwa upande wa Simba, Kagere, Mzamiru Yasin, Sharaf Shiboub wametoa asisti mbili huku Sheva na Ibrahim Ajibu wakitoa mojamoja.
Bao la mapema
Kagere anashikilia rekodi ya kuwa hatari zaidi kipindi cha kwanza ambapo mchezo wake wa kwanza dhidi ya JKT Tanzania alifunga bao dakika ya 1 akimalizia asisti ya Mzamiru Yassin huku kwa upande wa Azam FC, Naldo anashikilia rekodi ya kufunga bao la mapema kwa Azam mbele ya KMC alipachika bao dakika ya 14 akimalizia asisti ya Nicolous Wadada.
Wanaotegemewa Safu ya ulinzi
Azam FC imekuwa na ukuta usiobadilika ambapo kwenye mechi zote tatu Ndayiragije amekuwa akiwatumia Nicolaus Wadada,Daniel Amoah,Yakub Mohamed na Bruce Kangwa huku ile ya Simba ikibadilikabadilika  isipokuwa Mohamed Hussein ‘Tshabala’ amecheza mechi zote nne.
Watakaokosekana
Kwa upande wa Simba ni nahodha John Bocco ambaye ameanza mazoezi mepesi, Mohamed Hussein, Jonas Mkue huku nahodha wa Azam FC Agrey Moris akitegemea maamuzi ya mwalimu kutokana na kutoka kwenye majeruhi.
Vita ya kisasi
Azam FC itaingia uwanjani ikiwa na lengo la kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wao msimu uliopita wa 2018/19 kwa kufungwa mabao 3-1 uwanja wa Taifa uliowapotezea dira ya kutwaa taji la ligi na mwisho ukaotesha nyasi kibarua cha Kocha Mkuu, Hans Pluijm na Juma Mwambusi ambaye kwa sasa anainoa Mbeya City.
Hesabu za makocha hizi hapa
 Cheche kocha msaidizi wa Azam FC amesema kuwa hesabu zake kwa kila mchezo ni kupata pointi tatu muhimu katika kila mchezo.
“Tunakikosi kipana na cha gharama ukizingatia kwamba Azam FC ni timu kubwa nasi tutaonyesha ukubwa wetu kwenye mechi zetu zote,”.
Aussems amesema kuwa hesabu zake ni kuona anaendelea kupata ushindi bila kujali anacheza na timu ipi.
“Kila mechi nahesabia ni fainali, ninaona kwamba timu zte zimejipanga name pia nimewaambia wachezaji hesabu zetu ni ushindi hakuna jambo lingine,”.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic