October 27, 2019


INAELEZWA kuwa ule msikiti anaojenga mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, unatarajia kukamilika mwakani huku gharama zake zikiwa ni shilingi bilioni moja hapo hadi ukamilike.

Samatta anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, imepangwa kwenye Kundi E ikiwa na Liverpool ya Uingereza, Red Bull Salzburg ya Austria na Napoli ya Italia.

Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, akiwa mwenye rekodi kibao za kimataifa, anajenga msikiti huo katika eneo la Kidubwa, Vikindu mkoani Pwani.

Msikiti huo ambao una uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 600, kwa sasa umefikia katika hatua za mwisho kukamilika kabla ya kufunguliwa rasmi mwakani.


Championi Jumamosi juzi Alhamisi lilitembelea msikiti huo kwa mara ya tatu tangu uanze kujengwa Februari, mwaka jana na kukuta sehemu kubwa ya ujenzi ikiwa imekamilika kwa asilimia 80 na hadi uishe utakuwa umetumia bilioni moja na milioni kadhaa.

Championi limeshuhudia sehemu ya kuchukulia udhu wanaume ikiwa imekamilika kwa kuwekwa njia za maji ya kuchukulia udhu na vyoo tisa ambavyo vipo kwenye hatua ya mwisho sawa na upande wa kuchukulia udhu wanawake wenye vyoo sita vya uhakika na sehemu ya udhu.

Mbali na hilo, pia kuna chumba cha kuhifadhia na kuoshea maiti huko miundombinu yake imekamilika, kinachosubiriwa ni hatua za mwisho pamoja na ofisi ya Imam (viongozi wa msikiti).


Tayari msikiti huo umeshawekwa madirisha makubwa ya ‘grili’ huku ukiwa umeshapigwa plasta wote pamoja na sakafu ya zege katika sehemu kubwa ya msikiti, mbali ya hivyo tayari umeshafungwa wiring ikiwa na swichi kubwa ya umeme.

Katika ziara hiyo ya Gazeti la championi kwenye msikiti huo wa kisasa, lilikuwa limeambatana na baba mzazi wa nyota huyo, mzee ally Samatta ambaye alihusika katika kutoa maelekezo ya ujenzi wa msikiti huo hadi ulipofikia kwa sasa.

“Nadhani wenyewe mnaona ujenzi unaendelea vizuri umefikia katika hatua kubwa sana na jambo zuri watu wa maeneo haya wameanza kuutumia kufanyia ibada hasa kwenye sala za jioni licha ya kutokamilika. Ujenzi unaonekana kuchelewa, tatizo nini?

“Unajua kwanza ujenzi wa msikiti huu ulianza Februari mwaka jana na mwenyewe alitegemea ukamilike ndani ya mwaka huu lakini kuna mambo yamekwamisha ndiyo maana unaona umechelewa.

“Lakini kwa hatua ulipofikia utakamilika japo utachelewa kidogo kulingana na mipango ya mtoa pesa kwa kuwa unaweza kupanga ufanye hivi lakini mambo yakawa tofauti. Nini kinachokwamisha?

“Changamoto kwa sasa imekuwa ni pesa kwa kuwa alitegemea kama angefanikiwa wakati ule wa dirisha la usajili la Ulaya kuondoka Genk basi sasa hivi nadhani kila kitu kingekuwa tayari.

“Mipango yake ilikuwa inategemea usajili wa klabu za Uingereza kama Leicester City, West Ham na Aston Villa lakini kwa bahati mbaya haikuweza kufanikiwa kwa wakati ndiyo maana ujenzi unaona unakwenda kidogo kidogo.

“Lakini kama mipango ingeweza kumuendea vizuri kwa maana ya kusajiliwa basi msikiti sasa hivi angekuwa ameshaukabidhi kwa waumini ili waweze kutumia kwa ajili ya ibada. hadi ukamilike utagharimu kiasi gani?

“Kiukweli itakuwa ni pesa nyingi, inafika bilioni moja na itazidi pengine milioni 200 au 300 kwa sababu utakuwa wa kisasa ambao una vitu vya kisasa. “Mwenyewe alinieleza mbali ya kupiga tiles ‘vigae vya chini’ lakini anataka kuweka mazuria yale ambayo yanawekwa kwenye misikiti mikubwa ya nchi za Kiarabu na yanauzwa kwa bei kubwa,” alisema mzee Samatta.

1 COMMENTS:

  1. Mashallah!!M/Mungu akuzidishie pale palipopungua Captain Diego

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic