BUZINZA Y'ENGOZI WALIVYOKONGA MIOYO TAMASHA LA JAMA FEST DAR
Na George Mganga
ILICHUKUA muda wa siku nane kuanzia Septemba 21 mpaka 28 kwa tamasha kubwa la JAMA FEST kufanyika Tanzania katika jiji la Dar es Salaam na ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.
JAMA FEST ni tamasha ambalo linahusika na kuonyesha tamaduni asilia za Afrika ikiwemo mapishi, mavazi, malazi na asili ya vitu vinavyofanyika ndani ya nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla.
Tamasha hilo linahusisha jumla ya nchi sita zilizo ukanda wa Afrika Mashariki ambazo mbali na Tanzania, nyingine ni Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi.
Katika tamasha hilo lililofana kutokana na kuhudhuriwa na watu mbalimbali ikiwemo Makamu wa Rais katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samiah Suluh Hassan pamoja na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dr. Harrison Mwakyembe, lilihusisha vikundi mbalimbali kutoka Tanzania na nje ya Tanzania.
Moja ya makundi yaliyowakilisha kutoka Tanzania ni BUZINZA YE NGOZI OBUHOLO NEMILEMBE linalotokea Buchosa, Mwanza, ambalo lilikuwa chini ya Injinia Godfrey Thomas Nkombolwa aliyeratibu shughuli nzima za kundi hilo.
SALEH JEMBE na Injia Nkombolwa ambaye alifunguka mengi zaidi juu ya namna kundi la BUZINZA YE NGOZI OBUHOLO NEMILEMBE lilivyohusika ndani ya tamasha hilo.
NINI MAANA YA JINA LA KUNDI LENU?
"BUZINZA YE NGOZI OBUHOLO NIMELEMBE maana yake ni upendo na amani kwa Kiswahili, hii ni lugha ya Kizinza ambayo asili yake ni kutoka Buchosa katika wilaya ya Sengerema, Mwanza.
"Tuliamua kulitunga jina hili kwa lengo maalum la kuonyesha ushirikiano na mshikamano kama kundi na kwa wanajamii wanaotuzunguka kwa ujumla, na kundi letu lina jumla ya watu 33 pamoja viongozi.
AINA GANI YA MICHEZO MLIIONYESHA JAMA FEST?
"Kundi letu lilitumbuiza kwa kuonesha aina ya michezo miwili tuliyonayo sisi, ambayo ni MLEKULE na BUCHWEZI, michezo iliyokuwa inaonesha asili ya namna mababu zetu walivyokuwa wakicheza enzi hizo.
"MLEKULE ni aina ya mchezo wa kucheza mwili mzima, hii si kwamba unacheza kiuno pekee bali mwili mzima kwa maana ya viungo vyote vya mwili, mchezo huu ulikuwa unafanyika zaidi kipindi cha sherehe mbalimbali.
"BUCHWEZI huu ni mchezo wa ngoma uliokuwa unafanyika katika kipindi cha matambiko, ni ngoma iliyokuwa mahususi kuchezwa haswa pale mtu anapopatikana baada ya kupotea kwa muda mrefu au mfupi, siku akipatikana inatumika kumtambikia.
AINA YENU ZA MICHEZO ILIPOKELEWAJE NA WATAZAMAJI?
"Ilipokelewa vizuri kutoka na asili ya burudani ambayo ilikuwa inatolewa na kundi letu mpaka ilifikia hatua ya watazamaji wengi waliokuwepo pale kuomba irudiwe mara kwa mara kutokana na namna tulivyokuwa tunaimba.
CHANGAMOTO GANI MLIKUTANA NAZO WAKATI WA MAANDALIZI?
"Kiukweli katika suala hilo shida kubwa kwa sisi hapa Tanzania hatuna wawezeshaji kwa maana ya wadhamini, ukiangalia wenzetu serikali yao ilikuwa vizuri katika kuwasaidia, sisi bado tupo nyuma na hili tunaiomba serikali iweke mkono wake maana gharama nyingi unakuta tunawafanya watu binafsi.
UNAZUNGUMZIAJE WASANII WENGI WA SASA KUJITENGA NA MAMBO YA KIASILI?
"Nadhani kuna wakati ifikie hatua serikali iweze kutia morali juu ya tamaduni zetu, hili suala linaanzia kwa wazazi, wao wanapaswa kuwafundisha tangu wakiwa wadogo kwani zinaonesha uasili wetu na kuna fursa nyingi huku tofauti na mziki wa kizazi kipya watu wengi wamejaa.
KIPI MLIJIFUNZA KATIKA TAMASHA?
"Ni tamasha zuri ambalo vikundi tofautitofauti vilionesha kile walichokuwa nacho, tuliona namna ambavyo wenzetu walikuwa wamejipanga nasi kama BUZINZA YE NGOZI OBUHOLO NIMELEMBE tuliweza kuvichukua vizuri tulivyoviona na tutavifanyia kazi.
UNA USHAURI GANI KWA SERIKALI JUU YA KUTOA SAPOTI KWENYE MATAMASHA YA KITAMADUNI?
"Naiomba serikali ijaribu kuangalia na sekta yetu ya utamaduni kwani imesahaulika, nguvu wanayoitumia katika kusaidia mpira wa miguu nchini basi wailete na kwetu sababu ni wamoja.
"Najua serikali ina mambo mengi lakini naamini inaweza kutusaidia, ukiangalia katika kundi letu gharama zilikuwa juu yetu, mpaka tulipopiga kelee tulipata msaada wa Magufuli Hostel ambapo tuliweka kambi yetu wakati tukiwa Dar.
MNA MPANGO WA KUJIWEKA KARIBU NA WADAU WENU KUPITIA MTANDAO?
"Hivi sasa tupo kwenye mchakato wa kukamilisha website yetu pamoja na kufungua kurasa za mitandao ya kijamii, tunafanya hivi ili kujiweka karibu zaidi na wadau hata mashabiki zetu ili waweze kutufuatilia.
"Mpaka sasa tumeshafungua chaneli YouTube ambayo inajulikana kwa jina la MLEKULE, watu wanaweza kututafuta huko na kuweza kutazama kazi zetu.
NINI KINAFUATA BAADA YA JAMA FEST?
"Kwanza naweza kusema JAMA FEST imetusaidia kwasababu imetuwezesha kupata matamasha mengine ya kufanya kama Urithi Festival ambalo litafanyika Mwanza mwezi Novemba pamoja na Jubilee ya miaka 60 ya Hospitali ya Sengerema na mengine ambayo tutayataja wakati ukifika.
0 COMMENTS:
Post a Comment