Mshambuliaji wa Simba, Miraji Athuman’ Sheva’, jana amezua balaa katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam.
Katika mazoezi hayo Sheva alionyesha kuwa kile ambacho amekuwa akikifanya katika mechi ambazo mpaka sasa ameshaitumikia timu hiyo ni jambo la kawaida kwake baada ya kumtungua mabao sita kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula.
Jambo hilo lilionekana kumpagawisha vilivyo kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems na kujikuta akimpigia makofi kila alipokuwa akifunga.
Hata hivyo, baada ya mazoezi hayo Championi Ijumaa lilizungumza na Sheva na alisema kuwa kiwango chake kwa sasa kipo juu tangu ajiunge na Simba na kama mambo yatakuwa sawa amejipanga kufunga mabao 15 msimu huu.
Sheva ambaye tangu ajiunge na Simba msimu huu akitokea Lipuli FC alisema endapo atafanikiwa kufikisha idadi hiyo ya mabao itakuwa ni rekodi mpya kwake. Alisema tangu alipoanza kucheza soka la ushindani msimu wa 2014/15 hajawahi kufikisha idadi hiyo ya mabao.
“Tangu kipindi hicho nilichoanza kucheza soka la ushindani nimefanikiwa kufunga jumla ya mabao 23 katika Ligi Kuu Bara.
“Baada ya kutoka Simba B, nilienda Mwadui na hapo nilifunga mabao matatu, kisha nikaenda Toto Africans ambapo nilifunga mabao saba.
“Baadaye nilirudi Mwadui nikafunga mabao matatu kisha msimu uliopita nikiwa Lipuli nilifunga mabao saba na kutoa asisti sita.
“Kwa hiyo ukijumlisha na mabao yangu matatu ya sasa niliyofunga nikiwa na Simba jumla nimefunga mabao 23.
“Hata hivyo, lengo langu msimu huu ni kufikisha mabao 15 Mungu akipenda,” alisema Sheva.
KAULI YA AUSSEMS
Kocha mkuu wa Simba, Aussems alisema: “Amekuwa akifanya vizuri mazoezini lakini pia kwenye mechi na kila siku uwezo wake umekuwa ukiongezeka.
“Najivunia kuwa naye katika kikosi changu na ni matumaini yangu kuwa ataendelea kuwa bora zaidi kwa sababu ni mtu anayejituma na anayetaka kujifunza.”
Katika mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Simba ilicheza dhidi ya UD Songo ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Sheva ndiye aliyesababisha penalti iliyoipatia Simba bao la kusawazisha.
AMFUNGUKIA KAGERE
Kuhusu siri ya mafanikio yake, Sheva alisema: “Nimekuwa nikijifunza mambo mengi kutoka kwa Kagere, ananipa mbinu na kunifanya nijiamini sana ninapokuwa uwanjani.”
Miraji ni miongoni mwa kijana ambae atawashangaza wengi lakuomba Mungu amjalie afya endelevu. Fowadi zetu nyingi za kitanzania huwa zinakimbia mabeki lakini tofauti ya Miraji ni ile hali ya kujiamini mbele ya beki na ndio kitu kinachomtofautisha na wachezaji wetu wengi wa sasa.
ReplyDeleteNi sahihi kabisa. Ni kijana anayejiamini na analijua goli. Keep it Sheva. Sky is the limit for Sheva.
ReplyDelete