October 6, 2019


SAFU ya ushambuliaji ya kikosi cha Simba inazidi kunoga kwa sasa ikiwa ni kikosi kipya na kimeanza kuunda utatu wenye moto ndani ya Ligi Kuu Bara.

Utatu huo unaongozwa na Miraj Athuman ‘Sheva’, Meddie Kagere na Ibrahim Ajibu ambapo kwa kifupi unaitwa A.K.A.

Mpaka sasa kwenye utatu huo, Kagere ndiye baba lao kwani amecheza mechi zote nne akitumia dakika 357 kwa kuwa alifanyiwa mabadiliko kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar. Katika dakika hizo, amefunga mabao sita na kutoa asisti mbili.

Mechi zote za ligi kuu ambazo Simba imecheza mpaka sasa, Kagere amekuwa mchezaji wa kwanza kufungua ukurasa wa mabao akianzia katika ushindi wa 3-1 dhidi ya JKT Tanzania akifunga mabao mawili na kutoa asisti moja kwa Sheva.

Pia mbele ya Mtibwa Sugar, alifunga bao moja, haikuishia hapo, alifunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar na kutoa asisti kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, akamaliza hesabu mbele ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 2-0. Yeye akifunga moja.

Ajibu anazidi kuonesha kwamba amerejea nyumbani akitokea Yanga ambako huko alitoa asisti 17 msimu uliopita na kuzidisha ule udambwiudambwi kwani kwenye mechi tatu alizocheza kwa dakika 161, amedhihihirisha kwamba yeye habahatishi kwani tayari ametoa asisti moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Biashara United, bao likafungwa kwa kichwa na Miraj huku akipiga mpira safi.

Miraj yeye ni ‘super sub’ ndani ya Simba kwa sasa, akiwa amecheza jumla ya dakika 87 katika michezo mitatu akitokea benchi, huku mchezo mmoja alioanza akitumia dakika 83. Kwa jumla ya dakika 170 alizotumia kwenye michezo minne, Miraj amefunga jumla ya mabao matatu.

Alianza kufunga kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1, akafunga mbele ya Mtibwa Sugar na dhidi ya Biashara United, huku akitoa asisti moja kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Karume.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic