IKIWA chini
ya Felix Minziro, Singida United ilipanda daraja msimu wa mwaka 2017/18
mabadiliko yakafanyika mikoba ya Minziro akapewa Mholanzi, Hans Pluijm ambaye
aliwasha moto mwanzo mwisho.
Singida
United kwenye mechi 30 sawa dakika 2,700
ilishinda mechi 11, sare
mechi 11 na kuambulia kichapo mechi 8.
Ilimaliza
ikiwa nafasi ya tano baada ya kujikusanyia pointi 44 ila katika dakika 720 za kichapo
ilitumia dakika 180 sawa na mechi mbili kupoteza mbele ya Simba ilifungwa nje
ndani.
Msimu wa
2018/19 mambo yalizidi kupamba moto ambapo timu ziliongezwa na bodi ya ligi zikawa
38 ilifungwa nje ndani na Simba.
Ilimaliza
ligi nafasi ya 13 kibindoni na pointi 46 ndani ya dakika 1,260 za kupoteza
ilitumia dakika 180 sawa na mechi mbili kufungwa na Simba nje ndani hivyo leo
kazi itakuwa ngumu kwa timu zote kuhaha kuweka rekodi zao mpya.
Uwanja wa Amri Abeid Arusha moto utawaka na wajanja wa mjini wanasema ugali moto na mboga ni moto kwa
Singida United kutokana na haya hapa:-
Nafasi ndani ya ligi
Singida
United iliyo chini ya Ramadhan Nswanzurimo ambaye amepewa kandarasi ya mwaka
mmoja kwa sasa inahaha kurejea kwenye ubora wake kutokana na kutokuwa na
matokeo chanya ndani ya ligi.
Kwenye mechi
7 sawa na dakika 630 ambazo imecheza msimu huu haitambui ladha ya ushindi zaidi
ya kuambulia sare tatu na imepoteza mechi nne ipo nafasi ya 20.
Simba presha
yake kubwa ni kuendelea wimbi la ushindi kwenye mchezo wake wa sita baada ya
kuvuna jumla ya pointi 15 ikiwa nafasi ya kwanza kwenye mechi tano ambazo
wamecheza.
Vita ya kiatu cha ufungaji
Kwa Singida
United mambo bado mambo hayajawa sawa kwenye
mechi 7 mpaka sasa wamefunga mabao mawili la kwanza lilifungwa na Frank Zakari
kwenye sare ya bao 1-1 na Ndanda FC huku la pili likifungwa na Stephen Opoku
kwenye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.
Simba
wamecheza mechi tano kasi ya mfungaji bora wa msimu uliopita Meddie Kagere aliyefunga
mabao 23 imepamba moto akiwa ametupia mabao 7, Miraj Athuman matatu na Mohamed
Hussein bao moja na kufanya wafunge jumla ya mabao 11 jambo linaloongeza ugumu
wa mechi.
Rekodi ya kutofungwa na kufungwa
Hesabu za
Singida United ni kuvunja uteja mbele ya Simba kwa kufungwa nje ndani kwa
misimu miwili mfululizo baada ya kupanda daraja mwaka 2017/18, huku Simba wao
wakiwaza kuendeleza rekodi yao.
Mchezo wa
kwanza uliochezwa uwanja wa Uhuru Singida United ilikubali kichapo cha mabao 4-0
na ule wa raundi ya pili ikafungwa bao 1-0 uwanja wa Namfua. Msimu wa 2018/19
ilifungwa mabao 3-0 uwanja wa Taifa na ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 uwanja
wa Namfua hivyo leo kazi ni kupindua meza.
Kasi ya ubingwa kuongezwa na
kupunguzwa
Singida United
inautazama mchezo wa leo kuwa gia ya kuipunguzia kasi Simba kutetea ubingwa
wake kwani mpaka sasa kwenye mechi tano sawa na dakika 450 haijaambulia kichapo
jambo linaloongeza ugumu kwa timu zote leo uwanja wa Amri Abeid, Arusha.
Vita ya mbinu za Mrundi na Mbelgiji
Kwenye
benchi la ufundi la Singida United atasimama Ramadhan Nswanzurimo ambaye
anautambua upepo wa ligi ya Bongo kwani aliwahi kuifundisha Mbeya City msimu wa
2018/19 alikutana na Mbelgiji uwanja wa Taifa na alipoteza kwa kufungwa mabao
2-0 hivyo wote wanatambuana mbinu zao kazi itaonyeshwa leo.
Maneno ya makocha haya hapa
Ramadhan
Nswanzurimo, wa Singida United alisema kuwa anatambua mchezo utakuwa mgumu ila
anaamini watashinda kutokana na morali ya wachezaji.
“Kila
mchezaji anatambua hali ilivyo kwenye kikosi, hatujapata ushindi itakuwa vizuri
tukishinda mchezo wetu wa kwanza kuongeza hali ya kujiamini,”.
Patrick
Aussems alisema kuwa:” Haijalishi tunacheza na timu gani, kila mwalimu hesabu
zake ni pointi tatu hayo ndio malengo ya timu pamoja na benchi la ufundi,
tunatambua utakuwa mchezo mgumu tutapambana,”.
Simba itawakosa manahidha wake wote wawili ambao ni John Bocco na Mohamed Hussein wanaosumbuliwa na majeruhi.
0 COMMENTS:
Post a Comment