YANGA WAMLETEA UBISHI MO
Yanga ni kama wanamletea ubishi mwekezaji wa Simba, bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’, hiyo ni baada ya kutangaza miezi minne sawa na siku 120 za kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Kaunda uliopo kwenye makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Jangwani, Dar.
Hatua hiyo imekuja siku chache tangu Mo atembelee Uwanja wa Bunju unaomilikiwa na Simba ambao upo kwenye hatua za mwisho za kukamilika hasa ule wa mazoezi upande wa nyasi bandia. Mara baada ya Mo kutembelea uwanja huo aliahidi kumalizika kwa uwanja huo hivi karibuni kutokana na nyasi bandia kutua nchini na kupelekwa uwanjani hapo tayari kwa kuwekwa.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema kuwa hadi kufikia Februari 2020 ukarabati wa uwanja huo utakuwa umekamilika.
Mwakalebela alisema kuwa uwanja wamepanga kuutumia kwa ajili ya mazoezi, pia kambi ya pamoja ya kikosi chao katika kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu Bara na kimataifa.
Aliongeza kuwa hivi karibuni wanatarajia kuanza ukarabati wa jengo lao hilo zikiwemo hosteli za wachezaji zitakazotumika mara baada ya timu hiyo kuingia kambini na tayari Kampuni ya GSM ambao ndiyo waliojitolea ukarabati wa jingo, wameanza taratibu za awali.
“Zoezi lililopo hivi sasa katika ukarabati wa uwanja wetu wa Kaunda ni kujaza kifusi limekamilika ambalo limekamilika, kazi inayofanyika sasa ni usambazaji wa kifusi hicho tayari.
“Tayari yapo magreda mawili yanaendelea na kazi hiyo ya kusambaza na kusawazisha vifusi na baada ya kusawazisha udongo huo, zoezi litakalofuata ni kuweka udongo mwingine ambao ni wa rutuba kisha upandaji wa nyasi utafuatia.
“Kikubwa tunataka kabla ya mzunguko wa pili wa ligi kuanza tuwe tayari tumeanza kuutumia uwanja wetu, pamoja na kambi ya hapo kwenye hosteli zetu chini ya udhamini wa GSM waliochukua jukumu la kuukarabati uwanja huo,” alisema Mwakalebela.
Yanga hivi sasa inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam huku ikiweka kambi yake Nafeland Hotel, Magomeni Kagera, Dar.
0 COMMENTS:
Post a Comment