KABURI LA BONGO FLEVA LACHIMBWA
MUZIKI wa Nigeria umesambaa kwa kiasi kikubwa barani Afrika, Ulaya, Amerika na kwingineko. Hilo halina ubishi na ndiyo maana staa wa RnB wa Marekani, Beyonce Knowles hakupata shida kutafuta wasanii watakaojaza albam yake mpya ya The Lion King: The Gift kutoka Nigeria.
Kila mwaka muziki wao unakua huku wasanii wapya wakizaliwa na kubamba vilivyo. Lakini kwenye muziki huo bifu za wao kwa wao zipo na kwa asilimia kubwa zinakuwa kwenye muziki na zinaisha kwenye muziki.
Tumeshuhudia bifu kati ya Davido, Tekno na Wizkid ambalo lilikuwa la kibiashara na mwisho walilimaliza na kupanda jukwaa moja kufanya shoo.
Nchini Afrika Kusini napo kulikuwa na bifu kati ya rapa Cassper Nyovest na AKA ambalo lilikwenda mbali zaidi hadi kuandikiana mashairi ya kuudhi na kudhalilishana, lakini mwisho walikaa pamoja na kuyamaliza na sasa muziki wao wa Hip Hop unaendelea kupewa heshima.
Kibongobongo, kumekuwa kukizuka bifu za hapa na pale za wasanii ambapo nyingine zinakuzwa na mashabiki japokuwa wahusika wenyewe wanaendelea kukaa kimya na kuzifanya ziendelee kukua.
Chanzo hasa cha bifu hizi kwa asilimia kubwa zinaonekana kubebwa na wivu wa mafanikio na chuki kutoka kwa msanii mmoja kwenda mwingine.
Endapo bifu na chuki hizi zikiendelea, kuna shaka ya kuupeleka kaburini muziki huu unaowapa watu ajira kwani kaburi limeshaanza kuchimbwa taratibu.
Over Ze Weekend limekuandalia baadhi ya bifu kati ya wasanii wenyewe kwa wenyewe huku nyingi zikionekana kukolezwa zaidi na mashabiki.
HAMISA VS NANDY
Wawili hawa wanadaiwa kuingia kwenye bifu lililozaa ‘kublokiana’ kwenye mitandao ya kijamii.
Chanzo hasa cha bifu lao inaelezwa ni picha aliyowahi kupiga Nandy akiwa na Diamond au Mondi wakati huohuo, Hamisa akiwa katika uhusiano na staa huyo.
Licha ya kufanya wote filamu na muziki wa Bongo Fleva, wawili hao wamekuwa wakikwepana kila wanapokutana.
MONDI VS KIBA
Bifu la wawili hawa lilianza kama utani baada ya kusemekana Mondi ndiye aliyemkera mwenzake baada ya kumfuta kwenye Wimbo wa Lala Salama.
Yapo mengi yanayozungumzwa juu ya bifu hili lililodumu kwa zaidi ya miaka sita sasa. Bifu hili limefikia hatua ya mashabiki kutengeneza team za kushambuliana.
Sasa bifu hili limekwenda mbali zaidi baada ya Mondi kutangaza kumualika Kiba kwenye tamasha lake la Wasafi litakalofanyika jijini Dar, mapema mwezi huu.
Kiba kupitia ukurasa wake wa Instagram alionesha kupaniki kwa taarifa hizo na kuandika ‘waraka’ unaoonesha kuna kitu kikubwa nyuma yao ambacho wengi hawakijui.
HARMO VS WCB
Kwa sasa Harmonize au Harmo ameanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide (KMW) baada ya kujitoa lebo iliyomlea ya Wasafi Classic Baby (WCB).
Tangu kujitoa katika lebo hiyo, Harmo amekuwa hapewi sapoti yoyote kutoka WCB nikimaanisha kwa memba waliopo ndani ya lebo hiyo kama ilivyokuwa zamani.
Kwa sasa Harmo ameachia Wimbo wa Uno ambapo hakuna sapoti yoyote kutoka WCB tangu aachie.
RUBY VS NANDY
Hawa wana upinzani wa hali ya juu, hasa kwa aina ya muziki wao huku mashabiki wao wakiwa na mitazamo tofauti kuhusu wasanii hawa.
Wote kwa vipindi tofauti hawasemi kuwa wana bifu, lakini uhalisia wa mambo unaonesha wana bifu la kimuziki.
Wengine wanasema Ruby ana vocal nzuri na ana uwezo mkubwa, lakini wakati huohuo wengine wakimsifu Nandy kwa mpangilio wa ngoma zake.
Wawili hawa licha ya kutokea Jumba la Kuibua Vipaji (THT) hawajawahi kupikika chungu kimoja, si kwenye kuachia ngoma au kukutana au kusikia mmoja akimuongelea positive mwenzake.
Kuonesha hawapo sawa, miezi michache iliyopita Nandy alikuwa na tamasha lake alilozunguka baadhi ya mikoa ambapo aliwakusanya wasanii wengi wa kike na kiume Bongo huku Ruby akiwekwa pembeni.
NAY VS MONDI
Unakumbuka mwaka 2013 kipindi hicho Nay wa Mitego akiwa amemshirikisha Mondi kwenye ngoma yake ya Muziki Gani? Ni miongoni mwa ngoma zilizoteka hisia za mashabiki wengi.
Mwaka 2015, wawili hawa waliachia tena ngoma nyingine ya Mapenzi au Pesa nayo ikatikisa vilivyo na baada ya hapo haikueleweka nini kimetokea zaidi ya kila mmoja kufanya kazi kivyake.
Wakali hawa hadi leo hawajawahi kuonekana pamoja si jukwaani au kuachia ngoma kama ilivyokuwa zamani huku Nay akiendeleza kumchana kupitia ngoma zake.
BARAKAH VS KIBA
Barakah The Prince alikuwa msanii wa pili kusainiwa chini ya Lebo ya Rockstar4000 (Africa) baada ya mkongwe Lady Jaydee.
Katika lebo hiyo ambayo Kiba alikuwa miongoni mwa wasimamizi wakuu, Barakah alifanya ngoma moja na Kiba (Nisamehe) na baada ya hapo alijitoa na kuongea maneno yaliyosababisha kuibuka kwa bifu zito kati yao.
Kwa sasa Barakah anajisimamia katika lebo yake ya Bana Music huku akiwa bado hayupo sawa na Kiba.
KINGS MUSIC VS WCB
Kings Music ni lebo inayomilikiwa na Kiba wakati WCB ikimilikiwa na Mondi. Huenda bifu la Kiba na Mondi likawa limeathiri kwa kiasi kikubwa lebo zao kutokana na wasanii hao kutokuwa na umoja. Ni vigumu kuona Kings Music wakishirikiana na WCB.
Si kwa hilo tu, hata kwenye matamasha ya Wasafi haijawahi kutokea Kings Music wakapata mualiko wa kupafomu.
HARMO VS MONDI
Wengi wanaofuatilia burudani wanajua fika Mondi ndiye aliyemshika mkono Harmo na kumtoa kimuziki. Harmo ndiye alikuwa msanii wa kwanza katika Lebo ya WCB na pia wa kwanza kupelekwa nje ya nchi kutengenezewa video kali chini ya Director Godfather anayekimbiza Afrika.
Harmo huyuhuyu ndiye alikuwa wa kwanza kupewa koneksheni za kimataifa na Mondi ambapo hadi sasa ameshafanya kolabo za kutosha na mastaa Afrika kama Burna Boy, Phyno, Korede Bello, Yemi Alade, Eddy Kenzo na wengine wengi.
Tangu amejitoa kwenye lebo hiyo, wawili hawa hawaivi tena kuiva chungu kimoja.
HITIMISHO
Kama hali ikiendelea hivi na chuki kukua kila kukicha ni dhahiri kwamba kaburi la Bongo Fleva linakuja kama ilivyokuwa kwa Dansi, Taarab na Bongo Movie.
0 COMMENTS:
Post a Comment