Na Saleh Ally, Sousse, Tunisia
Kikosi cha Taifa Stars chini ya Kocha Etienne Ndayiragije kimefanya maandalizi yake ya mwisho leo mjini Sousse hapa nchini Tunisia, tayari kuwavaa Libya.
Stars imefanya mazoezi kwenye uwanja utakaochezewa mechi dhidi ya Libya nje kidogo ya Sousse ikiwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon, kesho.
Libya wanalazimika kucheza katika uwanja huru kutokana na hofu ya usalama kwao ambako ni jirani kabisa na hapa Tunisia.
Kocha Mkuu Ndayiragije, amesema kikosi chake kina hali nzuri na kimejiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo.
“Tuko vizuri kabisa tayari kwa mchezo, Libya si timu tunayoifahamu sana lakini tumefanya maandalizi mazuri na tuko tayari kwa mchezo,” alisema Kocha huyo raia wa Burundi.
Ndayiragije ambaye anasaidiwa na Selemani Matola amesema maandalizi ya kikosi hicho ni ya uhakika na wanachosubiri ni mapambano.
Mji wa Sousse ni kati ya miji maarufu ya utalii barani Afrika na unaongoza kwa kuzungukwa na mahoteli ya kisasa nchini hapa kwa ajili ya watalii.
Libya tayari wako hapa na wamekuwa wakiufanya mji huu kama nyumbani kwao.
Tayari Stars imecheza mchezo mmoja wa michuano hiyo na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Equatorial Guinea.
0 COMMENTS:
Post a Comment