November 16, 2019


JUMLA ya CV 40 za makocha zimetua Jangwani wakitaka kumrithi Mkongomani Mwinyi Zahera kuwa kocha mkuu wa Yanga, lakini kati ya hao, wapo ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo.

Awali, makocha waliokuwa wanatajwa kurithi nafasi hiyo ni Mserbia Kostadin Papic na Waholanzi wawili ambao ni Ernie Brandts na Hans Pluijm ambao wote waliwahi kukinoa kikosi hicho kwenye misimu tofauti lakini sasa habari ni tofauti.

Yanga hivi karibuni ilitangaza nafasi ya kazi hiyo ikiwa ni siku chache mara baada ya Charles Boniface Mkwasa kukaimu kwa muda wakati mabosi wakiendelea kumtafuta kocha mkuu ambapo jina la kocha aliyewahi kuinoa Zamalek ya Misri nalo lipo.

Mbali na kocha huyo, taarifa za uhakika kutoka Yanga ni kuwa jina la kocha Lodewjik de Kruif raia wa Uholanzi aliyezaliwa Oktoba 7, 1969 ndilo linapewa nafasi ya kukinoa kikosi hicho kama kocha mkuu.

Mtoa taarifa amesema kama mazungumzo yakienda vizuri, basi kocha huyo huenda akatua kuifundisha Yanga hivi karibuni pamoja na msaidizi wake ambaye ni raia wa Nigeria.

“Bado uongozi unaendelea kupitia CV za makocha mbalimbali, wapo makocha wakuu na wasaidizi wote kutoka nje ya nchi kwa hapa (Tanzania) hakuna aliyeleta CV yake, hatujajua sababu.

“Uongozi unavutiwa zaidi na kocha huyo Mholanzi wakiamini ana rekodi nzuri, pia elimu nzuri ya UEFA A-Licence ambayo inamtosha kuifundisha Yanga,” alisema mtoa taarifa.

Kocha huyo aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Bangladesh, Heartland FC, Ajax/Almere City FC U19, N.E.C. Nijmegen U19 – U17, FC Kleve, Beerschot Antwerpen na Beerschot Antwerpen U18 – U16.

KOCHA WA ZAMALEK

Kocha mkongwe mwenye umri wa miaka 66, Jorvan Vieira ambaye amewahi kufundisha klabu kadhaa kubwa Afrika na Brazil naye yumo kwenye orodha ya wanaowania nafasi ya Zahera.

Vieira ni Mbrazili ambaye enzi zake alicheza katika timu za Botafogo na Vasco da Gama za Brazil, aliwahi kuinoa Zamalek mwaka 2012 hadi 2013 pamoja na Ismaily mara mbili na ana uzoefu wa soka la Afrika kwa muda mrefu.

KOCHA MSAIDIZI

Upande wa kocha msaidizi Mnigeria, Felix Ifeanyi Nwosu mwenye elimu ya CAF leseni C ndiye ana nafasi ya kutua nchini kuwa kama kocha msaidizi wa kukinoa kikosi hicho.

Mnigeria huyo aliwahi kuzifundisha timu za FC Talanta inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Kenya, Heegan FC ya Somalia, timu ya taifa ya Wanawake ya Nigeria ‘Dream Stars’, Ambassador Child Youth Club (Nigeria).

KOCHA WA MAKAMBO YUMO

Mbali na hao, chanzo kingine cha habari kimewataja makocha wengine ambao wameshatuma wasifu wao klabuni hapo wakiomba ajira, akiwemo kocha ambaye alikuwa akimfundisha straika wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo.

Kocha huyo ni Didier Gomes da Rosa raia wa Ufaransa ambaye hivi karibuni alifukuzwa kazi katika kikosi cha Horoya kutoka Jamhuri ya Guinea.

Rosa alifukuzwa kazi katika kikosi hicho kutokana na kutofikia malengo ya klabu ya kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa timu yake ilitolewa hata kabla ya kufika hatua ya makundi.

Timu hiyo ilifika robo fainali mara mbili, hivyo mipango yao ilikuwa ni kusonga mbele zaidi.

Makocha wengine

CV za makocha wengine ambazo zimetumwa klabuni hapo pia, zinatoka katika nchi za Serbia, Yugoslavia, England, Ivory Coast, Brazil, Ujerumani na Ureno.

8 COMMENTS:

  1. Timu abaki NATO mkwasa anatosha kabisa

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hapana kiwango cha Mkwasa ni cha kawaida pia afya yake hatujui ya huko mbeleni anatakiwa Kocha nje ya Afrika mwenye kiwango cha UEFA

      Delete
  2. Mkwasa anatosha msilete matakataka ya bei kubwa

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hapana kiwango cha Mkwasa ni cha kawaida pia afya yake hatujui ya huko mbeleni anatakiwa Kocha nje ya Afrika mwenye kiwango cha UEFA

      Delete
  3. Yanga ni wa hovyo wakati wa dirisha kubwa la usajili mbwembwe tele lakini sasa hata robo msimu wa ligi bado tayari wanaanza kufukuza wachezaji, makocha,viongozi nakadhalika.Binafsi sikuona sababu ya kufukuzwa kazi Zahera. Kocha huwa anahitaji muda wa kujenga timu na nawasifu Simba kwa sasa hata kama vyombo vya habari mara nyingi hukimbilia kufurahia kutangaza mabaya yao ila Simba kuna memgi,mazuri sana ya kujifunza kwa klabu zetu za hapa nnchini. Simba imeonesha kuwa ni timu yenye uongozi uliojitosheleza.Ungozi wa Simba unampa nafasi kocha wao muda wa kujenga timu yake.Na naamini hata kama ipo siku Simba itachukua maamuzi mengine juu ya kocha wao basi hawezi kusema hakupewa nafasi ya kufanya kazi yake. Kocha wa Simba anapata mahitaji yake kamili.Ana benchi la ufundi lilokamilika kuanzia madaktari hadi wahudumu wengine. Anapata kambi bora za maandizi ya mwanzo wa msimu. Anawigo mpana wa wachezaji. Anauwezo wa kusajili mchezaji kila mchezaji anaetaka kumsajili lakini licha ya nguvu zote hizo alizonazo kocha wa Simba bado ameshindwa kuendana na kasi ya shauku ya wanasimba kuona timu yao ikiwa bora zaidi ya ilivyo sasa ila kwa busara viongozi wa Simba wanaoneakana wakifanya mambo yao kwa utulivu zaidi kuliko mihemko na muhimu zaidi kumpa nafasi kocha wao kufanya kazi kwani hata Guadiola pale England hufungwa na vitimu vya hovyo tu zidi ya timu ya matajiri ya wenye visima vya mafuta.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hapana kiwango cha Mkwasa ni cha kawaida pia afya yake hatujui ya huko mbeleni anatakiwa Kocha nje ya Afrika mwenye kiwango cha UEFA

      Delete
  4. Ndo vikocha kama Desabre vinasema haviijui Yanga? Sasa kama ndo hivi mbona wengi wakubwa tu wanaomba kufundisha

    ReplyDelete
  5. Wasisahau kuwaambia hao makocha kuwa Kama timu inakwama sehemu watoe hela zao ili kuokoka jahazi.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic