November 15, 2019





NA SALEH ALLY
NIKIKUAMBIA ni deni naweza kukushtua lakini uhalisia unaonyesha kuwa sisi mashabiki au wapenda soka, kuna kitu tunadaiwa katika mpira wa nchi yetu na hasa pale unapozungumzia timu ya taifa.

Timu yetu ya taifa inajulikana kama Taifa Stars, kwa sasa imekuwa moja ya timu tishio katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hii ni kutokana na mafanikio kadhaa ambayo yamepatikana mfululizo.

Ilishiriki Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon, ilikuwa ni mara ya pili na mara ya mwisho ikiwa mwaka 1981. Baada ya hapo, Stars ikaandika rekodi mpya kwa vizazi vya sasa.


Wakati bado kukiwa na shangwe za kufuzu ambazo ziliishia Misri kwa timu kutofanya vizuri, kwa mara nyingine tena timu hiyo imewatoa Watanzania kimasomaso kwa kufanikiwa kufuzu kucheza michuano mingine mikubwa ya Afrika.

Safari hii ni michuano ya Chan, hii inafuatia kwa ukubwa baada ya Afcon. Inashirikisha wachezaji wa ndani ya Bara la Afrika, yaani wanaocheza katika timu zilizo ndani ya bara hili.

Mara ya mwisho, Taifa Stars ilishiriki michuano hii mwaka 2009, timu ikiwa chini ya Kocha Mbrazil, Marcio Maximo. Ilifanyika katika miji miwili ya nchini Ivory Coast.

Ilikuwa jiji kubwa la Abidjan na Bouake, wakati huo ulikuwa ni mji wa wapinzani wakuu wa serikali. Katika soka mji huo ni maarufu kwa kuwa wanasoka wawili maarufu Yaya Toure na kaka yake, Kolo Toure wamezaliwa na kukulia katika mji huo.

Tanzania ndani ya muda mfupi, inakwenda katika michuano hiyo mikubwa. Hili ndilo deni ninalolizungumzia kwa kuwa wachezaji walio katika kikosi hicho wameonyesha hata kama uwezo hautakuwa mkubwa lakini ni wenye nia ya kufanya vema zaidi.

Wachezaji hao hiyo ni kazi yao lakini sote tutakubaliana kuwa ni mashujaa wanaolipigania hasa taifa lao. Wao ni Watanzania na ndio maana wanapambana kwa ajili ya taifa lao.

Kiuhalisia, sote hatuwezi kuingia uwanjani na kucheza. Kama wadau tunakuwa na kazi ya kuwapa moyo na kuwasisitiza mambo ya msingi ikiwemo kuwaambia wanaweza.

Maana yake, lazima tufike uwanjani na kuwaunga mkono. Tunapokwenda viwanjani kwa wingi hata wao hujiona wana deni kubwa.

Wanajiona wana deni kutokana na Watanzania wanavyojitokeza kwa wingi kuwaunga mkono huku wakionyesha kweli wanataka ushindi.

Watazamaji wanapokuwa kwa wingi jukwaani, wachezaji hujiona kuwa wanatakiwa kufanya jambo fulani kuwaepusha wale waliojitokeza.

Vizuri kwa wingi tukaenda uwanjani kwenda kuwapa deni wao kwa maana ya kuwahamasisha ili wapambane vilivyo na kuhakikisha leo wanashinda mechi dhidi ya Equatoria Guinea katika harakati za mapema kufuzu kucheza tena Kombe la Mataifa Afrika.


Sasa kauli ni “Twende Zetu Tena.” Hili haliwezi kukamilika au hatutalifikia kwa wachezaji pekee kuingia uwanjani huku wadau tukiwa tumekaa nyumbani au kwenye vibanda tukiangalia mechi sehemu nyingine.

Twende tukawe nao pamoja, twende Uwanja wa Taifa leo tukawaonyeshe tunahitaji ushindi na tunapenda timu yetu ishinde dhidi ya Equatorial Guinea.

Mechi za awali ni muhimu zaidi kuliko za baadaye, kama mnashinda hizi mnakuwa na nafasi ya kupanga hesabu za uhakika mapema, hivyo Stars hawapaswi kupoteza hata pointi moja katika mechi kama ya leo.

Unakumbuka, msimu uliopita kwenye kuwania kufuzu kucheza Afcon, mwishoni tulianza kulia na pointi za Lesotho ikionekana sare dhidi yao jijini Dar es Salaam ilikuwa ni walakini.

Tunaweza kuwa tumejifunza na walakini huo. Hivyo safari hii itakuwa vizuri tuwe tumejifunza kulingana na makosa na kitu muhimu kabisa ni kuungana na vijana wetu leo uwanjani na kuwashangilia mwanzo mwisho kwa kuwa timu wanayocheza nayo hatuijui vizuri na ubora wake ni jambo lisilotabirika.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic