December 26, 2019


ALIWAHI kutokea bwana mmoja aliyekuwa maarufu sana duniani katika miaka ya 1975, huyu jamaa aliitwa Arthur Ashe, mcheza tenisi wa Marekani aliyepata umaarufu mkubwa kwa kuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu hasa wale wenye asili ya Afrika, huyu jamaa aliwahi kusema hivi: “Success is a Journey, Not a Destination”, alimaanisha “Mafanikio ni safari na sio mwisho.”

Nimependa kuanza na bwana Ashe kwani maneno yake ndio msingi wa makala haya yanayomuangazia kiungo mshambuliaji hatari wa KMC, Hassan Kabunda, akitueleza changamoto kubwa alizowahi kukutana nazo katika maisha yake ya soka.

TUANZE NA HISTORIA YAKO KWA UFUPI

“Naitwa Hassan Salum Kabunda mtoto wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Salum Kabunda ‘Ninja’, kiufupi maisha yangu ya soka niliyaanzia katika kituo cha kukuzia vipaji cha DYOC jijini Dar, na baadaye nilielekea Ashanti Utd, ambako nilicheza kisha nikaenda Mwadui ya Shinyanga na mwaka 2018 ndiyo nikasajiliwa KMC ambako niko mpaka sasa.”

Zifuatazo ni changamoto kubwa alizowahi kukutanana nazo Hassan Kabunda;

AWEKWA BENCHI MECHI NANE KISA ZENGWE LA MWALIMU

“Unajua katika mpira unaweza kukutana na kocha akawa hakuelewi kabisa hata ufanye nini kiasi anaweza akakuweka benchi au hata kukutoa kwa mkopo na hili liliwahi kunitokea mimi nikiwa Mwadui ambapo kocha wangu kipindi hicho, Ally Bizimungu, aliniweka nje ya uwanja mechi nane bila sababu yoyote ya msingi, jambo ambalo lilinipa wakati mgumu sana kiasi cha kuniondolea hali ya kujiamini uwanjani.”

ASHUSHWA KWENYE BASI SAA TISA USIKU WAKIWA WANAELEKEA KWENYE MECHI

“Tukio lingine ambalo siwezi kulisahau ni lile la kushushwa kwenye basi la timu (akiwa Mwadui FC) saa tisa usiku tukiwa tunajiandaa na safari ya kwenda kucheza na Azam, eti kwa sababu watu waliokuwa wanaenda kucheza mechi walikuwa wamezidi, nakumbuka kocha Julio alikuwa anataka mimi nisafiri ila viongozi wakakataa, huwezi amini ilinibidi nishuke tu.”

APOKEA KIPIGO BAADA YA KUPIGA HAT-TRICK FAINALI

“Unajua mimi napenda sana mpira na mapenzi ya soka yalinipa wakati mgumu sana utotoni kwani nilikuwa napigwa sana na mama kwa sababu alikuwa akinikataza kucheza mpira na watu wakubwa akihofu wangeniumiza, sasa kwa ubishi wangu nakumbuka siku moja nilitoroka na kwenda kucheza mechi ya fainali ya ‘chandimu’ nikiwa naumwa, nikafanikiwa kufunga hat-trick kwenye mchezo huo ambao uliisha kwa sisi kushinda 4-2, basi ikawa shangwe pale tukafurahia sana ushindi, sasa ile kurudi nyumbani nikapokea kipigo kizito kutoka kwa mama lakini sikuacha kucheza kwa kuwa naupenda sana na uko kwenye damu.

“Hilo ni moja kati ya matukio mengi sana ya kupigwa kwa sababu ya mpira nakumbuka mama alikuwa akinipiga sana mpaka ikafika wakati akachoka na kuamua kunikabidhi kwa mjomba basi ilikuwa hatari mzee.”

ISHU YA MALIPO JE?

“Hapo kaka umegusa penyewe, unajua soka letu lina changamoto nyingi sana hasa linapokuja suala la malipo, nadhani unasikia hata Simba na Yanga jinsi changamoto hiyo ilivyo kubwa, suala linalopelekea usipokuwa mvumilivu unaweza hata kubeba mabegi yako na kurudi nyumbani, kwa mfano mimi binafsi Mwadui mpaka sasa naidai pesa yangu ya usajili, hivi ninavyokuambia nipo kwenye mchakato wa kupeleka madai yangu TFF ili kudai haki yangu kwani lile ni jasho langu.”

MATIBABU TATIZO HAPA NCHINI

“Unajua majeraha kwa mchezaji ni kawaida, ila changamoto huja katika suala la huduma za matibabu ambazo kwa kweli zina changamoto, na kwa upande wangu sikumbuki ni lini ila nakumbuka niliwahi kupata majeraha ya nyama za paja mazoezini tukiwa tunajiandaa na mechi kesho yake ambayo yaliniweka nje kwa muda mrefu kidogo na hili likichangiwa na huduma duni za kiafya kwa wachezaji.

“Nadhani hata wewe unaona kuna tofauti kubwa ya kwetu na wenzetu walioendelea kiasi kwamba huku kwetu kuna baadhi ya watu wamelazimika kuacha mpira kutokana na kushindwa kupata matibabu stahiki ya majeraha yao.”

NINI USHAURI WAKO KWA VIJANA WENYE MALENGO YA KUFANIKIWA KUNAKO SOKA?

“Kwanza niseme kuwa unapotaka kufanya jambo lolote lazima ujue utakutana na changamoto hivyo vijana wanaokuja kwenye soka wanapaswa kujitahidi sana kuwa wavumilivu, waachane na makundi potofu na starehe zisizo na mpango na wawekeze nguvu zao nyingi katika mazoezi, kuwa na heshima na zaidi sana wamweke Mungu mbele.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic