NA SALEH ALLY
TUSEME vipi sasa, kwamba ipi tofauti ya uongozi mpya wa Yanga na wale waliokuwa wanakaimu tukaomba ifanyike juhudi Yanga kupata uongozi mpya.
Yanga ilikuwa inakwenda kwa kusua, mambo mengi yalionekana yako kwa mikono binafsi badala ya uongozi sahihi ambao ungepeleka mambo sahihi.
Waliokuwa wanakaimu, tuliwaeleza ukweli kutokana na tunavyoona wanapeleka mambo kwa maslahi yao binafsi na si kwa maslahi ya klabu ikiwa ni pamoja na kuchelewesha mishahara katika kiwango cha kufikia hadi wachezaji wanaamua kugoma na kusababisha vurugu au mizozo isiyokuwa na sababu za msingi.
Ajabu, uongozi ulioingia hauna muda mrefu sana. Tayari tumeanza kuona yanayorejea sasa hayana tofauti kubwa na wale ambao walikuwa wanakaimu tu.
Hii inanifanya nianze kujiuliza kama mdau, kama mambo yanakwenda namna hii, Yanga walikuwa na sababu gani ya kufanya uchaguzi! Sote tunajua uchaguzi zaidi ulilenga kurekebisha mambo na kuyafanya mapya. Lakini kwa hali ilivyo, kama Yanga haijarudi palepale, basi imezidi kuporomoka katika suala la mpangilio sahihi na utaratibu unaotakiwa, nitakueleza kwa nini kwa ufupi tu.
Mfano, Kocha aliyeondoka, Mwinyi Zahera, alieleza aliendelea kutoa fedha zake mfukoni hata baada ya uongozi mpya kuingia. Jambo ambalo sikulitegemea, Zahera angetoa fedha za mfukoni wakati ule viongozi wanakaimu.
Sasa unaona, mchezaji kama Vicent Andrew ‘Dante’, hadi ameamua kususa, wazi inaonekana si suala la siku moja, si suala ambalo lilianza siku moja. Uongozi umeshindwa kulitatua, umeshindwa kumsaidia mchezaji huyo angalau kwa kuafikiana naye na kumlipa.
Juzi, wachezaji wa kigeni wameibuka wakidai fedha zao za mishahara na kusababisha taharuki miongoni mwa wachezaji wa Yanga hasa karibu kila mmoja akitaka kuvunja mkataba huku Sadney Urikhob akiamua kuvunja mkataba na kuondoka zake kutokana na kuona maisha yamekuwa magumu. Yeye amesema, hajalipwa mshahara wa miezi mitatu, uongozi umesema hajalipwa miezi miwili.
Ukiachana na Mnamibia huyo, beki Lamine Moro raia wa Ghana, mshambuliaji David Molinga raia wa DR Congo naye anataka kuvunja mkataba pia na Yanga imekuwa ikipambana kumbakiza.
Wachezaji kutoka Rwanda kama Issa Bigirimana naye aliondoka, ilielezwa ni sababu ya majeruhi. Lakini baadaye atatumika kama kigezo cha kushindwa kufanya vizuri ndio maana hakulipwa. Lakini tunaona wako wanaocheza na kufanya vizuri na hawajalipwa mishahara yao.
Nini tofauti ya wale waliokuwa wanakaimu wakawa hawajalipa mishahara ya miezi mitatu na sasa uongozi nao kuwa haujalipa?
Unaona wale wa wakati ule walikuwa na udhamini wa SportPesa na tulihoji kinachowafanya washindwe kulipa na wanalipwa shilingi bilioni moja kwa mwaka lakini sasa pamoja na mdhamini huyo kuna GSM ambaye yuko upande wa jezi lakini upande wa magodoro na hili ni sehemu ya yale ambayo tulikuwa tunaona ni mafanikio kwa idadi ya wadhamini kuongezeka.
Sasa wakati huo, Zahera anatoa fedha zake mfukoni tena, timu inasafiri kimkanda, wakati huu unaonekana mambo yamebadilika, wachezaji hawajalipwa fedha zao za usajili na baadaye tunasikia mishahara. Hii si sawa hata kidogo.
Najua, nitakuwa ninawakera sana kwa kuwa wengi ni rafiki zangu lakini kwa kuwa tunachoangalia ni maendeleo ya Yanga ambayo yatakuwa sehemu ya mafanikio ya timu ya taifa, basi ni lazima tuambiane ukweli.
Kuna haja ya kuacha kufanya mambo kwa mazoea na badala yake vitu viende kwa kufuata weledi na kusimamia usahihi.
Haya yanayotokea sasa yako ndani ya uwezo wa viongozi wa Yanga. Kikubwa waongeze ubunifu na wajue, timu ndio kitu cha kwanza kwa kuwa ndio kila kitu kwenye klabu.
Achaneni na hisia au mawazo eti mapenzi kwanza. Una mapenzi na klabu wakati wewe ni mchezaji na nyumbani kwako hawana matumizi, utacheza vipi katika ubora wako?








Ni kweli saleh umeongea kitu tatizo la viongozi wetu kusema ukweli hawawezi ingekua busara kwaviongozi was yanga kuwaambia ukweli wanachama wao ili wajue halihalisi ndani ya club yao
ReplyDeletePesa za KUBWA KULIKO NA ZA UDHAMINI ZINAKWENDA WAPI?
ReplyDeleteKweli kabisa tatizo team ya yanga Haina mpangilio Bora we atawala ndo maana wanayumba Sana kiichumi
ReplyDelete