*Hata ukimchukia hatapoteza lolote, hamumtaki kwenye tasnia ya uchambuzi, nyie ni kina nani hasa hadi mpange na wachambuzi..!
Na Saleh Ally
BONDIA Mtanzania, Hassan Mwakinyo alifanikiwa kumshinda kwa pointi Mfilipino Arnel Tinampay ambaye hakuna ubishi alionyesha kiwango kizuri na kusababisha mjadala mkubwa.
Mjadala ulikuwa ni Mwakinyo kuwa alipoteza au hakushinda na kila mmoja aliamini alivyoamini. Lakini tupo tuliojivunia ushindi mgumu wa Mwakinyo lakini ushauri ukawa ni lazima ajifunze kupitia pambano hilo gumu kupitia Tinampay ambaye ni sehemu ya kikosi cha bondia maarufu duniani, Manny Pacquiao.
Wakati mjadala ukiendelea, Mwakinyo ameibuka na jambo jipya, la ajabu na kushangaza na hasa unapolisikia kwa mtu kama yeye akiamua kumshambulia gwiji wa masumbwi nyumbani Tanzania, Rashid Matumla ambaye awali alijulikana kama Snake Boy, sasa wanamuita Snake Man.
Sauti ya Mwakinyo imesikika ikimshambulia Matumla kwa madai alimkosoa kocha wake wakati wa pambano lake na Tinampay, wakati huo Matumla akisema hayo alikuwa ni mchambuzi katika runinga ya Azam TV ambayo ilimualika.
Ajabu pamoja na kuzungumzia kuchukizwa na maneno ya Matumla, Mwakinyo amepeleka kashfa rundo kwa Matumla kwa kumuita eti “anavaa masuruali kama ya Tupac”, “bondia aliyekuwa akipoteza mapambano mfululizo.”
Hakutaka kocha wake akosolewe eti kwa kuwa naye Matumla hakuwa kocha bora na ndio maana watoto wake hawakufika kokote. Tena anawaomba Azam iwapo watafanya pambano pamoja naye, wasimuweke tena Matumla kwa kuwa alimkosoa kimajungu na kusababisha watu waone kama vile hajui.
Unajua hapa tunaweza kujifunza mambo mengi sana na kwanza kabisa kuangalia Mwakinyo anayemuambia Matumla kapoteza heshima kwake, hasa asipomuomba radhi kocha wake.
Binafsi imenisikitisha sana, sikutegemea bondia aliyekuwa ulingoni aanze kugombana na wachambuzi. Mfano leo, Ally Mayay anachambua pale Azam wakati wa Ligi Kuu Bara eti baada ya mechi umsikie John Bocco au Kelvin Yondani akigombana naye kwa kumpa maneno makali huku akitaka Azam wamuondoe.
Wamuondoe yeye kama nani, kwa kipi cha kupata heshima hiyo ya kuingilia hadi vyombo vya habari na kutengeneza amri kwa kutaka kutumia kigezo cha watu wengi alionao. Wangapi? Kama ni Wanatanga hivi wote unafikiri wanaweza wakawa wameunga mkono kitendo chake ambacho hakifanani na kiwango alichofikia?
Kama ungesema ni ubora na heshima kwa taifa, leo Matumla bado yuko juu zaidi maradufu ya Mwakinyo na hajawahi kuonyesha dharau ya namna hii na akazungumza maneno yasiyo na pumzi kama hayo.
Tunajivunia Mwakinyo aliyecheza mapambano 17, akashinda 15, kati ya hayo 11 ni KO na amepoteza mawili. Tunajivunia yeye kuwa na ubingwa wa UBO katika uzito wa Super Welter akiwa amempiga Joseph Sinkala pia taji la ubingwa World Boxing Pan African aliomshinda raia wa Botswana Anthony Jarman. Pia ana taji la uzito huo aliomshinda Fadhili Keya.
Pamoja na hivyo wakati tukijivunia Mwakinyo, tunajivunia zaidi kuwa na Matumla na familia yake. Matumla ambaye tunamuita gwiji kwa kuwa kafanya mengi makubwa ambayo leo, Mwakinyo hajafikia nusu na huenda kwa matarajio ndio alikuwa anakwenda kama angeamua kuwa bondia hasa.
Mabondia wanazungumza zaidi kwa mikono kwa maana ya utekelezaji. Bondia pekee aliyekuwa na maneno mengi zaidi ya wengine wote na akafanikiwa ni Mohamed Ali tu na alifanya hivyo kwa wapinzani wake, si wakubwa zake.
Angalia, mwaka 1997, Matumla alimchapa Mcameroon na kubeba ubingwa wa African Boxing Union (ABU). Mwaka 1998, hii nakumbuka ilikuwa Diamond Jubilee, akamtandika raia wa Hungary, Andras Galfi na kubeba ubingwa wa dunia wa World Boxing Union (WBU). Mwaka uliofuata Matumla akasafiri hadi Italia ambako alimchakaza Muitaliano, Paolo Tizzamiglio kwa TKO na kurudi na ubingwa wake.
Kwa wale mnaokumbuka, Matumla alipokonywa ubingwa huo kwa kushindwa kuutetea lakini mwaka 2002, akapanda ulingoni nchini Afrika Kusini na kumtwanga Garry Murray, akabeba tena ubingwa wa International Boxing Union (IBU). Ushindi huo ulimfanya azawadiwe gari aina ya Mercedes Benz, kwa wakati ule akaweka rekodi ya kuwa bondia anayeendesha gari hilo la kifahari, sijui kama ilivunjwa baadaye.
Kabla Matumla alishikilia mkanda wa ubingwa wa taia wa Welter kwa muda mrefu sana. Hiki ndicho kile kipindi cha ngumi zikiwa juu hasa. Ushindani wa Matumla ulikuwa kwa Joseph Marwa, ukahamia kwa Maneno Oswald na mwisho ukawa ni kwa Francis Cheka.
Matumla ameendelea kupigana kwa zaidi ya miaka 15 akiwa bado ni bondia maarufu na anayebeba mataji, jambo ambalo anastahili sifa zaidi na inamuweka kuwa mmoja wa mabondia wachache bora zaidi na zaidi kutokea katika nchi yetu.
Wakati mwingine ingekuwa si vibaya kumuona Matumla akidharauliwa na mwanasoka au shabiki. Si sahihi hata kidogo kwa bondia huyo kudharauliwa na bondia tena bila ya kuwa na kosa lolote.
Ninaamini Matumla ni kipenzi cha Watanzania, na hata Tanga kuna watu wanamuelewa hasa, wanamkumbuka na kuuthamini mchango wake kwa kuwa alikuwa nembo ya taifa na atabaki hivyo hadi mwisho wa maisha yake.
Matumla hawezi kuteteleka kwa kukosa heshima ya mtu mmoja, wawili, watatu au kumi. Ana heshima ya taifa hili ambayo inatokana na kazi kubwa aliyoifanya ambayo wengine akiwemo Mwakinyo wanalazimika kufanya kazi kubwa kuifikia.
Binafsi nilimuunga mkono Mwakinyo kwa juhudi zote tokea mwanzo na hata baada ya pambano, nilikuwa tofauti na maoni ya walioona kapigwa. Lakini siwezi kuunga mkono mambo ya hovyo kama haya ambayo tumepita kwingi hakukuwa na uropokaji wa namna hii. Mkumbuke, kabla ya Mwakinyo, tumekuwa na mashujaa wengi ambao walipambana katika ngumi na ndio maana leo wapo kina Mwakinyo.
Ninaamini Matumla ana busara sana, heshima yake haiwezi kushushwa na Mwakinyo bado ni kinda kwake. Vizuri akapuuzia na kuendelea na maisha yake, Mwakinyo akiwa muungwana, ataomba radhi, asipofanya hivyo iko siku dunia itamhukumu, tuombe uzima.
MWISHO:
BLOG ya SALEHJEMBE inampongeza Mwakinyo kwa kukubali kuomba msamaha kwa Matumla, kitendo ambacho kinaonyesha uungwana.
Pamoja na hivyo, Blog hii inawapongeza Watanzania wapenda michezo kwa kukataa kuona Matumla akidharauliwa na Mwakinyo. Walimtetea licha ya yeye kukaa kimya. Hongereni sana.









0 COMMENTS:
Post a Comment