December 4, 2019


Wakati Kocha Msaidizi akiwa Selemani Matola, jina la Kocha Mkuu wa AS Vita ya DR Congo, Jean-Florent Ikwange Ibengé limetajwa kuwa ndiye anayetarajiwa kumrithi Mbelgiji, Patrick Aussems katika Klabu ya Simba.

Tayari Championi linajua kuwa Simba wameshazungumza na Ibenge ambaye ni mmoja wa makocha wakubwa Afrika. Amekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya DR Congo kwa miaka mitano kuanzia 2014 hadi 2019 alipoamua kuachana na timu hiyo na sasa yupo huru.

Licha ya Ibengé kuchukua nafasi kubwa, lakini wapo makocha baadhi watatu kutoka Afrika, mmoja wapo huenda akatua Simba kama Ibenge akionekana kuwa mzito kukubali ofa hiyo.

Baadhi ya makocha wa Afrika ambao hivi sasa hawana kazi ni Mkongomani Mwinyi Zahera ambaye naye anatajwa, Mnigeria Emmanuel Amunike aliyekuwa Taifa Stars.

Beston Chambeshi aliyetumuliwa na Nkana Rangers ambaye hivi anaifundisha timu ya taifa ya vijana ya Zambia naye anatajwa katika nafasi hiyo Msimbazi.

Mwingine anayepewa nafasi kubwa ni Mfaransa Didier Gomez, ingawa huyu atapewa nafasi kama makocha wa Kiafrika wakishindikana.

Gomez kwa sasa ni bosi wa Klabu ya Horoya AC ya Guinea ambapo hivi karibuni alimsajili aliyekuwa straika wa Yanga, Heritier Makambo, raia wa DR Congo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatatu, limezipata zimedai kuwa hivi karibuni uongozi wa Simba ulifanya mawasiliano na Gomez kwa ajili ya kuja kuchukua nafasi ya Aussems.

“Hata hivyo, baada ya uongozi kuwasiliana na kocha huyo, alituma mwakilishi wake hapa nchini kwa ajili ya kuja kuangalia suala zima la utendaji wa timu hiyo.

“Jamaa huyo pia alikutana na Aussems na kuzungumza naye kisha akaondoka zake lakini baada ya siku chache tangu jamaa huyo aondoke, Gomez alimpigia simu Aussems na kumuulizia hali ya mambo jinsi ilivyo ndani ya Simba,” kilisema chanzo hicho.

Gomez pia amewahi kuzifundisha timu za Rayon Sports ya Rwanda, AS Cannes B ya Ufaransa na CS Constantine ya Algeria.

Mtu anayepewa nafasi kubwa ni Ibenge, lakini mtoa taarifa huyo alisema kuwa kitu kitakachomzuia Ibengé kujiunga na Simba labda mshahara mkubwa atakaoutaja, lakini siyo vingine.

Hivi sasa wapo kwenye mazungumzo naye ili arejee kuuwahi mchezo wa watani wa jadi, Yanga, unaotarajiwa kupigwa Januari 4, mwakani.

“Yapo majina mengi ya makocha yaliyopo kwenye mipango yetu, hivyo bado Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba imeendelea na vikao vyake kwa ajili ya kumpitisha mmoja atakayekuja kuifundisha timu yetu.

“Mabosi hao wamepanga kumuajiri kocha ambaye hivi sasa hana klabu ya kuifundisha kwa kuepuka gharama ya kusitisha mkataba na kocha anayetakiwa ni kutoka Afrika.

“Na Bodi ya Wakurugenzi wamefikia makubaliano mazuri ya kutomrudisha kocha yeyote aliyewahi kuifundisha Simba, zaidi wanataka kocha mpya ambaye hajawahi kuinoa timu yetu.

“Na kati ya hao ni Ibengé aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya DR Congo na klabu ya AS Vita ya nchini huko ndiye anayepewa nafasi kubwa pamoja na Mfaransa Gomez,” alisema mtoa taarifa huyo.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Anold Kashembe alizungumzia hilo kwa kusema: “Bado tunaendelea na mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya, suala la nani anayekuja bado muafaka, ni vema mkasubiria tutatoa taarifa kwenye Vyombo vya Habari.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic