NA SALEH ALLY
SASA hatunaye tena mzee wetu Ibrahim Akilimali ambaye ametangulia mbele ya haki na jana yalikuwa ni mazishi yake.
Mwenyezi Mungu amrehemu mzee wetu huyo ambaye tuna mengi ya kumkumbuka ambayo yako tunaweza kuyaacha na mengi tukayachukua kwa lengo la kufanya jambo zuri.
Kama lilivyokuwa jina lake, akili yake ilikuwa ni mali na faida katika mchezo wa soka nchini ingawa yeye binafsi alianzia upande wa klabu yake aliyoipenda kwa dhati, Yanga.
Yanga ndio klabu kongwe nchini, bila shaka hatuwezi kushindwa kusema Akilimali alikuwa mmoja wa mashabiki wakongwe kabisa wa soka nchini.
Mashabiki waliokuwa wakiweza kuielezea Yanga, Simba na soka yetu kwa jumla tangu katika miaka ya kuanzia 1960 kuja juu kwa ufasaha kabisa.
Mzee Akilimali alikuwa amekula chumvi ya mchezo wa soka hapa nchini. Ndio maana alikuwa na mengi sana ya kuelezea ingawa kuna sehemu alikosea.
Katika mambo ambayo nilimpinga sana hata tulipokutana mara kadhaa alitaka tujadili ni kuhusiana na kukataa Yanga kuwa chini ya Yusuf Manji kwa takribani miaka 10 kwa mkataba.
Niliamini ilikuwa sahihi vile kwa kuwa Yanga ingeendelea kupata fedha bila ya presha kubwa na bado ingeendelea kujijenga kabla ya kurejeshwa na Manji, nikiamini ingekuwa katika kiwango kikubwa cha mabadiliko huenda hata kuliko walivyofikia Simba leo hii. Mara kadhaa, alikuwa akiniambia alighafirika na huenda kulikuwa na jambo na Manji, yaani kati yao wawili.
Baada ya miaka kadhaa, nikaanza kujiuliza kama kweli Akilimali alikuwa ameona mbali kuliko mimi hasa baada ya Manji kupata matatizo kifedha na baadaye kuonekana kampuni zake ziko katika hali mbaya ya kifedha.
Je, Yanga Yetu ingekuwa inaendesha klabu hiyo mambo yangekuwaje? Kungekuwa na athari au la? Hii nayo ikanifanya niamini huenda aliona mbali.
Pamoja na hivyo, mengi Akilimali alifanya kuanzia kwa viongozi, wachezaji na hata mashabiki pale alipoona kuna kitu hakiendi sawa, alisema bila ya woga.
Wachezaji waliokuwa wakisuasua huku wakijua wamepewa dhamana kubwa ya kuitetea klabu hiyo. Aliwaeleza wazi na mmoja wao ni Obrey Chirwa na baada ya muda kweli akarejea kwenye kiwango, Akilimali akaibuka na kumsifia kwamba hicho ndicho alikuwa anataka.
Viongozi wanajua kuhusiana naye na alikuwa na sauti zaidi ya ile ya radi. Alijua namna ya kuyapanga mambo na wakati mwingine alikuwa wazi kabisa kwa kuwalenga walioboronga moja kwa moja kwa kuwataja majina hata wale viongozi waliokuwa madarakani.
Baada ya maneno yake wengi walijirekebisha na tunajua namna ambavyo baadaye mambo yalikuwa. Hakika Akilimali, amekuwa ni shujaa wa Yanga mara nyingi na akisema ukweli bila ya woga.
Akilimali hakujali kuhusiana na umasikini wake. Hakunyong’onyea sababu ya kipato chake, wala hakurudi chini sababu ya kiwango cha elimu yake. Alisema alichokiamini bila ya kujali wakosoaji watakosoa kwa kiwango kipi.
Watu wa aina yake ni wachahe sana, wale wanaokubali hata kukosea lakini wakaamsha mjadala ambao baadaye unakuwa msaada kwa kile ambacho kina faida ya watu wengi.
Hakuna ubishi, itafikia siku tutakumbuka na kuamini angekuwepo Mzee Akilimali, angeweza kusema na mambo yakarekebishwa. Lakini hatukonaye tena na inawezekana ikawa vizuri zaidi kama tutachambua na kuchukua mazuri yake au mfumo wake imara wa kusimamia kinachoaminika au kukosoa bila ya woga.
Hakuna mkosoaji aliyewahi kukubalika kwa watu wote. Lazima maneno machafu na lawama zitamuangukia ingawa alichokisema kikisaidia mabadiliko hakuna ambaye atamkumbuka alikuwa chanzo cha kilichotokea.
Nimewahi kufika nyumbani kwa Mzee Akilimali, hakika alikuwa Mtanzania wa kawaida kabisa ambaye nilishangazwa na yeye kutokuwa na woga hata mbele ya vigogo lilipofikia suala la Yanga.
Niliamini hata kama alifaidika, lakini Yanga ilifaidika zaidi kupitia yeye ambaye wengine waliona kuhojiwa kwake kama ni kero.
Leo, nivipongeze vyombo vyote vya habari vilivyompa nafasi Mzee Akilimali kuzungumza jambo wakati wa uhai wake.
Vyombo hivyo vilionyesha haki kwa kila Mtanzania na mdau wa michezo na kufuta hisia za kuwa kila anayezungumza lazima awe kigogo au mwenye fedha nyingi au cheo kikubwa.
Mzee Akilimali hakuwa na cheo lakini alipewa nafasi na ndio maana leo wengi tunamkumbuka na vyombo vya habari ndivyo vilivyofikisha yote aliyoyasema. Na huu ndio wakati wakati wa kutafakari kila linalokugusa kutoka kwake na haki na ukweli, ilikuwa ndio kauli yake kuu.
Pumzika kwa Amani mzee wetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment