December 1, 2019







Na Saleh Ally
MIEZI 18 tu imetosha kusitisha chai ya Unai
Emery ndani ya Klabu ya Arsenal.

Hakuna kombe alilolichukua, ameiongoza
Arsenal kwa mechi 78 tu, kati ya hizo, raia
huyo wa Hispania ameshinda 43, sare 16
na kapoteza 19 akiwa na wastani wa
ushindi wa 55.13.

Presha imeongezeka zaidi kwa Arsenal
baada ya kupoteza mechi yao ya Europa
League kupitia king’amuzi cha StarTimes
wiki hii watakuwa waliona namna Arsenal
ilivyoshindwa kufurukuta ikiwa nyumbani na
mashabiki wakiwa wamesusa kujitokeza
kwenye Uwanja wa Emirates.


Arsenal ilipoteza baada ya kuchapwa na
Wajerumani, Eintracht Frankfurt tena
wakiwa nyumbani Emirates kwa mabao 2-1,
mechi ambayo kupitia king’amuzi cha
StarTimes ilionyeshwa moja kwa moja huku
uwanjani kukiwa na mashabiki wachache kabisa.

Mashabiki ndiyo wamekuwa presha ya
mwisho ya Unai kwa kuwa klabu hizo
zinafanya biashara na mashabiki wanakuwa
kila kitu maana sasa mambo yamebadilika.


Kocha huyo alionekana ndiye ambaye yuko
katika hali ngumu zaidi, wengi walihoji
kuendelea kwake kuwepo Emirates, Arsenal
ikaendelea kusuasua na hakuwa ameibuka
na ushindi kwa mechi sita mfululizo.


Katika mechi hizo sita, Arsenal imetoka sare
tatu na kupoteza tatu huku wakiwa
hawajashinda hata moja. Jambo ambalo
limeifanya presha iwe kubwa zaidi.


Mmiliki wa Arsenal, Stan Kroenke, jana
mchana alikuwa akisubiriwa kutoa uamuzi
wa mwisho kuhusiana na kocha huyo
kubaki au atupiwe virago. Lakini ujumbe wa
mtoto wake aitwaye Joshua Kroenke kupitia
mtandao wa kijamii wa Twitter ndiyo
hatimaye uliwashitua watu baada ya
kuandika akimtakia kila la kheri Unai.


Mfano, sifa ya kubeba mfululizo Kombe la
Europa League lakini mambo yamegoma
akiwa na Arsenal ambayo mara ya mwisho
aliiongoza Arsenal kushinda bao 1-0 dhidi
ya Bournemouth, Oktoba 6, mwaka huu.


Huenda kusingekuwa na sababu ya
kumuondoa na Arsenal walionekana ni
wavumilivu wakubwa katika suala la
makocha hasa kipindi cha Wenger.

Inakumbukwa kuwa enzi hizo mashabiki
waliingia uwanjani na mabango kama
walivyofanya hivi karibuni kwa Unai, pia
waliwahi kususa lakini Arsenal iliendelea
kumshikilia kocha huyo ikihakikisha
anaendelea kubaki.

Ukubwa wa Arsenal huenda unaweza
usionekane kama hautapata nafasi ya
kufika kwenye Uwanja wa Emirates au
katika moja ya mechi zake.

Arsenal ni kubwa hasa na inategemea
kwelikweli mashabiki wake kama sehemu ya biashara. Uongozi unajua hauna ujanja
na hauwezi kufanya biashara kama
mashabiki watakuwa “wamekunja mioyo
yao” dhidi ya klabu yao.

Inatumia mamilioni ya pauni kujiendesha,
hivyo lazima ifanye biashara kubwa kama
watu kuingia uwanjani kwa wingi, watu
kununua vifaa vyake, pia suala la haki za
runinga ambalo timu yenye mvuto zaidi
ikiwemo kuwa na mashabiki wengi
uwanjani, mechi zake zinaonyeshwa zaidi.


Arsenal haiwezi kuwa na mechi zisizokuwa
na mashabiki. Hivyo inaonekana wazi
ulifikia wakati wa kuchagua Unai au
mashabiki wake ambao ndiyo “madereva”
wa timu na klabu hiyo maarufu.


Uvumilivu kama ule wa Wenger haukuwa
na nafasi tena na hii inakwenda kwenye ule
mfano wa Alex Ferguson na Manchester
United ambayo kwa chochote ingemvumilia
kocha huyo lakini baada yake, David Moyes
hakupata nafasi hiyo kama ilivyokuwa kwa  Louis van Gaal na Jose Mourinho.

Hii inadhihirisha ukubwa wa makocha wawili
wakubwa ndani ya Ligi Kuu England ambao
wameandika historia kubwa kwa kipindi
kirefu.

Wenger alitua Arsenal mwaka 1996
akitokea Grampus Eight ya Japan wakati
Ferguson alijiunga na Manchester United
mwaka 1986 akitokea Aberdeen ya kwao
Scotland na hawa ndiyo makocha pekee
ambao wangeweza kuwa na nguvu zaidi ya
mashabiki.

Ferguson alipata kashkash kubwa kati ya
mwaka 1986 na 1988. Lakini uongozi chini
ya Edward Martin aliyekuwa mwenyekiti
ulishikilia msimamo na kuhakikisha anabaki
hadi mwisho. Baada ya pale, Ferguson
alikuwa na maisha mazuri sana kwa kuwa
mafanikio taratibu huku yakipanda
yalionekana.

Ferguson hakutoka licha ya mashabiki
kutaka aondoke hadi alipowaziba midomo

na mafanikio yake. Wenger hali kadhalika,
mambo yalikuwa mazuri mwanzoni, katikati
lakini mwishoni yakayumba kabisa na
unaona miaka yake takribani saba ya
mwisho haikuwa “mitamu” kwake na
mashabiki walitaka aondoke, lakini ikawa
ngumu kwao.

Lazima leo wanamkumbuka au
kumzungumzia kutokana na mwendo wa
timu yao lakini hakuna ubishi, juhudi zao za
kumng’oa Arsenal zilikwama kwa muda
mrefu sana.

Leo unaona namna Unai alivyong’oka
kirahisi. Hata miaka miwili tu imekuwa kazi
kwake, inaonyesha wazi kuna ugumu kuja
kupata nguvu ya kocha kama Wenger ndani
ya Arsenal.


Imeonyesha kuwa Arsenal si kwamba
walikuwa wagumu kumfukuza kocha badala
yake nguvu ya Wenger ndani ya klabu hiyo
ilikuwa ni kubwa sana na ikawapa wakati
mgumu viongozi kuamua kile walichoona ni
sahihi.

Sasa tumejifunza jambo kwamba Arsenal si
wavumilivu kama tulivyoamini, nguvu ya
Wenger iliwalazimisha kuwa na subira.
Heshima yao kwake iliwalazimisha kusubiri
tena na tena lakini sasa kwa kocha yeyote
atakayeharibu baada ya kutua Emirates,
ategemee kibuti.


MECHI SITA ZILIZOPITA...
Watford 2-2 Arsenal
Sheffield 1-0 Arsenal
Arsenal 2-2 Crystal Palace
Leicester 2-0 Arsenal
Arsenal 2-2 Southampton

Arsenal 1-2 Frankfurt

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic