MAMBO MATATU UTATA WA USHINDI KWA MWAKINYO VS TINAMPAY
BONDIA wa ngumi za kulipwa Tanzania, Hassan Mwakinyo, juzi alifanikiwa kumchakaza kwa pointi mpinzani wake, Arnel Tinampay raia wa Ufilipino.
Katika pambano hilo la kimataifa lililokuwa la raundi kumi ambalo halikuwa la ubingwa, lilifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku likiweka rekodi ya kuwa pambano la kwanza kuhudhuriwa na mashabiki wengi hapa nchini.
Ushindi wa Mwakinyo umeonekana kuwa na utata mkubwa kutokana na majaji kutoa pointi nyingi kwake tofauti na vile uhalisia wa pambano ulivyokuwa, hali iliyopelekea kuzuka mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii juu ya ushindi huo.
Jaji wa kwanza alimpa Mwakinyo pointi 97, na Tinampay 93. Jaji wa pili alitoa 98 kwa Mwakinyo na 92 Tinampay, wakati jaji wa tatu alitoa 96 kwa Mwakinyo na 96 kwa Tinampay.
Lakini kabla ya kuanza kwa pambano hilo, kulijitokeza utata kufuatia Mfilipino huyo kugomea glovu alizopewa kwa madai ya kuwa hazikuwa rasmi kwa ajili ya pambano, hivyo akaomba zibadilishwe kwake na kwa Mwakinyo.
Spoti Xtra linakuchambulia mambo yaliyoonesha utata wa ushindi wa bondia huyo huku wengi wakitarajia kwamba angeshinda kirahisi kama alivyokuwa akijigamba.
MZITO
Hii itakuwa si mara ya kwanza au huenda ukawa ndiyo mtindo wake alioamua kuutumia Mwakinyo katika mapambano yake.
Juzi Mwakinyo alionekana kuwa mzito zaidi katika kufungua mikono kwa kupiga ‘vinu’ vizito kwa Tinampay, licha ya kupiga ngumi za pointi, lakini katika raundi ya kwanza hadi ya tatu hakuweza kufunguka kuonyesha moto wake.
Rejea pambano lake kule England dhidi ya Sam Eggington, ambalo aliweza kushinda kwa TKO ya raundi ya pili na lile la Kenya dhidi ya Sergio Eduardo Gonzalez raia wa Argentina.
Hapa kama Mwakinyo angegundua jambo hilo mapema na kulifanyia kazi huenda makelele yanayoendelea katika mitandao ya kijamii leo yasingekuwepo tena kubeza ushindi wake kutokana na kumzidi vitu vingi kiufundi mpinzani wake.
Mwakinyo hakuwa kabisa na spidi ambayo ilipelekea kumchakaza vibaya Sam kwa kuwa kila wakati aliopata kuzipeleka ngumi kwa mpinzani wake hakuweza kuzifanyia muunganiko licha
ambaye alikuwa akirusha ngumi zake kwa tahadhari huku akitumia muda mwingi kujiweka kwenye kamba za kona hali ambayo ilikuwa ikitoa fursa kubwa ya kushambuliwa kila wakati alipokuwa akijazwa kwenye maeneo hayo.
HAKUWA NA MIPANGO
Huenda Mwakinyo alicheza kwa woga wa kuhofia kupigwa KO na Tinampay kwa kuwa anatokea kwenye kambi ya bondia bora duniani, Manny Pacquiao, hiyo ilipelekea kukosa mipango ya maana kukamilisha kazi yake mapema kama alivyofanya kwenye mapambano yake manne ya mwisho ambayo alishinda kwa KO.
Kwanza Mwakinyo alimzidi urefu mpinzani wake, lakini pia alimzidi nguvu kwa asilimia kubwa, vyote hivyo juzi kwa upande wa Mwakinyo havikuweza kufanya kazi ilivyotakiwa.
Katika raundi zote kumi walizopigana juzi, mpinzani wake alishajua anacheza na bondia wa aina gani, alitumia udhaifu huo kumpa wakati mgumu Mwakinyo kuifanya kazi yake kama ilivyotarajiwa na wengi.
Mwakinyo hakuweza kuutumia vema urefu wake kwa kuwa alitakiwa arudi chini kidogo kupata usawa na mpinzani wake, halafu kwenda naye sawa lakini pia hakuweza kutumia udhaifu wa mpinzani wake kutumia ngumi nyingi zilizokuwa nyepesi kwa kuwa tayari anamzidi nguvu na urefu kwa asilimia kubwa.
Kitendo hicho ndiyo kilipelekea Mwakinyo kufukuzwa muda wote kwenye ulingo licha ya kuweza kupata nafasi ya kutuma makonde yaliyokuwa yanamfikia vilivyo mpinzani wake, lakini haikuleta furaha ilivyotarajiwa na wengi.
Hata hivyo, Mwakinyo amekiri kupata changamoto kubwa kutoka kwa bondia huyo tofauti na matarajio yake lakini amesisitiza hawezi kumridhisha kila mtu afanye anavyotaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment