Ametibua tena! Ndivyo unavyoweza kutafsiri baada ya staa wa Bongo Fleva, Abdul Rajab almaarufu Harmonize kushindwa kufanya shoo kwenye tamasha lililokuwa limeandaliwa na Radio NRG ya jijini Mombasa nchini Kenya, IJUMAA limedokezwa.
Tamasha hilo lililofanyika Jumapili iliyopita (Disemba 29, 2019) pia lilihusisha mwanamuziki nguli anayewika kwa sasa wa Nigeria, Burna Boy na wasanii wengine wa Kenya wakiwemo Nameless na Jua Cali.
Aidha, Harmonize au Harmo ambaye alipaswa kuwa mmoja wa wasanii waliotarajiwa kupafomu kwenye tamasha hilo, imeelezwa kuwa alikataa kukamua baada ya waandaaji hao kukiuka makubaliano ya malipo ya shoo hiyo.
SABABU HIZI HAPA
Kwa mujibu wa meneja wa Harmo; Jembe ni Jembe ni kwamba waandaaji hao wa NRG walitaka kumlipa kiasi cha fedha kilichobakia kulingana na makubaliano yao baada ya kukusanya pesa za kiingilio katika mauzo ya tiketi mlangoni.
Alisema ingawa Harmo aliwasili mapema nchini humo na mpenzi wake na kujivinjari katika viunga mbalimbali vya jiji hilo kuhamasisha Wakenya kushiriki tamasha hilo ambapo mambo yaliingia doa baada ya kubainika kuwa waandaaji hawana pesa za kumalizia malipo yake kwa mujibu wa makubaliano.
“Huu ni udhalilishaji, hatuwezi kufanya kitu hicho,” aliandika Jembe ni Jembe kwenye mazungumzo yaliyonaswa na moja ya vyombo vya habari nchini humo.
ALIVYOKITIBUA KWA WAKENYA
Kutokana na Wakenya hao kumsubiri kwa hamu Harmo bila mafanikio, baada ya kukacha kupafomu kwenye tamasha lililokuwa linafanyika katika Uwanja wa Mombasa Sport Club huko Mombasa, baadhi yao walielezea hisia zao namna mwanamuziki huyo anavyowaangusha kila wanapojiandaa kupata burudani yake.
Malalamiko hayo yanakuja kwa kuwa hii ni mara ya pili kwa staa huyo kukacha kufanya shoo nchini humo, kwani Novemba, mwaka 2019, alikataa kufanya shoo katika tamasha moja ambalo lilikuwa linafanyika mjini wa Eldorent nchini humo.
Licha ya Wakenya kuwalaumu waandaaji wa tamasha hilo, pia walielekeza lawama kwa msanii huyo kwa madai kuwa sasa anapoteza imani kwa mashabiki zake.
Awamu ya kwanza msanii huyo alikwenda nchini humo na kuzunguka na magari ya matangazo kuwa atashiriki onesho hilo, lakini mambo yalikwenda kombo ambapo alipanda ndege na kurejea nyumbani, vivyo hivyo wiki iliyopita msanii huyo alikwea pipa na kuelekea Tandahimba alikokuwa na shoo ya kufunga mwaka.
“Kwa sababu hii ni mara ya pili, sasa tutamuamini vipi kuwa akija tena kutuhamasisha kuwa hakutakuwa na manenomaneno?” Alihoji mmoja wa Wakenya kwenye ukusara wake wa Twitter na kuungwa mkono na wenzake.
TAMASHA LAINGIA DOA
Kutokushiriki kwa Harmo pia hakukuacha salama tamasha hilo kwani msanii aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu, Burna Boy naye hakupafomu kwa wakati.
Ilielezwa kuwa msanii huyo aliyepaswa kupanda jukwaani saa tano usiku, alipanda saa tisa usiku, hali ambayo ilichochea hasira za Wakenya ambao tayari walikosa uhondo wa Harmo.
Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza kuwa Burna Boy alichelewa kufika kwenye tamasha hilo baada ya kugoma kuchukua usafiri wa awali aliokuwa ameandaliwa na NRG kutoka hotelini hadi kwenye uwanja huo.
Kama hiyo haitoshi, pia Wakenya hao walilalamikia kitendo cha waandaaji hao kuandaa vinywaji vya kutosha, hali iliyosababisha wengi wao kukosa vinywaji kwa kuwa viliisha.
“Waandaaji wamechemka kabisa, kila saa tunaambiwa na MC kuwa Burna Boy anapanda, matokeo yake anakuja kupanda asubuhi, halafu hamna vinywaji, wakati huohuo tayari Harmo tuliyehakikishiwa atakuwepo, lakini hayupo, huu ni uandaaji mbovu kabisa,” aliandika mmoja wa Wakenya katika Mtandao wa Twitter.
0 COMMENTS:
Post a Comment