DAR: Wakati wimbi la wasanii kujitosa kwenye siasa likiendelea, staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ huenda akakwaa kisiki baada ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mtwara kumweka kikaangoni, Gazeti la IJUMAA limedokezwa.
Hatua hiyo imekuja kutokana na msanii huyo kudaiwa kukiuka kanuni za uchaguzi CCM, kwamba, ameanza kufanya kampeni za chini kwa chini mapema pamoja na kujitangaza kuwa atawania ubunge kwenye Jimbo la Tandahimba, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Hatua kama hiyo pia inatarajiwa kumkumba Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (CCM), baada ya kutangaza hadharani kuwa atawania Jimbo la Tarime- Vijijini, hali iliyoulazimu uongozi wa CCM mkoani Mara kutangaza kumchukulia hatua za kinidhamu.
Harmonize au Harmo ambaye tayari ameonesha nia ya kuwania Jimbo la Tandahimba linaloshikiliwa na Katani Ahmed Katani (CUF), ndoto yake ya kuingia kwenye siasa ilipatiwa mwanga na Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ alipokuwa ziarani mkoani Mtwara, Oktoba 15, mwaka jana.
“Lakumalizia… nawapongeza sana waimbaji hawa akina baba, lakini nampongeza sana Harmonize, sijui anatoka jimbo gani, Tandahimba? Mbunge wa kule ni nani?…Aaa ningetamani kweli Harmonize akagombee kule akawe Mbunge wa Tandahimba,” alisema Rais Magufuli baada ya msanii huyo kutumbuiza katika ziara hiyo iliyofanyika mwaka jana.
Baada ya Rais Magufuli kuzungumza hivyo, Harmonize alisema anamshukuru kwa kuona mchango wake kwenye jamii na Mungu akipenda atagombea.
AANZA HARAKATI
Katika kile kilichoonekana kuanza kampeni kabla ya wakati, Oktoba 20, mwaka jana wakati anatambulisha mgahawa wake, Harmonize alisema atagombea nafasi ya ubunge jimboni Tandaimba.
Aidha, katika sherehe za kufunga na kuukaribisha Mwaka Mpya 2020, msanii huyo wakati akitumbuiza katika usiku wa sherehe hizo, alitangaza tena hadharani kuwania jimbo hilo.
Mbali na hivyo, pia amedaiwa kutumia kivuli cha umaarufu wake kama msanii, kutoa misaada kwa wananchi wa Tandahimba, jambo ambalo limeanza kutafsiriwa kuwa anawaandaa kisaikolojia wananchi ili wampe kura muda wa uchaguzi mkuu utakapowadia.
KAMATI KUAMUA HATIMA YAKE
Kutokana na hali hiyo, Gazeti la IJUMAA lilimtafuta Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Yusuph Nannila ambaye alisema suala hilo amelisikia hivyo atalifikisha kwenye vikao vya chama.
“Siwezi kuzungumza nje ya kikao, mimi kama kiongozi nazungumza kwenye kikao… kwa hiyo wewe kama unataka taarifa, subiri vikao vya kamati ya siasa, utapata taarifa.
“Tunafuata kanuni za chama kwenye vikao hivyo vya kimaamuzi, maamuzi ya wajumbe wa kikao kile, mimi kama mwenyekiti ndiye nitatolea tamko.
“Nikizungumza sasa hivi hayatakuwa maamuzi ya kichama, hayo yatakuwa maamuzi yangu Yusuf. Kama kuna watu watatoa ushahidi kuhusu kijana Harmonize, basi tutatoa muongozo,” alisema Nannila.
0 COMMENTS:
Post a Comment