ZAMA za sasa wachezaji wengi wamekuwa wakishindana kwa kudizaini na kuingia na mitindo tofuati ya nywele. Wapo ambao huzipamba nywele zao kwa mitindo tofauti, kuna wanaopenda kunyoa kawaida, vipara, kuweka dawa au kunyoa pembeni na kuacha nywele sehemu ya juu ‘kiduku’.
Lakini kuna miongoni mwao kuna wale ambao wamezifuga nywele zao na kutengeneza rasta ambapo idadi yao ni chache sana. Licha ya uchache huo wachezaji hao wanaweza kuunda timu kama wakikutanishwa sehemu moja.
Makala haya yanakupa chama la wachezaji wa Ligi Kuu Bara ambao wana rasta ambapo wanaweza kucheza na timu yoyote ile Bongo.
Kipa: Razack Abarola
Ni mali ya Azam FC ambayo amejiunga nayo zaidi ya misimu miwili nyuma akitokea kwao Ghana. Kipa huyu ndiye ambaye atakabidhiwa jukumu la kukaa katika milingoti kama ikitokea kikosi hiki kitakuwa pamoja, yeye rasta zake siyo ndefu sana.
Beki wa kulia: Azizi Sibo
Moja ya mabeki wa kulia ambao wamecheza kwa muda mrefu ndani ya Ligi Kuu Bara kwa sasa yuko zake Ndanda FC huu ni msimu wa pili mfululizo na kikosi hicho. Sibo atakula mbavu ya kulia katika kikosi hiki cha marasta ambapo yeye pia ana rasta fupi.
Beki wa kati: Yakub Mohammed
Kitasa hiki cha Azam FC kimekuwa msaada mkubwa sana katika kikosi hicho cha Aristica Cioaba, atakipiga katika nafasi hiyohiyo endapo tu ikitokea wachezaji wenye rasta wakaenda kikosi chao. Yakub raia wa Ghana ana rasta ndefu ambapo mara nyingi huzifunga wakati akiwa uwanjani.
Beki wa kati: Hassan Isihaka
Baada ya kupita Simba, African Lyon na Mtibwa kwa sasa Isihaka anakula maisha pale Kagera Sugar aliyojiunga nayo msimu huu. Isihaka atashirikiana vizuri na Yakub ndani ya kikosi hiki.
Beki wa kushoto: Yassin Mustapha
Mlinzi huyu ameufanya upande wa kushoto wa Polisi Tanzania uwe moto kutokana na kasi yake nzuri ya kupanda kusukuma mashambulizi na kukaba. Yassin ambaye msimu uliopita alikuwa Ndanda FC amefuga rasta ambazo zinaendelea kukua na anapokuwa uwanjani huzifunga kwa nyuma.
Kiungo mkabaji: Papy Tshishimbi
Mkongo huyu ndiye nahodha wa Yanga ambaye alitua klabuni hapo misimu miwili iliyopita akitokea Mbabane Swallows ya Eswatini. Tshishimbi ana rasta ndefu atakuwa mkabaji kwenye chama hili.
Kiungo mchezeshaji: Baraka Majogoro
Polisi Tanzania ndiyo klabu ambayo katika ligi ina wachezaji wengi ambao wana rasta wakiwa watatu. Kiungo Baraka Majogoro ni moja ya wachezaji hao watatu ambapo yeye rasta zake ni fupi.
Winga wa kulia: Salum Kihimbwa
Moja ya watu muhimu kwenye kikosi cha Mtibwa Sugar cha Morogoro. Anajulikana kutokana na rasta zake fupi ambazo amezisuka kwenda juu. Kihimbwa kwa sasa anasakwa na Yanga katika dirisha hili dogo.
Winga wa kushoto: Jafary Mohammed
Kiraka huyu ana uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani, ambapo ukiondoa jezi yake namba 23 kitu kingine kinachomtambulisha ni rasta zake ndefu.
Mshambuliaji: Awesu Awesu
Ingawa ni kiungo lakini ana uwezo mkubwa wa kucheza kama mshambuliaji ambapo kwa sasa yuko Kagera Sugar ya Kagera. Awesu ambaye alianza kuonekana akiwa Madini FC ya Arusha ana rasta ndefu huku pia akiwa mmoja ya watu muhimu katika kikosi cha Kagera.
Mshambuliaji: Hassan Nassor
Ukimuondoa Yassin na Majogoro, Nassor pia ni moja ya wachezaji wenye rasta ndani ya Polisi Tanzania, ambapo yeye ana rasta ndefu.
Winga wa kushoto: Awadhi Juma
Kiungo huyu huku nyuma ameshapita African Lyon na Njombe Mji ila kwa sasa yuko Mtibwa Sugar. Yeye ana rasta ambazo ameziweka kati pekee huku pembeni akiwa amenyoa.
Wachezaji wengine ambao wana rasta ambao wanaweza kuingia kwenye kikosi hicho ni Muharami Issa wa Yanga ana rasta ndefu, Francis Kahata wa Simba mwenye rasta ambazo amezifuga kati huku akinyoa pembeni na Kennedy Juma wa Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment