KAMA ulikuwa unawaza kuna mtu kwenye tasnia ya Bongo Fleva wa kushindana naye mpaka sasa, unajiongopea! Mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz ama Simba’, hakamatiki kwa kufuru ya pesa, anazitengeneza za kutosha, IJUMAA WIKIENDA linakujuza.
TUPATE HABARI KAMILI
IJUMAA WIKIENDA limechimba taarifa za ndani kutoka kwenye uongozi wa Lebo ya Diamond au Mondi, Wasafi Classic Baby (WCB) na kukutana na data zinazoonesha mwamba huyo anazidi kuzikusanya pesa nyingi ndani ya kipindi cha miezi saba ya 2020.
“Ana shoo nyingi sana za nje. Kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, ameshakuwa booked kwa takriban shoo 23. Hizo ni za nje, achana na zile zitakazojitokeza za ndani,” alieleza mtoa taarifa wetu ndani ya Lebo ya Wasafi.
SHOO ZENYEWE
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilijiridhisha kupitia orodha ya shoo hizo ambapo ratiba yake inaonesha imeanza tangu Januari 7, mwaka huu ambapo Mondi alikuwa Hurghada nchini Misri na Januari 11 alikuwa Lagos, Nigeria.
Listi inaonesha Januari 31, mwaka huu, Mondi atakuwa na shoo jijini Nairobi nchini Kenya, Februari 7-8 (Conakry nchini Guinea), Februari 15 (Naivasha nchini Kenya) na Februari 22 (Addis Ababa nchini Ethiopia).
Nyingine ni Februari 29 (Marekani), Marchi 6 (Zurich nchini Uswisi), Machi 7 (Copenhagen nchini Denmark), Machi 13 (Brussels nchini Ubelgiji), Machi 14 (Helisinki nchini Finland), Machi 28 (Dortmond, nchini Ujerumani), Aprili 3 (Marseille nchini Ufaransa) na Aprili 4 (Stockholm nchini Sweden).
Haijaishia hapo, Aprili 18 atakuwa Abidjan nchini Ivory Cost), Juni 1 (Antananarivo nchini Madagascar), Juni 6 (Reunion Island), Juni 7 (Majunga nchini Madagascar), Juni 12 (Ambanja, Madagascar), Juni 14 (Antalaha, Madagascar), Juni 19 (Comores Island), Juni 20 (Mayotte Island) na Julai 4 ni Amsterdam nchini Uholanzi.
KUINGIZA BILIONI 2.3
Kwa mujibu wa chanzo kutoka Wasafi, shoo hizo zinatofautiana kulingana na nchi na nchi ambapo wastani wa chini inaanzia shilingi milioni 100 na kuendelea.
“Inategemea nchi na nchi, lakini kimsingi shoo za Diamond nje ya nchi si chini ya shilingi milioni 100. Hii inatokana na gharama za uandaaji, kuna zile za viwanjani na zile za ukumbini, hivyo gharama hutofautiana kwa maana ya kuandaa majukwaa na mambo mengine,” alisema mmoja wa viongozi wa Wasafi.
MCHANGANUO ULIVYO…
Kwa mchanganuo wa harakaharaka, idadi ya shoo hizo ambazo tayari zipo ‘confirmed’ ni 23 hivyo ukizidisha kwa wastani wa shilingi milioni 100 kila shoo, maana yake kuanzia Januari, mwaka huu hadi Julai 7, Mondi atakuwa ameingiza shilingi bilioni 2.3 fasta tu.
KUFURU KAMA ZOTE
Taarifa kutoka Wasafi zimeeleza kuwa, mbali na mkali huyo kuingiza mkwanja huo ndani ya muda mfupi na kutunisha akaunti yake, yupo mbioni kuingiza mabasi ya kifahari (YouTom) yatakayofanya safari zake mikoani.
“Ni mabasi ya kifahari kwelikweli, si chini ya shilingi milioni 150 kwa moja, sasa unaweza kuona ni namna gani kijana anakwenda kuwa tajiri mkubwa mbali na miradi aliyonayo sasa,” kilieleza chanzo hicho.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimvutia waya meneja wa WCB, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ili kupata ufafanuzi kuhusu mradi wa mabasi hayo ambapo alipopatikana aliwataka mashabiki wa Mondi kuwa watulivu kwani mambo yapo mengi kwenye mipango.
“Mambo mazuri yapo mengi na yanakuja, hivyo subirini mtayaona. Ni suala la muda tu,” alisema Tale kwa kifupi.
UTAJIRI WA MONDI
Hadi mwaka jana, Mondi alitajwa kuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia shilingi bilioni 11 ambapo uchunguzi uliofanywa na IJUMAA WIKIENDA unaonesha kwamba mkali huyo anazidi kuchanua kimafanikio kwa mwaka huu, hivyo huwenda utajiri wake ukaongezeka zaidi.
CHANZO: IJUMAA WIKIENDA
0 COMMENTS:
Post a Comment